TRA wasanukie kodi ya udangaji tuongeze mapato ya serikali huko!

Muktasari:
Pendekezo la kodi ya udangaji limetolewa. Kwani vipi? Wabunge wa kitaa, Luqman Maloto na Dk Levy wanajadili.
SAUTI zinavuja kutoka ‘siasani’, vipi michezoni na kunako burudani? Zari amefichua kuwa Diamond hajatuma hata mia kwa watoto wake mwaka sasa.
Pendekezo la kodi ya udangaji limetolewa. Kwani vipi? Wabunge wa kitaa, Luqman Maloto na Dk Levy wanajadili.
LEVY: Luqman nd’o kusema bado una ‘hangover’ ya posho za Irene Uwoya? Ulilewea au hukupata sasa unaugulia maumivu?
LUQMAN: Acha kupiga domo, wewe sema uliokota wekundu wangapi kwenye sadakalawe ya Uwoya?
LEVY: ‘Levo’ zangu siyo za kutafuna pesa za Irene. Mimi niko kwenye ‘levo’ za kumuwezesha zaidi ili aendelee kutapanya.
LUQMAN: Kwani sasa hivi unamwezesha nani? Huyo unayemwezesha mbona hatuoni akigawa noti kwa sadakalawe kama Uwoya?
LEVY: Kwani mpaka nijitangaze? Mimi siyo mtu wa mboyoyo. Mie ni ‘andagraundi’ pedeshee nahonga mpaka figo na maini.
LUQMAN: Acha hizo, unaweza kuhonga Toyota Prado Land Cruiser kama la Diamond alilomnunulia Tanasha?
LEVY: Sasa naona unachanganya madesa. Kuna kuhonga, kurogwa, kukomoa na sifa za kushangaza. Upedeshee wangu ni wa kimataifa. Yaani nakupa dawa za kufubaza wadudu wa Ukimwi, kisha nakuamuru uendeshe shughuli zako nitakavyo mimi.
LUQMAN: Kwani kati yako na Diamond Platnumz nani mhongaji mkubwa?
LEVY: Usiniweke kwenye eneo lake la kurogwa, kukomoa na hizo sifa. Diamond karogwa na uchawi fulani unapatikana Nakuru. Unaitwa ‘Sokomeza ndani’. Na pia ana kitu kinaitwa ‘Komoa’, yaani anamkomoa Zari!
LUQMAN: Mwanaume ambaye anamhonga mwanamke gari la milioni 200. Anamnunulia mama yake gari la milioni 200. Halafu hajalipia ada watoto wake mwaka mzima, huyo unamwitaje?
LEVY: Kifupi huwezi kukulia Tandale ukawa mhongaji vile. Tambua tu kuwa kamhonga Tanasha.
LUQMAN: Ooh, kwa hiyo ile ndinga Toyota Land Cruiser VX chapa ya mwaka 2018 anaendesha baba wa kambo wa Diamond? Wewe ulimuona wapi?
LEVY: Sasa unadhani mchongo wake ni upi? Ni mwendo wa kulamba lips na ‘kumdraivu’ bebe la bebe kila kona anakoenda. Huku wakisubiri kipato toka kwa Mnyama Simba toka Mbuga ya Tandale. Umarioo ukiuotea sehemu, huwezi kuona mabadiliko ya kisiasa wala majira. Unaweza kudhani Rais bado ni Kikwete, na mwaka mzima ni masika tupu. Umarioo ni ‘dili’ mjini kuliko siasa.
LUQMAN: Hapa inabidi nikufunge breki, hukawii kusema Baba Dangote wa kambo anadanga kwa Mama Dangote. Ishia hukohuko. Wivu tu!
LEVY: Sitashangaa nikisikia kajiweka kwa Uwoya. Maana wale watu wana ufundi wa kunusa viumbe uzao wa Eva wenye ukwasi mrefu. Sema ni vile pesa za mabebe wa Bongo Movie utadhani vocha za jero. Unakwangua haraka, unajaza haraka na kuisha haraka. Maisha ya Uwoya hata Wolper, Wema na Kajala wameyapitia. Watafute hii leo, mmoja sijui fundi uashi sijui cherehani, mwingine yuko ‘bize’ na michezo ya ‘kubeti’, mwenzao sijui ana duka sijui ‘grosare’ kama siyo ‘famasi’ ya nguo za watoto.
LUQMAN: Hivi unaweza kumjua aliye nyuma ya fujo za Uwoya kwa sasa? Nataka pia nijue TRA huwa wanatoza kodi pesa za kudanga? Makusanyo ni shi’ngapi? Kama hawakusanyi, huoni kuna umuhimu wa kutoza kodi mapato haya? Mbona mawigi yanatozwa kodi?
LEVY: Mimi kwa ‘intelejensia’ yangu inaonyesha danga linatoka Kenya na lina vinasaba na Ikulu ya Nairobi. Nimejaribu kufuatilia Bongo nimegundua pesa za kuchezea hivyo vyanzo vyake vingi viko jela. Na vingine vimejikita ‘Sauzi Afrika’ kukimbia mkono wa mrefu. Hapa Bongo hakunaga madanga ‘nawadeizi’. Kuhusu TRA sina uhakika sana maana hata nikiwa ofisa wa TRA kwenda kumdai Uwoya, labda mnitoboe macho. La sivyo hiyo kodi naweza kuomba mnikate mimi kwenye mshahara wangu ila yeye msimguse.
LUQMAN: Ungekuwa ofisa wa TRA ungeambiwa uende ukadai kodi ya mapato ya aina hiyo kwa Uwoya, Wema Sepetu, Hamisa Mobetto na yule sijui Sanchi, wapi ungepata wakati mgumu kudai?
LEVY: Hao wengine nawaweka selo bila dhamana. Uwoya ile ni mashine ya kusaga na kukoboa, Uwoya mmoja ni Hamisa 10, Wema 20, Sanchi 40. Katika hali ya kawaida kumuweka Uwoya kwenye kundi la hao unastahili kufunguliwa mashitaka. Uwoya ni mgodi wa Tanzanite unaopiga misele town.
LUQMAN: Kama Uwoya ni mgodi wa Tanzanite mbona Dogo Janja hajatajirika? Si alimuoa kabisa? Yule H-Baba yupo wapi? Si alikuwa wa kwake kwa miaka?
LEVY: Kwani madini ya Tanzanite yaligundulika lini kule Mirerani? Je, wakazi wa eneo la Simanjiro wametajirika? Kutajirika inategemea na akili za mtu. Sasa Dogo Janja mwenyewe anaomba ‘Banana’ badala ya pesa, H-Baba kaomba ‘Penzi Bubu’ badala ya utajiri.
LUQMAN: Sasa ukiwa na Uwoya unafanyaje ili upate mkwanja. Tugee maujanja yaliyowashinda akina Janjaro na H-Baba.
LEVY: Unataka kuacha shughuli zako ukaatamie kwa Uwoya? Acha janja janja wewe kijana kafanye kazi. Uwoya wa sasa siyo yule wa enzi za kina Kanumba na Sajuki. Uwoya wa sasa yuko juu mawiguni, ana pesa zinazoweza kuvunja kamera za mamilioni ya pesa, itakuwa ndoa za mahari ya mbuzi na debe la mbege?
LUQMAN: Uwoya hana nyimbo. Vile vi elfu sabini alivyowarushia waandishi ndio unamuona ana pesa? Wema aliwahi kukokota Q7 Audi. Akawaleta Bongo akina Omotola Jalade na Van Vicker. Stori kubwa ya Uwoya ni ipi zaidi ya kutemwa na supastaa Ndikumana kisha akaolewa na Janjaro?
LEVY: Stori kubwa ni kuwavuruga waandishi kwa kuwarushia pesa na wao kuwehuka kiasi cha kuvunja vitendea kazi. Kama ni elfu sabini, kwanini wavuje kamera za mamilioni kugombea elfu sabini? Hili tukio halijawahi kufanywa na yeyote duniani. Waandishi waligombea pesa kama wali wa shughuli uswahilini.
LUQMAN: Hebu tubaki kwenye masuala mtambuka, Zari anasema kumbe Diamond na mbwembwe zote hata matumizi ya watoto hatumi, ada halipi na hajui wanakula nini?
LEVY: Inakuwa ngumu kujua yupi mwenye tatizo. Lakini vyovyote iwavyo, Dangote na wale mababa watatu wanaojiita mameneja wana kitu cha kufanya kwa ajili ya wadogo wale. Kama vipi Zari akiona hakieleweki akapange ‘masta’ moja Soweto kule, kisha lile jumba apangishe watu. Kodi yake alipie ada na ujinga mwingine. Fella, Tale, Sallam na wenzao wameshindwa hata kukopa busara sehemu kumaliza hii tatizo? Anahonga Prado za mamilioni kesi ndogo ya viada inamzingua? Tatizo ni uelewa tu wa wengi Kibongo Bongo wanachukulia poa. Kwetu Amerika na Ulaya Dangote angejuta. Wangegawana pesa za shoo zote na Zari.
LUQMAN: Suala sio kupanga wala kutokuwa na pesa. Juzijuzi Zari ameonyesha mijengo yake kadhaa ya kifahari Sauz. Mingine wanakaa wapangaji na mingine imetelekezwa, hakai mtu. Zari mwenyewe juzikati kanunua bonge la mjengo. Wale watoto wanasoma shule za bei mbaya, wanaishi maisha ghali sana na hawakosi kitu. Suala hapa ni baba kuwajibika. Unahonga gari la milioni 200 halafu watoto wako hujui wanasomaje, wanakulaje, wanavaaje.
LEVY: Iko kazi. Nasikia mshua wa Sangote pia alikuwa anauza pamba mtaa wa Pemba - mastaa wa kitambo kina Abeid Mziba, Said Mwamba Kizota, Moshi Wiliam, Dk Remmy, Pawa Mabula kina Said Swed Scud, Mzee Small, Lunyamila, Dua Said, Athuman China na kina Masatu walikuwa wananunua kwake pamba za kijanja. Akaishia kula bata huku Diamond akisota na mama’ke Tandale. Naona naye du!
LUQMAN: Sijui mama Dangote huwa anamshauri nini kijana wake. Kama yeye alimlea kwa tabu, basi atakuwa kwenye wakati mzuri wa kumshauri mtoto wake awajali wajukuu zake. Mama angewaza vizuri angekataa VX V8 alilopewa ili pesa hiyo itumike kulea wajukuu au kama pesa ipo, basi mamilioni mengine yaende kwa wajukuu.
LEVY: Usimuingize hapo Bi Mkubwa, ingawa ana nafasi kubwa sana ya kushauri au kuelekeza. Hivi hujui kuwa familia ya uswahilini mtoto akiwa na pesa hugeuka nd’o baba nd’o mzazi nd’o kila kitu? Kama huna hela hata ushauri wako unapuuzwa na nduguzo. Umri wa Dangote siyo wa kusubiri ushauri wa mama juu ya watoto wake. Na sasa kanaongeza mwingine toka Kenya.
LUQMAN: Wewe ungekuwa babu ungeridhika kupewa gari la milioni 200 na mtoto wako, halafu hujui wajukuu zako wanaishije?
LEVY: Kwani kuna tofauti gani na Ajibu kununuliwa kwa milioni 100 ili acheze mechi za kombe la thamani ya milioni 70? Au Simba yenye usajili wa bilioni 1.3 inashiriki kombe lenye thamani ya milioni 70. Nd’o Diamond naye, anahonga ndinga za mamilioni akiwa kapanga nyumba Mbezi na hajui watoto wanaishije Sauzi. Lakini mbona zipo habari kuwa Zari kambania kuwaona watoto? Tusubiri tu itajulikana tuendako!