Udambwidambwi

Muktasari:

Makala haya yameangalia mwenendo wa ligi hadi sasa na kukuletea baadhi ya matukio yaliyojiri na kusababisha maumivu kwa timu, wachezaji na viongozi.

MWANZA.WAKATI Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kwa muda kupisha kalenda ya michuano ya kimataifa, tumeshuhudia matukio mbalimbali katika ligi hiyo.

Pamoja na ushindani ulioonyeshwa kwa timu shiriki lakini yapo baadhi ya matukio yalijitokeza kwa klabu, wachezaji na hata viongozi na kusababisha kwenda mapumziko haya mafupi kwa maumivu.

Hadi sasa tayari baadhi ya timu zimeshacheza mechi 14, huku Yanga pekee ndio ambao imecheza michezo michache (10) na kujikita nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26, sawa na Simba iliyoshuka uwanjani mara 11, huku Azam FC ikiongoza kwa alama 30 baada ya mechi 12.

Makala haya yameangalia mwenendo wa ligi hadi sasa na kukuletea baadhi ya matukio yaliyojiri na kusababisha maumivu kwa timu, wachezaji na viongozi.

VICHAPO KWA RUVU SHOOTING

Msemaji wao, Masau Bwire haishiwi na maneno, amejikuta katika wakati mgumu pindi timu yake iliporuhusu mabao mengi ndani ya mechi mbili dhidi ya Simba na Mtibwa Sugar.

Ruvu Shooting licha ya kuwa nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 16, itaendelea kuuguza maumivu ya kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Simba SC na kumfanya, Bwire kuondoka Uwanja wa Taifa kimya kimya.

Kama haitoshi timu hiyo baada ya kipigo dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, ilijikuta taabani tena mkoani Morogoro kwa kukung’utwa mabao 4-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

BIASHARA USHAMBA MZIGO

Pamoja na kutofungwa mabao mengi, lakini itakuwa ijiuliza ‘mzimu’ unaoiandama kwenye Ligi Kuu kwani imejikuta ikicheza mechi saba katika uwanja wa nyumbani bila kuonja ushindi.

Ipo chini ya Kocha Mnyarwanda, Hitimana Thiery imeshinda mchezo mmoja kati ya michezo 13 iliyocheza hadi sasa na kuzidi kuburuza mkia ikiwa na Pointi 10 na kusababisha mashabiki wake kutishia kutojitokeza uwanjani.

Licha ya kuwa na wachezaji wengi wazoefu na wa kimataifa, lakini matokeo yameendelea kuwa magumu kwenye Ligi Kuu na kuanza kutabiriwa kushuka daraja mapema.

AUSSEMS APOPOLEWA CHUPA

Pamoja na kwamba kwa sasa, Patrick Aussems ameweza kuwashawishi mashabiki wa Simba kutokana na matokeo mazuri wanayopata, lakini tukio la Septemba 20 katika Uwanja wa CCM Kirumba la kurushiwa chupa za maji halitasahaurika kichwani mwake.

Mbelgiji huyu alijikuta katika wakati mgumu baada ya klabu yake kudundwa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC, huku mashabiki wengi waliofurika dimbani hapo wakishindwa kuamini kilichotokea.

ALLIANCE YATIMUA MAKOCHA

Katika hali isiyo ya kawaida, Uongozi wa Alliance FC ilifikia uamuzi mgumu wa kuachana na makocha wake wawili, huku wengine wawili wakiwekwa kiti moto kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Ilikuwa ni kama sinema pale uongozi ulipobaki pekee kwenye benchi la ufundi wakati timu hiyo ikipepetana na bingwa mtetezi, Simba na kujikuta ikilala kwa kipondo kikali cha mabao 5-1.

Aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbwana Makata na msaidizi wake, Renatus Shija waliikacha timu kwa madai ya kuingiliwa majuku na uongozi kuamua kuwafyekelea mbali.

JOHN BOCCO YAMKUTA

Nahodha wa Simba SC, John Bocco alijikuta matatani baada ya kubainika kumpiga ngumi beki wa Mwadui, Revocatus Mgunga na kufungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000.

Hii ilikuwa ni msimu wa pili mfululizo kwa nyota huyo wa zamani wa timu ya Azam kuparuana na beki huyo kinda, ambapo msimu uliopita katika mechi yao mjini Shinyanga, Bocco aligongana naye na kushindwa kuendelea na mchezo.

Kamati ya uendeshaji na usimamizi ya ligi ilimuweka ‘mahabusu’ nahodha huyo wa Wekundu kwa kumfungia mechi tatu na faini ya Sh 500,000.

AFRICAN LYON YAKIMBIWA

Kutokana na Ligi Kuu msimu huu kutokuwa na udhamini na kusababisha klabu shiriki kuwa katika hali ngumu kiuchumi, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Lyon, Soccoia Lionel na Straika tegemeo, Victor Da Costa walishindwa kuhimili na kuamua kuikacha timu hiyo.

Ilikuwa ni mechi tisa tu sawa na dakika 630 ambazo walikaa ndani ya klabu hiyo, Lionel na Da Costa baada ya kuona hali si nzuri kiuchumi na kuamua kurudi kwao Ufaransa na kuiweka katika wakati mgumu Lyon.

Kuondoka kwao kuiifanya timu hiyo kuendelea kuwa kwenye hali mbaya kwenye Ligi Kuu kwani kati ya michezo 13 iliyocheza hadi sasa, imeshinda miwili, sare tano na kupoteza sita ambapo imevuna pointi 11 na kukaa nafasi ya 18.

SAKATA LA KMC NA HUMOUD

Katika hali ya kushangaza klabu ya KMC ilitangaza kuachana na kiungo wake, Abdulharim Humoud ‘Gaucho’ kwa madai ua utovu wa nidahamu ndani na nje ya timu.

Humoud ambaye aliisaidia KMC kupanda Ligi Kuu tena akiwa nahodha wa kikosi hicho lakini uongozi uliamua kutangaza kuachana naye tena kwa kumshushia tuhuma kibao zisizofaa, licha ya mchezaji huyo naye kuibuka na kukanusha vikali madai yaliyotolewa na uongozi.

Humoud alisema tuhuma hizo si za kweli na baadhi ya viongozi walihitaji rushwa kutoka kwake ili apewe nafasi ya kucheza na alipoonyesha kutokuwa tayari ndipo wakaanza kumzushia tuhuma mbalimbali.

KUULI KIFUNGONI

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) Wakili, Revocatus Kuuli alijikuta akifungiwa maisha kujihusisha na soka kwa kile kilichodaiwa kusambaza nyaraka za shirikisho hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Hamidu Mbwezeleni ilifafanua, Kuuli alikwenda kinyume na Katiba ya TFF kwa kusambaza barua aliyotumiwa na katibu mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidao ya kutoa maelezo ya kuingilia Uchaguzi Mkuu wa Simba.

Hata hivyo, Shirikisho la SokaTanzania (TFF) chini ya Rais, Walles Karia linapaswa kuangalia changamoto kubwa na kuzifanyia kazi ili soka letu liweze kuwa la ushindani na kusonga mbele. Pamoja na kuwapo kwa changamoto mbalimbali kwenye soka letu ikiwamo hali ngumu ya kiuchumi, lakini ni vyema maadili yakatawala ili kuendeleza soka letu na kufikia malengo. Tayari hadi sasa waamuzi na viongozi wa klabu mbalimbali wamekuwa wakihofia kila wanapoitwa kwenye kamati inayohusika na maadili kwa kuhofia kufungiwa kutokana na hali ya hewa ilivyotawala kwa kipindi kifupi ambacho Karia amekuwa madarakana na hii inaonyesha namna ya uongozi wake jinsi ulivyo.