TRA United kufumua kikosi
Muktasari:
- Timu hiyo ambayo ilijulikana awali kama Tabora United ilimaliza Ligi Kuu msimu wa 2025/26 katika nafasi ya tano kwa pointi 43 ikizidiwa na Singida Black Stars iliyoshika nafasi ya nne kwa pointi 50.
TRA United imesema licha ya mafanikio ya kumaliza nafasi tano za juu, lakini malengo yao hayakutimia kama ilivyotarajia, ikiahidi kusuka upya kikosi kujiandaa na msimu ujao ikisisitiza kubaki na mastaa wake waliong'ara.
Timu hiyo ambayo ilijulikana awali kama Tabora United ilimaliza Ligi Kuu msimu wa 2025/26 katika nafasi ya tano kwa pointi 43 ikizidiwa na Singida Black Stars iliyoshika nafasi ya nne kwa pointi 50.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa timu hiyo Ettiene Ndayiragije amesema malengo yao ilikuwa ni kuitambulisha rasmi TRA United kwa wadau na mashabiki wa soka ndani na nje, lakini wakihitaji kumaliza nafasi nne za juu.
Alisema kutofikia malengo hayo benchi la ufundi linaenda kujipanga kusuka upya kikosi kwani wachezaji waliokuwa kikosi cha kwanza walitofautiana kwa ukubwa na waliokuwa wakisubiri benchi.
“Wale wa kutegemewa walikuwa 12, utagundua utofauti ni mkubwa na wale waliosubiri benchi, kwa maana hiyo tunaenda kusuka upya kikosi na lazima tuje na mabadiliko makubwa ili kupambania uwakilishi wa kimataifa mwakani,” alisema Ndayiragije.
“Kumaliza nafasi ya tano ni mafanikio pia ukizingatia timu niliikuta katikati ya ligi, kwa nafasi yangu nitaweza kushawishi uongozi ili kuwabakiza wachezaji waliofanya vizuri, atakayeamua kuondoka kwa maslahi yake ni sawa kwakuwa ni suala la mikataba.”€ Kocha huyo ambaye ni raia wa Burundi ameongeza kuwa Ligi Kuu Bara inazidi kubadilika kwa ubora kutokana na miundombinu, ushindani na kufuatiliwa na wadau wengi ndani na nje ya nchi akieleza kwamba anaitarajia kuzidi kutesa Afrika.
Kwa upande wake, msemaji wa timu hiyo, Christina Mwagala amesema uongozi unaenda kufanya tathimini na kurekebisha na kuboresha walipofanikiwa akieleza kuwa matokeo waliyopata si mabaya.
Kuhusu hatma ya wachezaji wanaotajwa kuwindwa na timu nyingine, Christina amesema kumaliza msimu bila wachezaji kutajwa kutakiwa na wapinzani lazima kujiuliza akieleza kuwa hatua hiyo ni bora kwao.
“Kuwa na wachezaji wanaotajwa kuhitajika na timu pinzani ni dalili za kwamba tulikuwa na kikosi bora, uongozi utalifanyia kazi kwani na sisi tunayo malengo yetu msimu ujao hivyo tunatarajia kuja kivingine,” alisema Christina.