Ufaransa yaanza kwa sare ugenini

Munich, Ujerumani. Kocha wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, amewapongeza vijana wake kwa kupambana na kuambulia sare ya 0-0 dhidi ya Ujerumani, katika mchezo wa mashindano mapya ya Ulaya ‘Uefa's Nations League’.
Wakicheza mchezo wao wa kwanza tangu walipotwaa ubingwa wa Dunia katika fainali zilizofanyika nchini Russia, Julai mwaka huu, Ufaransa ilionyesha kiwango kizuri ikiwapa wenyeji wakati mgumu kila ilipofanya shambulizi.
Mshambuliaji Antoine Griezmann ndiye aliyepata nafasi nzuri zaidi ya kufunga kuliko zote zilizotengenezwa na Ufaransa hata hivyo kipa Manuel Neuer aliokoa kwa umahiri wake.
Kwa upande wa wenyeji kile kilichowafanya kuvuliwa ubingwa wa Dunia kwa aibu kiliendelea kujitokeza, kwani licha ya kuwa nyumbani na kufanya mashambulizi mengi hawakuwa makini katika umaliziaji, wakipiga vishuti vilivyodakwa kirahisi na kipa chaguo la pili wa Ufaransa, Alphonse Areola.
Baada ya mchezo huo Kocha Didier Deschamps, alisema amefurahi kuona vijana wake wamecheza kwa nidhamu na umakini wakiepuka makossa waliyoyafanya katika fainali ya Euro 2016 walipofungwa na Ureno.
Alisema katika mchezao ujao dhidi ya Uholanzi ambao watakuwa nyumbani watahakikisha wanapata ushindi nia ikiwa kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
Matokeo mengine ya mechi za mashindano hayo zilizofanyika jana ni: Jamhuri ya Czech 1 Ukraine 2, Wales 4 Ireland 1, Kazakhstan 0 Georgia 2, Armenia 2 Liechtenstein 1, Norway 2 Cyprus 0, Slovenia 1 Bulgaria 2, Latvia 0 Andorra na Gibraltar 0 Macedonia 2.