Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tukijiuliza maswali haya tutaacha ujinga wetu, tutaamua

Muktasari:

Baadaye, Pele alikaririwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa hatimaye kupitia kwa Lamptey alikuwa mchezaji wa soka mwenye kipaji kama chake au zaidi yake. Alidai kwamba Lamptey ndiye aliyekuwa mrithi wake sahihi katika soka.


NII Oderty Lamptey. Wachache wanamkumbuka staa huyu wa Ghana. Aling’ara katika michuano ya Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 17 pale Glasgow Scotland. Aliyeshangazwa zaidi na kipaji chake alikuwa Mfalme wa soka duniani, Pele.

Baadaye, Pele alikaririwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa hatimaye kupitia kwa Lamptey alikuwa mchezaji wa soka mwenye kipaji kama chake au zaidi yake. Alidai kwamba Lamptey ndiye aliyekuwa mrithi wake sahihi katika soka.

Unadhani Lamptey alifika wapi? Hakufika popote. Alihama timu moja kwenda nyingine bila ya mafanikio. Mwishowe akasingizia kwao Ghana alikuwa anarogwa. Lakini ukweli ulibaki mmoja tu. Alikuwa amedanganya umri kwa umri mwingi sana. Wakati Pele akimsifia yeye kama kinda, kumbe alikuwa anapitisha miaka 30.Si yeye tu. Ghana ilikuwa inatesa katika soka la vijana kupitia kizazi cha kina Lamptey ilikuwa haijawahi kupata mafanikio. Baadaye Waghana wakajiuliza, ‘huu ujinga wa kudanganya umri kwa miaka mingi unatusaidia nini?’.

 Wakaweka nia ya kuachana nao. Mwishowe ni kweli wakapunguza kudanganya umri. Baada ya kufanya hivyo tu, Waghana wakavuna kizazi ambacho kilikwenda Kombe la Dunia 2006, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia yao. 

Hii ni baada ya vizazi vya kina Abeid Pele, Frank Amakwah, Charles Akunnor, Tony Yeboah na wengineo kushindwa kufikia hatua hiyo.

Tulipofika, Tanzania inabidi tujiulize swali kama hili katika jumla yake. Mambo mengi ya ovyo ambayo tunayafanya kwa sasa katika soka letu, yanatusaidia nini? Afadhali wao Waghana walijiuliza katika swali moja, sisi inabidi tujiulize katika maswali mengi.

Tunapanga matokeo dhahiri, waamuzi wanahongwa katika mechi za Ligi Kuu dhahiri, tunapanga ratiba za upendeleo dhahiri, tunazuia wachezaji wetu kucheza nje wakipata timu na mashabiki wanashabikia dhahiri, waandishi wamegeuka kuwa wapambe wa klabu fulani dhahiri, mabosi wa TFF wana timu zao za daraja la kwanza na za Ligi Kuu dhahiri, haya yote yatatusaidia nini? Kioo cha yote haya tunakipata kupitia katika timu ya taifa. Tujiulize, upuuzi wote huu ambao tumeufanya kwa miaka nenda rudi umesaidia nini timu ya taifa ya Tanzania? Huku katika klabu tunafahamu kuwa hakuna kitu, je katika Timu ya Taifa ya Tanzania imesaidia nini?

Tumewahi kwenda Kombe la Dunia? Tumewahi kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika baada ya mwaka 1980? Kuna timu yetu imewahi kufika walau nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa au Shirikisho? Kama hali ni hii, basi tulifuate swali na jibu la Waghana. Wao walijiuliza katika swali moja, sisi tujiulize katika maswali mengi.

Kama yote haya yanayoendelea hayataweza kubadilika, basi njia moja kubwa ya kuupa mafanikio mchezo wa soka nchini ni kuchukua vijana wengi na kuwaweka katika shule za soka za klabu mbalimbali kubwa na ndogo kule Ulaya. Baadaye tutawavuna tu.

Kwa mfumo huu ambao tunaendelea nao, kumpata Mbwana Samatta mwingine itachukua miaka 30 mingine. Bahati mbaya zaidi ni kwamba sioni kama ligi yetu ya ndani kwa hali ilivyo inaweza kututengenezea timu ya taifa itakayokuwa imara kuliteka Bara la Afrika. Tumejaribu hivyo kwa miaka nenda rudi na imeshindikana.

Sana sana kinachoendelea kwa sasa ni kuanza kuzitengenezea timu nyingine za taifa vikosi imara hasa wale majirani zetu. Kama ambavyo Burundi na Rwanda zimekuwa zikiimarika kwa wachezaji wao kucheza nchini miaka ya karibuni lakini tukikutana nazo wanatudhuru kama kawaida.

Mataifa ya Afrika Magharibi nayo yana matatizo makubwa katika uendeshaji wa mpira. Kikubwa kinachowabeba ni kiu ya wachezaji wao kutaka kucheza nje ya mipaka yao. Baadaye wanarudi kuwakilisha mataifa yao na inaonekana kama vile wana mipango mizuri katika soka kumbe hakuna.  Kama soka la Afrika lingekuwa linapimwa kwa mipango ya ndani hapana shaka timu za Afrika Magharibi zingekuwa nyuma sana. Lini ilikuwa mara ya mwisho kwa timu ya Afrika Magharibi kuchukua ubingwa wa Afrika? Hauwezi kukumbuka kirahisi.

Pia angalia katika michuano ya Chan iliyomalizika hivi karibuni Rwanda, ndiyo utapata kioo halisi cha jinsi ambavyo katika soka la ndani, soka la Afrika Magharibi limekuwa likiendeshwa kwa ubabaishaji na kinachowabeba ni wachezaji wao walioondoka kwenda Ulaya wanapocheza timu za wakubwa.  Tulipofika inabidi tuamue kufanya kitu. TFF ya rafiki yangu Jamal Malinzi inaturudisha nyuma zaidi na sioni kama tunaweza kusonga mbele kiurahisi.

Maswali yanakuwa mengi zaidi kuliko majibu. Inabidi tuamue kuachana na kila ujinga tunaoufanya au tuchukue chaguo la pili la njia ya mkato.

Kinachokera  ni kwamba sioni hata kama tunaweza kujibu swali kama hili ambalo Waghana walikuwa wamelijibu na wakasonga mbele.