Ukiona hizi pacha ujue kuna mabao

HAKUNA kitu kizuri kama kushuhudia kikosi chake kinakuwa na uwezo wa kufunga mabao katika kila mechi. Lakini, kitu kizuri zaidi ni kuona kwenye mamabo hayo yanapatikana kwa ushirikiano wa baadhi ya wachezaji kwenye kikosi unachokishangilia.

Kwenye Ligi Kuu England msimu huu kumeshuhudiwa wafungaji wengi wa mabao, lakini kuna pacha hizo zilihusika kwenye mabao mengi kwenye mechi za Ligi Kuu England msimu huu. Hizi hapa ndiyo pacha zilizohusika kwenye mabao mengi zaidi ya Ligi Kuu England msimu uliomalizika hivi karibuni.

5.Martial- Lukaku, mabao 6

Manchester United walifurahia msimu wao bora kwa mara ya kwanza tangu 2012/13 kipindi ambacho Sir Alex Ferguson ulikuwa mwaka wake wa mwisho kwenye timu hiyo na kuwapa ubingwa wa ligi. Kocha Jose Mourinho alifanya kazi nzuri na washambuliaji wake walifanya vyema pia. Straika Romelu Lukaku alifunga mabao 27 katika msimu wake wa kwanza baada ya kutua kwenye timu hiyo kwa uhamisho wa pesa nyingi akitokea Everton. Kwenye Ligi Kuu peke yake, Lukaku amefunga mabao 16 katika mechi 34. Katika mabao hayo, Anthony Martial alimtengenezea matatu, ikiwa ni sawa na ambayo yeye alimtengenezea pia staa huyo wa Ufaransa. Jambo hilo linawafanya wawili hao kuhusika kwenye mabao sita kwenye Ligi Kuu England. Pacha nyingine zilizohusika kwenye mabao sita ni Harry Kane- Son Heung-min huko Tottenham na Manuel Lanzini- Marko Arnautovic kwenye kikosi cha West Ham.

4.Salah- Firmino, mabao 7

Sadio Mane alimtengenezea Mohamed Salah mabao sita kwenye msimu wa Ligi Kuu England uliomalizika hivi karibuni. Staa huyo wa Misri, alitengenezewa mabao manne pia na fowadi wa Kibrazili, Roberto Firmino. Kwa upande wake Salah alimtengenezea Firmino mabao matatu katika ligi na hivyo kufanya kombinesheni ya washambuliaji hao wawili wanaotamba kwenye kikosi cha Jurgen Klopp kuhusika kwenye mabao saba. Hii ina maana kwamba fowadi ya wachezaji watatu kwenye kikosi cha Liverpool imeshirikiana vyema kabisa na ndiyo maana wametinga ndani ya Top Four na kwamba watakuwapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

3.Mane-Salah, mabao 7

Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England, Mohamed Salah amekuwa gumzo kwa msimu huu kutokana na huduma yake bora aliyotoa kwenye kikosi cha Liverpool. Staa huyo ameshinda kila tuzo zilizopaswa kutolewa kwa msimu huu na bila ya shaka atashukuru ushirikiano mzuri na mastaa wenzake Sadio Mane na Roberto Firmino. Wawili hao wamekuwa na ushirikiano mkubwa kwenye kweli, ambapo Salah na Mane pacha yao imeleta mabao saba kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Mane amemtengenezea Salah mabao sita, wakati Salah amemtengenezea Mane bao moja. Kwa pamoja fowadi hao wamehusika kwenye mabao saba.

2.Morata- Azpil icueta, mabao 7

Straika wa Chelsea, Alvaro Morata amefunga mabao 11 kwenye Ligi Kuu England tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Real Madrid kwenye dirisha la uhamisho wa wachezaji la mwaka jana. Katika mabao hayo, Cesar Azpilicueta amempigia asisti sita, wakati mshambuliaji huyo, Morata amesaidia beki huyo wa pembeni kufunga bao moja, hivyo wanafanya kombinesheni yao kuzalisha mabao saba. Ni jambo linaloshangaza kuona kwenye timu kombinesheni inayoleta mabao mengi inahusu mshambuliaji na beki. Kazi ya kutengeneza nafasi za mabao ni ya biungo, lakini kwa Chelsea mambo ni tofauti na Wahispaniola hao wawili wameonekana kushirikiana vyema uwanjani.

1.Mahrez-Vardy, mabao 7

Mashabiki wa Leicester City watakuwa kwenye sala nzima kuomba bao ambalo alifunga Jamie Vardy kwenye mechi dhidi ya Tottenham Hotspur baada ya asisti ya Riyad Mahrez haliwezi kuwa la mwisho la ushirikiano baina ya wachezaji hao wawili kwenye fowadi ya wababe hao wa King Power. Kilichopo kwa sasa, Mahrez anahusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Manchester City baada ya dili hilo kushindwa kutimia kwenye dirisha la Januari. Ushirikiano baina ya Mahrez na Vardy umeleta mabao saba kwenye kikosi cha Leicester City msimui huu ikiwa ni mengi zaidi kwenye Ligi Kuu England.