Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Hiki hapa kinachowapa kiburi Yanga kwa Mamelodi

Muktasari:

  • Kama ni presha wameshapitia. Wana kiburi kwa sababu timu wanayo. Hawana hofu. Kwa kifupi, wamejipata.

YANGA ina kiburi sana. Ndicho unachoweza kusema kwa sasa. Mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns ilikuwa dume, nini utawaeleza Yanga. Walishacheza na vigogo wa Afrika karibu wote.

Kama ni presha wameshapitia. Wana kiburi kwa sababu timu wanayo. Hawana hofu. Kwa kifupi, wamejipata.

Baada ya sare na Mamelodi, miamba hiyo ya Afrika Kusini imeanza kubezwa. Wengi walijua Yanga itafungwa mabao mengi. Hata hivyo, ikawa tofauti, Yanga imetengeneza timu ambayo inaweza kucheza popote na timu yoyote na kupata matokeo mazuri.

Hapa ndipo kiburi chao kilipo. Mamelodi ni klabu inayoendeshwa kisasa. Haina fitina za Kiswahili wala mauzauza ya Kiafrika. Imewekeza pesa nyingi sana kwa wachezaji na miundombinu ili ishinde mechi ndani ya dakika 90.

Ubora wa Yanga umeifanya kwa kiasi kikubwa ionekane ni ya kawaida Jumamosi Kwa Mkapa! Kiuhalisia Mamelodi sio timu ya kawaida. Ni moja ya timu bora Afrika isipokuwa imekutana na Yanga kiburi. Yanga jeuri. Yanga dume kweli kweli.

Soka letu linaenda pazuri na ndani ya miaka mitano tutakuwa mbali sana. Naona tumeanza kuusogelea ubingwa wa Afrika. Uwekezaji wa wachezaji na makocha kwenye timu zetu hasa Simba na Yanga ni wa hali ya juu. Tunakula sahani moja na miamba ya soka Afrika na tuna kiburi cha kushindana nao uwanjani.

Saa moja kabla ya kuachiwa kwa kikosi cha Yanga kitakachoanza kwenye mchezo huo wa Jumamosi, mijadala ilikuwa mingi na wengi waliamini Mabigwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara itapoteza kwa sababu majina makubwa matatu ya wachezaji wa kikosi hicho hayakuwemo, Daktari Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Yao Kwasi.

Wachezaji hao kwa sasa ndio mhimili mkubwa kwenye timu. Ndio kipenzi cha mashabiki. Hata hivyo bila ya uwepo wao, Yanga ilikuwa salama chini ya Dickson Job, Kennedy Musonda na Jonas Mkude waliochukua nafasi zao.

Hakuna ubishi Yanga ingeanza na wachezaji hao watatu, huenda ingeshinda. Kukosekana kwao si jambo dogo. Hata hivyo, Kocha Miguel inabidi abadilike. Ana wachezaji wengi wenye ubora, lakini amekuwa akiwatumia wachache.

Ni muhimu kuwapa nafasi wote ili inapotokea dharura kila mmoja awe fiti kuipigania timu. Kiwango alichoonyesha Mkude Jumamosi sio wa kumweka benchi kila siku. Ufundi wa Augustine Okrah sio wa kuuweka benchi kila siku. Wanapaswa kupewa walau dakika 25 uwanjani kila mechi.

Wapo pia wengine wenye ubora kama Kibwana Shomary. Alikuwa tegemeo chini ya Kocha Nasreddine Nabi, lakini kwa Gamondi, amekuwa mtu wa benchi kila siku.

Nadhani anahitajika kupewa walau dakika chache kila siku uwanjani kwani bado ni kijana mdogo kukaa benchi kunamshusha kiwango.

Farid Mussa yuko pale. Tangu atoke Hispania, sidhani kama ametumika sawa sawa. Ni fundi kweli kweli wa boli. Kocha Gamondi anapaswa kuongeza ukubwa wa kikosi chake kwa kutengeneza balansi nzuri katı ya wachezaji wanaoanza na wa akiba.


MECHI YA SAUZI

Iko wazi kwa yeyote. Mamelodi ina ubora karibu kila eneo na ni wazi itakuwa tofauti sana ikiwa nyumbani, huku kwa Yanga inahitaji kuwa bora hasa eneo la kiungo na ushambuliaji.

Mechi ya ugenini inahitaji kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kutumia nafasi chache kikamilifu. Sundowns haitoruhusu Yanga itawale mchezo. Muda mwingi Yanga itatakiwa kuzuia mashambulizi. Hakuna kitu kigumu kwenye soka kama kucheza bila mpira. Hii ndiyo shughuli kubwa Yanga inatakiwa kuifanya.

Tangu msimu uliopita Yanga imekuwa ikijua namna ya kucheza mechi za ugenini na imeshinda takriban mechi sita za ugenini mfululizo kabla ya kufungwa na CR Belouizdad na Al Ahly.

Mpangokazi wa mechi ya Afrika Kusini lazima uwe tofauti. Mamelodi ni timu yenye uwekezaji mkubwa sana wa wachezaji na miundombinu lakini hata wao bado sio wafalme wa Soka la Afrika.

Ni mabingwa mara moja tu wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu ngumu na bora Afrika zinabaki ni Al Ahly, Zamalek na TP Mazembe. Sina maana Mamelodi ni wepesi, nazungumzia mataji ya Afrika.

Moja ya faida inayopata Yanga ni kutoruhusu bao la nyumbani. Mechi za mtoano na hasa kwenye kanuni ya bao la ugenini, ni dhambi kubwa kuruhusu bao ukiwa nyumbani.

Unampa faida kubwa sana mpinzani wako. Yanga ikipata bao ugenini, itawapa ugumu sana Mamelodi. Bado naona mechi ya pili ikiwa wazi sana kwa timu zote mbili.

Gamondi ndiye atakayeiamua mechi. Nasubiri sana kuona kikosi chake cha kwanza, atakavyokuwa amefanya mabadiliko ya wachezaji. Amekuwa mzito sana kwenye mabadiliko. Mechi kama hizi zinataka sana uharaka wa maamuzi.

Zinataka mtu mwenye uwezo wa kuusoma mchezo haraka sana.

Mamelodi haina muda wa kupoteza. Sio waarabu wale. Ina ubora na kasi na inataka mpira utembee. Ukiingia kwenye mfumo, unaweza kula hata bao tano pale.

Gamondi ni lazima awe na mikakati haswa ya mechi ya ugenini. Naona baada ya mechi şifa nyingi sana zimeenda kwa Yanga lakini haijaisha hadi iishe. Mechi ya pili itakuwa tofauti sana!

Hakuna kitu kinachanganya kwenye soka kama kufungwa bao la mapema.

Mipango mingi huanza kupotea hapo na kujikuta mnakuwa watumwa mechi nzima. Mamelodi itataka sana kupata bao la mapema ili kushusha presha.

Tayari kiwango cha Yanga kitakuwa kimewashtua na hasa inapoona imecheza na Yanga iliyowakosa pia nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza.

Kocha wa Mamelodi, Rulani Mokwena anaonekana kuijua sana Yanga, kila mchezaji na ubora wake.

Ukimsikiliza kwenye mahojiano aliyofanya kabla ya mechi, ameeleza mazuri mengi ya kila mchezaji wa Yanga lakini hakusema chochote juu ya mapungufu yao.

Huo ni mtego. Kama anajua ubora wa kila mchezaji na tunakubaliana nae, basi kuna namna anajua pia mapungufu yao. Mpira upo kwa Gamondi, mimi tayari nipo kwenye Kideo nasubiri Shoo!