Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tatizo yanga sio bao la mamelodi

Muktasari:

  • Ulikuwa ni wakati mzuri wa Tanzania kuwa na timu mbili kwenye michuano hiyo na kwa wapenzi wa soka kuona timu zao mbili zikishuka dimbani kila wikendi kimataifa.

Kama ulikuwa nje ya Tanzania, habari ikufikie tu timu kutoka Tanzania zilizoshiriki robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga zimetolewa kwenye michuano hiyo na kurudi nyumbani vichwa chini.

Ulikuwa ni wakati mzuri wa Tanzania kuwa na timu mbili kwenye michuano hiyo na kwa wapenzi wa soka kuona timu zao mbili zikishuka dimbani kila wikendi kimataifa.

Hata hivyo, wakati wenzetu wamekuwa wakiendelea kwa kujifunza kila siku wanapokosea, sisi tumechelewa kwa sababu ya kujisifia kila siku na kujipongeza tunaposhindwa.

Msimu uliopita Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini mapokeo ilikuwa ni kama Yanga katwaa ubingwa!

Simba amekuwa akiishia robo fainali mara nyingi tu ya michuano ya Afrika na ilikuwa ina furaha kwa sababu Yanga ilikuwa haifiki hatua hizo.

Msimu huu naona Simba haina raha licha ya kufika hatua ile ile.

Unajua shida ni nini? Ni rahisi tu. Yanga pia imefika huko na licha ya zote kutolewa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara inaonekana ilipambana zaidi kuliko Wekundu wa Msimbazi.

Yanga inabidi ijipange vizuri msimu ujao na kutokuona kama imefanikiwa tayari.

Haisaidii kuona imetolewa kwa sababu imeonewa.

Ni wakati wa kuangalia namna ya kukiongezea ubora kikosi chao ili msimu ujao mambo yawe mazuri zaidi kwani ni wazi haijaonewa bali kuna mahali ubora ulipungua.

Tujiulize, dakika 90 za Kwa Mkapa na 90 za Pretoria, Yanga kafanya nini hasa nyumbani? Hakuna kitu.

Ni wazi ilishindwa mechi ikiwa nyumbani kwani kwenye mchezo huo muda mwingi Mamelodi Sundowns ilitawala.

Ni wazi kama ingepata bao moja au mawili nyumbani, shughuli ingekuwa imeishia hapa hapa.

Hata hivyo, baada ya dakika ya 90 pongezi zikawa nyingi kwao kuliko kwa Mamelodi! Hapa ndipo tatizo lilipo kwenye soka letu.

Tunapenda kupongezana na kujipa faraja.

Kwenye mchezo wa marudiano, mambo yalikuwa ni yale yale, pamoja na kupaki basi, ilipata nafasi mbili za wazi na kushindwa kuzitumia, achana na bao la Stephane Aziz KI lililoleta utata pia kuna ya Clement Mzize.

Kabla ya mechi, zaidi ya asilimia 80 ya wadau wa soka walijua Yanga itatolewa na Mamelodi, ikawa hivyo ingwa ilitakiwa ipindue kauli zao na kufanya kweli.

Hata hivyo, tatizo kubwa linaloonekana Yanga ni ushambuliaji/ufungaji na pamoja na kuwa na viungo wazuri wanaofunga, lakini suala la kumpata mshambuliaji mzuri liko pale pale.

Ni wazi kama ingekuwa na mshambuliaji hatari kama Fiston Mayele msimu uliopita, uwezekano wa kumtoa Mamelodi ungekuwa mkubwa.

Tatizo lingine ni kwenye kupiga penalti. Hakuna mtu anayeamini timu za Tanzania zinaweza kusonga mbele inapofika hatua ya kupigiana matuta. Hapa ndipo vituko vipo.

Miaka ya karibuni, Simba ilitolewa kwenye hatua hiyo mara mbili kwa mikwaju ya penalti. Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika. Hili ni tatizo la kiufundi.

Naamini Yanga ingeweza kufuzu pia kwa mikwaju ya penalti na ilipoteza tatu za Dickson Job, Stephane Aziz KI na Ibrahim Bacca.

Hata hivyo, ingeweza pia kufuzu nusu fainali bila ya bao la Aziz KI lililokataliwa na mwamuzi kwani mechi ilikuwa wazi kwa Yanga.

Kuna mengi ya kujifunza kipindi hiki, tuache kuridhika, kujipongeza na kujifariji ili timu zetu zifike mbali.

 Timu zetu ziendelee kuwekeza kwenye mambo ya ufundi na Teknolojia. Hatuko pabaya sana. Tuachane na malalamiko ya kuhisi kuonewa kila siku.

Soka ni mchezo wa makosa kiasili, tupunguze kujilizaliza. Ni muda wa kuboresha timu zetu ili msimu ujao, Al Ahly na Mamelodi zisitoke kwa Mkapa.

Simba kuna mahali ilikuwa imesogea sana misimu minne ya nyuma. Sijui nini kimetokea, lakini imepungua ubora.

Ilikuwa na timu bora ya kusumbuana na Al Ahly. Sikuiona msimu huu wala msimu uliopita.

Tunahitaji kuiona Simba imara ikirejea. Ukitazama msimu hii miwili, Yanga imepiga hatua kubwa Kimataifa. Ni muda wa kuongeza nguvu kikosini na sio kujilizaliza Caf.

Mambo ya kusema Mamelod Sundowns na Yanga ni sawa, ni kujidanganya, Mamelodi iko mbali.

Wakati tukijipongeza kwa kutofungwa na Mamelodi ndani ya dakika 180 za nyumbani na ugenini, wao wanasikitika! Hii ndiyo tofauti yetu na wao.

Tunapaswa kubadilika.Tuache kupongezana, timu zetu zimetolewa kwa kukosa uwezo. Hakuna Sababu nyingine yoyote kubwa.

Simba kazidiwa uwezo na Al Ahly, Yanga katolewa na Mamelodi kwa kuzidiwa uwezo.

Tukikubali hilo na kujifunza, tutarejea tukiwa bora sana msimu ujao.

Soka ni mapambano ya Kiufundi, sio malalamiko. Nimeona Yanga imeandika  barua kwenda Caf kulalamikia bao lao kukataliwa. Sio jambo baya lakini halisaidii kitu msimu ujao kama Yanga haitaboresha timu. Kama Yanga ingekuwa na timu bora, hata baada ya bao kukataliwa, bado wangeweza kufuzu. Ukishakuwa na timu bora ni rahisi kubebeka. Yanga imekosa nafasi ya wazi kwa Mzize, imekosa penati tatu. Hapa utasema nini? Ubora. Ubora. Ubora.

Tuache kupongezana, Simba na Yanga rudini kutengeneza timu kwa ajili ya msimu ujao. Period!