Try Again aiwahi AC Horoya

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Simba, Salim Abdallah 'Try Again' yupo Morocco kwa ajili ya mambo mawili makubwa ya kuinufaisha klabu hiyo.
Jambo la kwanza Try Again ni miongoni mwa wawakilishi wachache kutokea Afrika ambao wataudhuria mkutano wa Shirikisho la soka duniani (FIFA), kuhusu mambo mbalimbali ya soka la dunia.
Baada ya hapo Try Again atakuwa na kikao cha Shirikisho la soka Afrika (CAF), kuhusu mambo mbalimbali ya soka la Afrika ikiwemo mashindano ya (Super League), ambayo yataanza hivi karibuni.
Jambo lingine litakalo jadiliwa kwenye mkutano wa CAF, masuala ya bajeti nzima na kila timu itakayoshiriki inatakiwa kupata kiasi gani ili kujikimu kabla na baada ya mashindano.
Haraka baada ya kumaliza mambo hayo mawili Try Again atachukua ndege na kutua Guinea kwa ajili ya kuunganisha nguvu na Mratibu wa timu, Abasi Ally kwa ajili ya kuweka mazingira sawa.
Kuna mambo ya msingi Try Again atayaweka sawa Guinea kwa ajili ya kuhakikisha kikosi baada ya kufika siku mbili kabla ya mchezo kukutana na mazingira yote mazuri yapo tayari.
Kikosi cha Simba baada ya kumalizana na Al Hilal kwenye mchezo wa kirafiki uliyochezwa jana Jumapili kinatarajia kuondoa nchini Februari 8, kwa ajili ya kwenda Guinea.
Simba itacheza mechi ya kwanza hatua ya makundi Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Horoya Februari 11.