Tyr Again: Wanaongoza Ligi kwa baiskeli ya mbao, tutawapita

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again'  alipokuwa akizungumza na wanachama wa klabu hiyo leo katika mkutano mkuu wa Simba.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' amesema nia na uwezo wa klabu yao kutetea ubingwa wanao.

Amesema wale waliotangulia kwenye msimamo ni sawa na baiskeli ya mbao, Simba itawapita na kutwaa ubingwa wa msimu huu kwa mara nyingine.

Huku akishangiliwa kwa nguvu na wanachama waliojitokeza kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo, Try Again amesema uwezo wanao wa pesa pia wanazo.

"Tunayo jeuri kwa kuwa tumewekeza katika mpira, sio kwenye kejeli, fitina na vijembe, huko tuneshatoka hii ni next level," ametamba Try Again.

Amesema kwenye klabu 10 bora Afrika Simba imo, huku akihoji upande wa pili ni ya ngapi Afrika huku wanachana baadhi wakijibu kwa utani kuwa ni ya 80.

"Kwenye Ligi mmeona juzi jinsi tulivyocheza Mwanza, sisi ni tik tak hao wanaoongoza tutawapita kama wamesimama na watashangaa, amesema Try Again.

Amesema klabu yao imewekeza kwenye mpira, na bado wamo kwenye Afrika (Simba inashiriki FA baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa).

"Sisi ndiyo wenyeji Novemba 28 Simba utacheza na Red Arrows ya Zambia na tutawapiga, mipango na mbinu zote tunazifahamu," amesema.

Amewaomba wanachama kushikama kwenye mchezo huo wa mtoano wa FA utakaofanyika kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam kabla ya marudiano nchini Zambia Desemba 5.

Huku akiwakebehi watani zao Yanga kuwa hawajalala tangu jana baada ya mechi za mzunguko wa raundi ya sita, Try Again amesema timu yao itafanya vizuri nchini na kwenye FA watafika mbali.