UCHAMBUZI: Yanga yaandika rekodi

ILIPOIFUNGA Asas ya Djibouti kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kuna baadhi ya watu walisema imecheza na timu nyepesi. Hata ilipoitungua KMC kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa mabao 5-0 kuna waliosema Yanga haina kitu. Hata ilivyorudiana na Asas na kuipiga tena 5-1 kejeli ziliendelea kwamba Yanga imewapiga wanyonge.

Yanga haikujali ilitulia na kuwafumua maafande wa JKT Tanzania kwa mabao 5-0, bado kejeli zilizoendelea kwamba sio kipimo kizuri kwa mabingwa hao wa Bara na wana fainali wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Sasa unaambiwa jana ikiwa Kigali, Rwanda, Yanga iliuvunja mfupa ilioushindwa kwa muda mrefu kwa kuifunga Al Merrikh ya Sudan kwa mabao 2-0, huku wakiupiga mpira mwingi kwenye Uwanja wa Kigali Pele (zamani Nyamirambo).

Yanga ilipata ushindi huo ambao ni rekodi kwa klabu hiyo, kwani ilikuwa haijawahi kupata ushindi mbele ya wapinzani wao hao kwenye michuano ya CAF tangu mwaka 1973. Katika mechi nne za awali walizokutana kati ya 1973 na 2007, mara zote Yanga ilipigika ugenini na kung’olewa michuanoni baada ya sare ya nyumbani, lakini jana ikicheza kwenye uwanja wa nyumbani wa Wasudani hao ilionyesha msimu huu Wanaume hao wana jambo lao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi cha Kocha Miguel Gamondi kikicheza nje ya jiji la Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo ya CAF msimu huu, kiliwakimbiza wenyeji wao hao kutoka Sudan ambao waliuchagua Uwanja wa Kigali Pele kuwa wa nyumbani na kufungwa mabao hayo 2-0.

Matokeo hayo yameiweka Yanga kwenye nafasi nzuri ya kutinga makundi kwa mara ya kwanza tangu 1998 ilipocheza, ikiwa na maana kwa miaka 25 mfululizo timu hiyo ilikuwa ikihaha kucheza tena hatua hiyo, licha ya kufanya makubwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabao ya mtokea benchi Kennedy Musonda katika dakika ya 63 aliyemalizia friikiki ya Pacome Zouzoua na jingine na Clement Mzize aliyetumia vyema pasi tamu ya kisigino ya Stephane Aziz KI, yaliifanya Yanga kuizima Al Merrikh kwenye uwanja uliojazwa na mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.

Mashabiki kutoka jijini Dar es Salaam waliosafiri kwa mabasi zaidi ya 15 na wale waliopo Kigali na nchi jirani na Rwanda, waliifanya Yanga kuonekana kama ipo nyumbani kuliko wenyeji wao ambao licha ya kucheza kwa kutumia mipira mirefu na kusumbua ngome ya Yanga ilishindwa kufunga bao na kuendeleza rekodi ya kutofunga bao lolote kwenye mechi ilizocheza Kigali katika michuano hiyo ya CAF. Katika mechi yao ya raundi ya kwanza dhidi ya Otoho d’Oyo ilitoka suluhu baada ya awali kutoka sare ya 1-1 ugenini jijini Brazzaville na kufuzu hatua ya sasa kwa faida ya bao la ugenini.

Sare yoyote kwa Yanga kwenye mchezo wa marudiano Septemba 30 itaivusha kwenda makundi na kuwa historia kwa Gamondi ambaye jana hakumuweka hata benchi Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ tofauti na alivyoeleza akiwa jijini Dar es Salaam kwamba anaweza kumtumia baada ya kutoka kwenye majeraha.

Hata hivyo, haikufahamika kilichomfanya Skudu asiwepo kikosini, huku eneo la mbele akiwatumia nyota wake wenye kasi, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Mzize na Aziz Ki kisha kuja kumuingiza Hafiz Konkoni, Zawadi Mauya, Jesus Moloko na Musonda kipindi cha pili kuchukua nafasi za Mzize, Aziz KI, Pacome na Mudathir Yahya.


NINI KIFANYIKE

katika mchezo wa jana Yanga ilitengeneza nafasi nyingi ambazo kama ingezitumia ingepata mabao mengi zaidi, hivyo mechi ijayo ni lazima iwe makini kwa vile Al Merrikh itakuja Dar es Salaam ikiwa haina cha kupoteza kutokana na matokeo ya nyumbani.

Kwa mfano Mzize alikosa utulivu kabla ya kufunga bao la pili, huku pia alikuwa hatulii kwenye eneo lake kwa kuhamahama muda mrefu hadi alipotolewa kumpisha Hafiz.


MAXI NZENGELI

Ni mchezaji bora na mzuri na akipunguza kujiamini kwa kila anachokifanya uwanjani inaweza kuwa faida kwa timu kwani jana alikuwa ndiye aliyeushikilia mchezo wa Kigali kwa namna alivyoiendesha timu.


MATUMIZI YA KONA, FRIIKIII

Kocha Gamondi anapaswa kufanyika kazi eneo hilo, kwani jana aliyehusika kupiga mipira hiyo mara nyingi alikuwa ni Aziz KI, wakati mwingine hata kwenye maeneo ambao sio rafiki kwake.

Na kutaka kujua namaanisha nini, angalia friikiki za Pacome ilivyokuwa na faida kwa Yanga pale Musonda aliporuka kichwa na kufunga bao la uongozi kabla ya Mzize kuongeza la pili.


MECHI IJAYO

Mabao 2-0 ugenini ni mengi, lakini katika soka sio ya kuaminika kwani lolote linaweza kutokea, hivyo Yanga ijipange kuhakikisha hairuhusu bao lolote na badala yake ikomae ipate mabao zaidi ili itinge makundi.

Kwa jana Yanga ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu huku mabeki wakicheza kwa utulivu wakisaidiana na kipa Diarra Djigui ambaye aliwakatali washambuliaji wa Al Merrikh ambao mara ya mwisho ilipocheza na Yanga kwenye Kombe la Kagame 2011 ilitoka sare ya 2-2 hatua ya makundi.


Vikosi vya mechi ya jana;

AL MERRIKH: Almustafa, Mener, Karshoum, Bakhit, Rami, Tabanja, Alrashed, Wagdi, Altish, Brayan na Ramadan

YANGA: Diarra, Yao, Lomalisa, Bacca, Job, Aucho, Mudathir/Musonda, Pacome/Moloko, Mzize/Hafiz, Maxi na Aziz KI/Mauya.