Prime
Simba yaonyesha ukubwa Morocco

Muktasari:
- Simba itavaana na Berkane ikiwa ni mechi ya tatu kwa kukutana katika michuano hiyo ya Shirikisho, kwani awali zilikutana katika makundi msimu wa 2021-2022 na kila moja kushinda nyumbani, timu ya Morocco ikianza kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 kisha Wekundu kulipa kisasi kwa 1-0 Kwa Mkapa.
CASABLANCA: SIMBA haijasafiri kinyonge kutoka Dar es Salaam kuja hapa Casablanca, Morocco ambako itakaa kwa muda kisha kwenda Berkane ambako Jumamosi ya Mei 17, 2025 itashuka Uwanja wa Manispaa ya mji wa Berkane, kuvaana na RS Berkane katika mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba itavaana na Berkane ikiwa ni mechi ya tatu kwa kukutana katika michuano hiyo ya Shirikisho, kwani awali zilikutana katika makundi msimu wa 2021-2022 na kila moja kushinda nyumbani, timu ya Morocco ikianza kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 kisha Wekundu kulipa kisasi kwa 1-0 Kwa Mkapa.
Na sasa timu hizo zinakutana wikiendi hii, huku Simba ikitua Casablanca ikiwaonyesha ukubwa wa timu hiyo katika msafara ulioambatana na timu hiyo.
Msafara wa umejumuisha makundi na aina tofauti za watu jambo linaloashiria kwamba Simba imepania kupata matokeo mazuri katika mchezo huo dhidi ya Berkane.
Serikali imewakilishwa vyema katika msafara huu wa Simba ambapo kiongozi aliyepewa dhamana ya kuongoza msafara huo ni Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ambaye ameambatana na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo.
Ikumbukwe pia Mwana FA ndiye aliongoza msafara wa Simba katika mechi ya marudiano ya hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini iliyochezwa jijini Durban ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana ambayo iliifanya Simba isonge mbele kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0.
Ni zaidi ya watu 230 ambao wamesafiri kutoka Dar es Salaam kuja hapa Morocco na katika kundi hilo kuna viongozi wa timu, wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi, mashabiki, waandishi wa habari, maofisa wa klabu na wanasiasa.
Upande wa uongozi, kundi kubwa la wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Simba lipo kwenye msafara huu likiongozwa na makamu wa Rais wa Bodi na mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.
Simba imejumuisha pia idadi kubwa ya maofisa wa sekretarieti yake wanaoongozwa na ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Zubeda Sakuru na msaidizi wake Belinda Paul na upande wa kikosi kipo chini ya kocha mkuu Fadlu Davids na ni wachezaji wawili tu ambao hawajasafiri na timu nao ni Aishi Manula na Hussein Kazi.
Baadhi ya wadau wakubwa wa Simba ambao wapo kwenye msafara huu ni mfadhili wake wa zamani, Azim Dewji, wenyeviti wa zamani Salim Abdallah ‘Try Again’, Hassan Dalali ‘Field Marshall’ na Swedi Nkwabi huku pia wakiwepo makatibu wa zamani wa Simba, Kassim Dewji na Hassan Hassanoo.
Kuna zaidi ya mashabiki 100 ambao wamesafiri kuja na Simba hapa Morocco na baadhi maarufu ni Swalehe Madjapa, King Faida, Kisugu, Kay Mziwanda na Baby Mary Simba.
VIGOGO SIMBA WAMSHUKURU RAIS SAMIA
Wadau mbalimbali wa Simba waliosafiri na timu hiyo kuja hapa Morocco kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane, Jumamosi, Mei 17 wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ndege iliyosafirisha msafara wa timu hiyo.
Mfadhili za zamani wa Simba, Azim Dewji alisema; "Mama amefanya mambo makubwa kwa klabu yetu na tunamshukuru sana. Ukianzia katika hamasa ya goli la mama na sasa ametupatia ndege yote ni kuonyesha mapenzi kwa sisi wanae. Nawaomba Wanasimba tuendelee kumuombea Rais wetu.”
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu amesema; "“Kutupatia ndege hii ambayo imebeba kundi kubwa la watu ni jambo ambalo limekuwa na msaada mkubwa kwetu na kwa namna ya kipekee klabu ya Simba inatoa shukrani kubwa na za dhati kwa Mheshimiwa Rais. Dhamira yake ya kuendeleza michezo iko wazi na kiukweli anastahili maua yake.”
WACHEZAJI, MAKOCHA KWANZA
Wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Simba wanaonekana kupewa kipaumbele cha kwanza katika kila kinachofanyika safarini.
Kabla ya kuondoka hadi ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mohammed V hapa Casablanca, Simba imehakikisha maofisa wake wa benchi la ufundi na wachezaji hawapati changamoto inayoweza kuwaathiri kisaikolojia katika maandalizi yao ya mchezo dhidi ya RS Berkane, Jumamosi Mei 17, 2025.
Wakati timu inajiandaa kuondoka, wachezaji na benchi la ufundi la Simba ndio walitangulia katika ukaguzi wa hati za kusafiria na baada ya hapo wakafuata viongozi wa serikali, viongozi wa klabu na kisha makundi mengine.
Msafara ulipofika Morocco, wachezaji na makocha pamoja na maofisa wengine wa timu ndio walitangulia katika kukamilisha taratibu za uhamiaji kisha wakawahishwa kwenye gari lililoandaliwa na kupelekwa hotelini.
Ukaguzi wa hati za kusafiria kwa wasafiri wanaoingia Morocco umeonekana kwenda taratibu jambo ambalo limechelewesha kundi kubwa la watu waliokuja hapa Casablanca kutoka uwanjani na kwenda hotelini.
Simba imepanga kukaa hapa jijini Casablanca kwa siku mbili kisha baada ya hapo itasafiri kuelekea katika jiji la Berkane ambako mechi yake itachezwa siku ya Jumamosi wiki hii na mchezo wa marudiano utafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mei 25, mwaka huu.
Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kucheza hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambalo lilianzishwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa Kombe la CAF na Kombe la Washindi Afrika.
Hata hivyo hii ni mara ya pili kwa Simba kucheza hatua ya fainali ya mashindano ya klabu Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa 1993 ilipofungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast katika Kombe la CAF.