UCHAMBUZI: Hata Morrison atatushangaa asipofungiwa

LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea kushika kasi kwa utamu na ushindani wa hali ya juu,kila timu haitaki kuleta masikhara mapambano ya kutafuta pointi tatu ni maubwa ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kusalia kwenye ligi.

Angalia mabao makali yanayofungwa. Tumeshuhudia mabao makali sana yakifungwa katika mechi nane hizi, lakini tumeshashuhudia matokeo ya kushtua kwa vigogo na hata timu ndogo hali ambayo inaleta tafsiri kwamba hakuna aliyeshindikana.

Ndani ya ushindani huo pia yapo matukio ambayo yamekuwa yakiibuka na kuleta msisimko na hata mshtuko kiasi cha kushangaza.

Pia kwamba kitu kama hiki kinawezaje kutokea kisha vikanyamaziwa mithili ya hakuna kilichotokea.

Narudia tena leo kwa mshambuliaji wa Simba Bernard Morrison ambaye bado anapambana kutafuta utulivu wa kuonyesha thamani yake ndani ya klabu yake mpya ya Simba ambayo ilimchukua akidaiwa kuwa huru akitokea Yanga huku klabu husika ikigoma na bado wanavutana kimyakimya.

Mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu Shooting Morrison alifanya kioja kingine alipompiga konde beki wa Ruvu mkongwe Juma Nyosso.

Hiyo ilikuwa ni baada ya tukio moja la kuumizwa kwa mchezaji mwenzake Luis Miquissone..

Tukio hilo lilisimamisha mpira kwa dakika kadhaa - kwa wachezaji kuanza kutaka kushambuliana kwa makonde kutokana na wale wa Ruvu kukerwa na kitendo kilichofanywa na Morrison na uwanja ulitibuka kwa muda kidogo.

Tukio lile lilinipa sura mbili kwamba bado wanaosimamia kanuni za soka na hata viongozi wenyewe wako nyuma katika kujua jinsi mpira wa sasa unavyoongozwa katika kuamua matukio ya namna hii ambayo yanaweza kuja kuleta shida kubwa wakati mwingine.

Sura ya kwanza ambayo naiona ni kwamba, sasa ni wakati muafaka kabisa kuona Morrison anafundishwa kwa kuadhibiwa ili makosa ya namna hii aachane nayo, kwani ni mara ya pili anafanya kitu kama hili la hatari katika soka.

Itakumbukwa Morrison alitangulia kufanya tukio kama hili akiwa Yanga akimpiga mmoja wa wachezaji wa Prisons ya Mbeya, lakini baadaye licha ya wanaosimamia mpira wa nchi hii kukimbiana mwisho alifungiwa mechi tatu na faini kwa kosa hilo.

Kuna wakati ilikuwa kama Morrison hatafungiwa tena, kwani alikuja kufungiwa wakati ambao watu na hata mchezaji husika inawezekana alishasahau alifanya kosa gani, mpaka adhabu hiyo ikamfikia na hakukuwa na ulazima wowote maamuzi hayo kuchelewesha ilikuwa bado ‘ujinga’ uleule wa siasa za soka.

Sasa mchezaji huyohuyo ameamua kurudia tena - tukio kama lile, lakini safari hii akatua kwa Nyosso ingawa bado amebaki katika timu za jeshi akifanya hivyo Jumatatu Oktoba 26 pale Uwanja wa Uhuru likiwa tukio la kushangaza kidogo.

Nasema la kushangaza kwa sababu Morrison tayari hakuwa na sababu ya kufanya kitu kama hicho kwa kuwa mwamuzi alishatoa faida kwa timu yake tena ya penalti. Kwa hiyo alipaswa kutulia na kujipanga kusawazisha bao lao hilo likiwa ndilo kitu muhimu.

Sioni ulazima wa siasa hapa kwani hata kama mwamuzi hakuona hilo ni sahihi sasa Kamati ya Saa 72 - kuliamua haraka tukio hilo - tena kwa kutumia marudio ya mkanda wa video kwa kumpa adhabu kali Morrison kwa kuwa anarudia tukio kwa mara ya pili katika misimu miwili tofauti.

Kumfungia Morrison ni kama kumsaidia kumkumbusha kwamba sasa anatakiwa kuacha tabia zake za ajabu kisha atulie afanye kazi ambayo Simba walivutiwa na kumsajili, kwani matukio yake yanaonekana hata kuwakera wachezaji wenzake na sasa kufanya kazi ya kumtuliza wakiwa uwanjani na mchezo ukiendelea.

Mwisho naona kuna haja ya waamuzi kumuangalia pia Morrison kwa kuwa inawezekana matukio ya namna hii yanatokana na kuchokozwa, ingawa bado inasimamia palepale kwamba bado mchezaji husika angekuwa anajielewa angetambua kuwa nidhamu ni muhimu.