UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ni uungwana kweli kuizomea TFF?

Muktasari:
WAPO watakaosema ndiyo, wapo watakaosema hapana. Kumekuwa na msuguano kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa muda mrefu sana, ni kama vile Yanga wanaona hawatendewi haki na uongozi huu.
WAPO watakaosema ndiyo, wapo watakaosema hapana. Kumekuwa na msuguano kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa muda mrefu sana, ni kama vile Yanga wanaona hawatendewi haki na uongozi huu.
Ni kama vile TFF inaona Yanga hawana shukrani, inasikitisha kuona wanachama wa Yanga wanamzomea Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, inasikitisha kuona uongozi wa Yanga umekaa kimya baada ya tukio lile, wikendi iliyopita Kidao alizomewa na wanachama wa mkutano Mkuu wa Yanga kwa madai ya kutoridhishwa na namna shirikisho linavyowakandamiza wao na kuibeba Simba.
Ni vigumu sana kumpata Mtanzania asiyefungamana na upande wa wowote wa ama Simba au Yanga.
Kidao ni moja kati ya watu waungwana sana, ni mmoja kati ya watu wanaopambana usiku na mchana kuupigania mpira wetu.
Yanga ni kama mtu asiyekuwa na pesa, mawazo yake siku zote yamekuwa ni kuona anaonewa tu, mawazo ya mtu asiye na pesa, siku zote ni kulaumu tu ndugu zake kwamba wamemtelekeza.
Hawamjali tena. TFF ni kama taasisi nyingine yoyote, wana mapungufu yao ambayo yanaletwa na mazingira yao ya kazi, kama Taasisi nyingine, kama Ofisi nyingine lakini, hatupaswi kufika huku.
Moja kati ya vitu vivyoongeza chuki kwa TFF ni Yanga kutokuwa na timu bora, ni Yanga kuukosa ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo, usipokuwa na timu bora kiwanjani, kila siku utawaona waamuzi wabaya, kila siku utaona unakwamishwa na TFF.
Kidao alialikwa kama mwakilishi wa shirikisho ambalo Yanga ni mdau wao, alipaswa kupewa heshima anayostahili, alipaswa kuheshimika, ilikuwa sawa kwa Yanga kuizomea TFF?
Nipe maoni yako kwa kuniandikia ujumbe mfupi kupitia namba ya simu hapo juu.
Kwa upande wa shirikisho nao hawapaswi kulichukulia poa suala hili, kuna haja ya kujitathimini, kuna picha inajengeka haiwaweki kwenye hali nzuri.
Yanga wanaona kama Shirikisho linawazingua, wanaona wanakandamizwa na mifano ipo. Kitendo cha Afisa Habati wa Yanga, Hassan Bumbuli kufungiwa kujihusisha na soka halafu, baadaye akashinda rufaa ni kuonyesha kuwa kifungo cha awali kilikuwa na walakini.
Kitendo cha Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kufungiwa kujihusisha na soka kwa miaka mitano, halafu baadaye kushinda rufaa yake nayo inaonyesha hawa watu wanaonewa kwenye maamuzi.
TFF wasichukulie poa sarakasi hizi, kazi kubwa ya kudumisha mahusiano ni lazima ifanyike, timu zinazofanya vizuri duniani kote, huwa zinaonekana kama zinabebwa, wakati Manchester United ya Sir Alex Ferguson inafanya vizuri, kila mtu aliamini kuwa walikuwa wanabebwa.
Imewatokea Manchester City, imetokea FC Barcelona, imetokea Real Madrid, ikitokea pia kwa Yanga enzi za Mwenyekiti Yusuf Manji, ndiyo tabia ya timu bora.
Yanga wanahitaji kuimarisha timu, ukishakuwa na timu bora, inapunguza lawama kwa Shirikisho na unapunguza lawama na Waamuzi.
Shirikisho wanafanya kazi kubwa ya kuipigania Yanga ikiwa ni pamoja na kuwakopesha mpaka pesa kabla ya GSM kuanza kusaidia, lazima Yanga wawe waungwana, lazima wawe na utu.
Kidao amekuwa mstari wa mbele kupigania klabu zetu kusonga mbele, ilikuwa sawa kweli kwa Wanachama wa Yanga kumzomea Kidao? Nipe maoni yako kwa kuniandikia ujumbe mfupi kupitia namba ya simu hapo juu. Zinedine Zidane aliwahi kuzomewa na mashabiki wa Real Madrid pale Estadio Santiago Bernabeu, Cristiano Ronaldo aliwahi kuzomea kwenye Dimba hilo na mashabiki hao hao.
Wote hawa wawili wameondoka kama wafamle ndani ya klabu hiyo, unajua walichokifanya? Walicheza mara mbili, waliupiga mwingi sana, walifanikiwa kuwaziba mdomo mashabiki waliowadharau na kuwatusi.
Hiki ndicho ambacho Kidao na TFF yote kwa ujumla wanachotakiwa kufanya, kuendelea kufanya kazi nzuri, kuidisaidia Yanga, kuendelea kuwashauri kuelekea mchakato wao wa kubadili muundo wa uendeshaji wa klabu yao.
Msimu wa 2020/21 unaelekea ukingoni na imani yangu ni, msimu ujao Yanga itakuwa imeimarika, watapunguza malalamiko na maisha mengine yataenda, ukishakuwa na timu ya uhakika, lazima utapunguza malalamiko. Kuna makosa yanafanyika ya kawaida sana kwa Simba, kuna makosa yanafanyika ya kawaida sana kwa Yanga, huwezi kusema kuna timu inapendelewa, nikufurahi kuona Yanga wamekubali kubadili mfumo, walau utasaidia kuwa timu bora. Walau wataweza kushinda bila kudhani kama wanaonewa, kuna tofauti kubwa sana kati ya mtu aliyefanya kosa na aliyependelea.
Kidao ni moja wa vijana wanaochapa kazi kweli kweli, pamoja na kunasibishwa na Simba lakini, ni moja kati ya watendaji waadilifu, hakustahili kukutana na tabu ile, alistahili zaidi heshima.
Kwa mabadiliko waliyoanza kufanya Yanga, bila shaka yoyote timu inakwenda kuimarika, Taasisi mpya inakwenda kujengwa.
Wana mifumo ambayo ukiitazama kwenye makaratasi, utakubaliana na mimi kuwa Yanga inakwenda kuzaliwa upya.
Kumzomea Kidao haifanya Yanga kuwa bora, timu bora hupunguza malalamiko, haya wanayopitia Yanga kwa sasa, Simba pia walipitia.
Watu walifika mahali hadi wakafanya kitendo kiovu cha kung’oa viti uwanjani, unaijua sababu? Ni rahisi tu, Simba hawakuwa na timu nzuri ya kushindana, Simba walikuwa wakali kama Pilipili. Ndiyo mpira ulivyo, kuna muda unakuwa na timu nzuri na kuna wakati unachekesha tu.
Viongozi wa Yanga wasikae kimya tu, inabidi watoke hadharani na waseme mema wanayotendewa na TFF, hiki kilichotokea hakina afya kwenye mpira wetu, mahusiano mazuri kati ya timu na shirikisho ndiyo yanayojenga msingi wa kuwa na ligi bora.
Ni sawa kweli kwa Wanachama wa Yanga kuizomea TFF? Nipe maoni yako kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwa namba yangu ya simu hapo juu.
Imeandikwa na OSCAR OSCAR