UKWELI NDIVYO ULIVYO: Akili zetu zimeisha kwa Morrison

Sunday October 04 2020
bm 3 pic

SOKA la Tanzania limejaa ubabaishaji mwingi. Limejaa mizengwe na kuendeshwa zaidi kwa mihemko na ushabiki kuliko misingi na kanuni. Kuanzia kwa viongozi waliopo ndani ya shirikisho mpaka kule kwenye vyama vya soka vya wilaya hadi mikoa wote wana kasumba ya aina moja.

Hata ukija kwenye ngazi ya klabu mambo ni yaleyale. Viongozi, wanachama mpaka mashabiki wanaishi kwenye kasumba hiyo ya kufanya mambo kishabiki kuliko uhalisi wa kusaka maendeleo ya klabu zao.

Kasumba ya Usimba na Uyanga imewavaa wadau kiasi cha kuwa tayari kupindisha kila kitu ama kusahau mambo mengine ili tu kuzitumikia klabu hizo mbili kongwe nchini.

Ndio maana haishangazi wakati mwingine kumkuta kiongozi wa Kagera Sugar au Ndanda kwenda kupiga kura katika uchaguzi wa Simba ama yule wa Toto Africans na Mwadui kushiriki mambo ya Yanga, licha ya klabu zao kuwa ndani ya ligi moja na vigogo hao. Hii inatoa picha gani? Ni kwamba Usimba na Uyanga ndio kila kitu na mengine yanafuata. Ndivyo ilivyo pia hata ndani ya Shirikisho la soka nchini (TFF).

Kwa hali kama hiyo huenda ni moja ya mambo yanayochangia kudumaza soka la Tanzania. Kwa miaka karibu 60 ya Uhuru wa nchi, Tanzania haijawahi kunyakua taji lolote la maana la kimataifa. Sio timu ya taifa, Taifa Stars wala klabu - wawakilishi wa nchi iliyowahi kurejea nchini ikiwa na ubingwa wa Afrika ama ule wa michuano ya klabu za soka Afrika kuanzia Ligi ya Mabingwa mpaka Kombe la Shirikisho Afrika.

Lakini sikiliza kelele zinazopigwa na mashabiki wa soka hususani wa Simba na Yanga. Kama ni mgeni kwao na pengine huzijui timu hizo kubwa na kongwe nchini unaweza kudhani ni zaidi ya Barcelona. Ni zaidi ya Bayern Munich na wakali kuliko PSG.

Advertisement

Viongozi wa klabu hizo akili zao zipo kwenye kutambiana wenyewe kwa wenyewe. Kufungana zenyewe kwa zenyewe kwenye derby na pia kunyang’anyana wachezaji, hususani wale wa kigeni. Mabosi wa TFF nao baadhi yao wanapoingia ndani ya shirikisho hilo akili zao zinawaza kuzibeba timu wanazozishabikia.

Utakataa nini? Angalia namna sakata la Bernard Morrison linavyowavuruga. Wakati wadau wengi wakiamini jambo hili limeisha, wiki hii tena sakata hilo limeibuliwa upya. Na ukifuatilia litawashughulisha watu hadi kusahau majukumu mengine.

TFF iliyotangaza mkataba mpya wa mchezaji huyo Mghana na klabu yake ya awali, Yanga kuwa una upungufu, leo inadaiwa kuhaha kuficha aibu ya kuruhusu mkataba wenye kusainiwa na upande mmoja kutoa leseni ya winga huyo kucheza Ligi Kuu msimu huu.

Yanga ambayo ilishakimbilia Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo (Cas), imeamua kuibuka na dai lao juu ya mkataba huo wa Simba na Morrison. Kuna mtu juzi kanipenyezea kwamba ule mkataba waliouonyesha Yanga ni halisi uliokubaliwa na TFF kutoa leseni ya Morrison, lakini swali je nani aliyeuvujisha kutoka ndani ya shirikisho hilo? Hapo ndipo utakapoona uadilifu wa watu waliopewa dhamana ya kuongoza soka la Tanzania ulivyo na dosari. Aliyevujisha kafanya kwa sababu ya unazi tu!

Tayari kuna taarifa za chinichini zisizothibitishwa, eti mabosi wa TFF wameshawapelekea upya Simba mkataba huo ili kujaza maeneo yaliyo wazi kwa nia ya kutaka kufunika kombe. Taarifa hizo zinadokeza kuwa, lengo ni kutaka kuja kuipiga KO Yanga siku watakapotangaza uamuzi wa malalamiko ya klabu hiyo juu ya mkataba huo.

Kama ni kweli hili linafanyika, basi ni wazi soka la Tanzania lina kazi kubwa ya kujikwamua mahali lilipo. Linahitaji kupata daktari mwenye taaluma ya hali ya juu ya kulitibu tatizo na ugonjwa unaolitafuna soka la Tanzania. Daktari ambaye ataweza kumaliza kansa ya unazi wa Usimba na Uyanga ndani ya taasisi ya soka hata kwa wadau wengine wa soka nchini. Ukweli ndivyo ulivyo.

Hata kama ni kweli Yanga, haina uhalali wa kuulalamikia mkataba huo kwa vile Simba na Morrison walishakubaliana mkataba wao uwe hivyo, lakini ni vipi TFF iliyokataa mkataba wa Yanga kwa madai una upungufu kwenye kusainishwa na tarehe waliridhia mkataba wa aina hiyo.

Ilikuwaje wakatoa leseni wakati mkataba haujakamilika wala kukithi matakwa ya kisheria na kikanuni kama wanavyofafanua wataalamu wa sheria?

Ukiangalia hilo na namna klabu kubwa zinazoshindana kumgombea mchezaji wa kigeni asiye na maajabu makubwa, ndipo tunapobaini kumbe soka la Tanzania linakwamia wapi?!

Yaani wakati klabu kubwa na TFF zikitakiwa kutafakari zifanye nini ili kuwatafuta na kuwaibua kama sio kuwaendeleza kina Mbwana Samatta wapya watakaoitangaza Tanzania anga za kimataifa, wenyewe wanamuwaza Morrison tu. Yanga inamlilia Morrison, hata kama inajua haitamtumia kikosini kwao. Simba inamtaka Morrison, licha ya kutambua ilifanya hila wakati wa kumshawishi kujiunga kwao. TFF nao wanatumia nguvu kubwa kuhakikisha Morrison anaenda kule wanakotaka wao na sio anakostahili kwenda, halafu eti tunataka soka la Tanzania lisonge mbele...Maweee!

Samatta aliyekuwa Ligi Kuu ya England (EPL) kwa sasa yupo Uturuki akikiwasha ndani ya klabu ya Fenerbahce. Ndio jicho la Watanzania kwenye anga za kimataifa hasa barani Ulaya, lakini umri unamtupa. Farid Mussa aliyetarajiwa kuwa mrithi wake alishindwa kule Hispania akaamua kurudi. Ni sawa tu na ilivyokuwa kwa Shaaban Idd Chilunda alichemsha kucheza Ulaya. Shomary Kapombe, Haruna Moshi ‘Boban’ na Thomas Ulimwengu nao walikwamia njiani. Umri wa Samatta unasonga mbele. Baada ya miaka michache huenda asiwepo tena kwenye soka la Ulaya na hata la Kitanzania. Hapo ndipo TFF na klabu zilipotakiwa kukaa chini na kutengeneza mipango ya kufikiria kina nani wanachukua nafasi ya Samatta mara atakapostaafu.

Lakini kwa vile wasimamizi wa soka la Tanzania wanafikiria zaidi mambo yenye kukuna nafsi zao kishabiki hawana mpango na ishu hiyo. Wenyewe wanakazana kuhakikisha klabu wanazoshabikia zinafanikiwa kunyong’onyesha wengine. Wanapambana kumpigania zaidi Morrison kutoka Ghana, kuliko kujua kina Samatta wapya watatokea wapi na kusaidiwaje waje kulibeba taifa mbele ya safari.

Wanasahau kama Morrison atafanya vurugu zake, huku Simba na Yanga zikichekana, lakini mwishowe atarudi kwao Ghana.

Jiulize tu, ni kweli Simba na Yanga zinamhitaji zaidi Morrison kiasi cha kushindwa kufikiria jambo jingine. Ni kweli Tanzania haina wachezaji wenye vipaji kuliko Morrison, kiasi cha kuwafanya mabosi wa klabu hiyo kupambana kuhakikisha wanakuwa naye kikosini?

Ni kweli pale TFF hakuna jambo la kujadiliwa zaidi ya kushughulikia suala la winga huyo Mghana? Nadhani ifike wakati wanaopewa dhamana ndani ya TFF na hata klabu za soka nchini, kufikiria mambo yatakayolisongesha soka la Tanzania mbele kuliko vitu vingine vinavyowadhalilisha hata kwa wageni.

Huenda Morrison anachekea mbavuni anavyoona Yanga, Simba na TFF zinavyoshughulika naye, kuliko kushughulika na mipango ya kutaka kulifikia angalau kidogo taifa lake la Ghana katika soka la Kimataifa.

Kama viongozi wataendelea kuishi kwa mazoea na kufikiria ndani ya boksi badala ya nje ya boksi sio ajabu Tanzania ikamakamilisha karne nzima bila kushuhudia timu yao ya Taifa ikifuzu Fainali za Kombe la Dunia na pia kushindwa kubeba taji lolote kubwa, huku Simba na Yanga zikizeeka bila kula sahani moja na klabu zenye umri nao sawa kama TP Mazembe na nyingine zinazotawala soka la Afrika.

Advertisement