Tshabalala: Imeisha hii

KAMBI ya Simba imezidi kunoga pale Mo Simba Arena, Bunju kwa mastaa wa timu hiyo wakijiandaa na mchezo dhidi ya Yanga kwa kupigishwa tizi la maana, huku kukiwa na ulinzi mkali wa kutoruhusu mtu yeyote asiyekuwa na kibali kuingia, lakini nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ametoa kauli ya kibabe.
Tshabalala amevunja ukimya na kusema kwa maandalizi waliyoyafanya kwa sasa haoni kitu gani kitakachoizuia safari hii Simba isitoke na ushindi mbele ya Yanga kwenye mechi utakaopigwa Jumapili hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tuanze kwanza na mazoezi ya juzi Jumatano jioni ambako Kocha Juma Mgunda alikuwa akitoa mbinu nyingi za kushambulia kupitia upande wa kushoto anaocheza Tshabalala na Augustine Okrah ulitumika zaidi kwenye zoezi hilo.
Mgunda alikuwa akiwasisitiza viungo wake, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin kwa nyakati tofauti kufuatilia mashambulizi yalivyokuwa yakipelekwa kwa Tshabalala na Okrah kwani wana uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji.
Tangu Kocha Mgundu amekabidhiwa timu, Tshabalala na Okrah wamekuwa wanacheza kwenye maelewano makubwa hasa timu inapokwenda kutengeneza mashambulizi katika lango la timu pinzani na huenda mbinu hiyo wakaitumia kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya watani wao wa jadi.
Mara baada ya zoezi hilo, Tshabalala alisema uimara wake wa kucheza kwenye kiwango bora wakati huu anahitaji timu ifanye vizuri kwenye michezo yote kama vile ambavyo malengo yao waliyojiwekea.
Alisema mechi zote dhidi ya Yanga alizowahi kucheza hakuna hata moja uliowahi kuwa rahisi kutokana na ukubwa wa pambano hilo ila kutokana na maandalizi waliyokuwa nayo sasa kuna dalili ya kwenda kufanya vizuri na kupata ushindi.
“Huku kwetu wachezaji kama tuna deni vile kila mmoja kwa nafasi yake atakwenda kupambana kuliko kawaida na wale ambao watakuwa wanaangalia mechi watashangaa na tunafanya hivyo kwa sababu tunahitaji ushindi,” alisema Tshabalala na kuongeza;
“Ushindi utakuwa na maana kubwa kwetu, tutajiweka kwenye mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na utakuwa mwendelezo wa kufanya vizuri tangu katika michezo ya hivi karibuni.
“Hatuna matokeo mazuri dhidi ya Yanga hivi karibuni ila kutokana na maandalizi tunayoyafanya kila kitu kinakwenda vizuri naamini tutapata matokeo bora kwenye mchezo wa Jumapili.”
Okrah kwa upande wake aliesema amewahi kucheza michezo wa dabi (Sudan na Ghana), ila hii ya Tanzania imekuwa na ushindani mkali na wa aina yake kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili hata mashibiki nje ya uwanja.
“Kikubwa nahitaji kwenda kushindana zaidi ya wapinzani walivyo, kucheza kwa malengo ya timu ili kupata ushindi ambao utatuweka kileleni mwa ligi kwa uhakika zaidi, kutokana na ubora wa kikosi chetu kwa sasa hilo linawezekana,” alisema Okrah.