Timbe aleta mbinu za Uholanzi Yanga

Kocha wa Yanga, Sam Timbe akizungmza na wachezaji wake wakati wa mazoezi
CALVIN KIWIA KOCHA wa Yanga, Sam Timbe ametoa mpya, sasa anataka kuona kila mchezaji akifunga wakati wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, akikumbushia mtindo wa 'Total Football' uliokuwa unatumiwa na timu za soka za Uholanzi katika miaka ya 1970. Mtindo wa Total Football, ambao ulibuniwa na kocha wa zamani wa Ajax ya Uholanzi na timu ya taifa ya nchi hiyo, Rinus Michel unataka mchezaji kufanya vitendo vyote uwanjani bila ya kujali anacheza nafasi gani. Ulikuwa ukitumiwa zaidi na Ajax kuanzia mwaka 1969 hadi 1973 na timu ya taifa ya Uholanzi kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1974 nchini Ujerumani. Ilifika hatua ya fainali katika miaka ya 1974 na 1978. Kwa ubunifu huo, Fifa ilimteua Michels kuwa kocha bora wa karne kutokana na mafanikio ya mtindo huo, ambao unataka mchezaji kujua majukumu ya kufunga na kuzuia. Mwanaspoti ilimshuhudia Timbe, ambaye alishikwa na hasira baada ya timu yake kuondoka na ushindi wa kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, wiki iliyopitaa amekuwa akiendesha mazoezi huku akitoa maelekezo kwa ukali. "Sitaki kuona tunamtegemea Asamoah (Kenneth) peke yake, nataka kuona kila mmoja," alisikika akiwaambia wachezaji wakati wa mazoezi ya timu hiyo, jana Jumatatu kwenye uwanja wa Kaunda jijini Dar es Salaam. "Nafasi ya kufunga inaweza ikamtokea mchezaji yeyote yule, hivyo hatuna budi kufunga unasikia Taita (Godfrey)," alisisitiza na kuongeza kuwa pale mabeki wanapopanda mbele basi washambuliaji wanapaswa kushuka kusaidia shughuli za kulinda lango. Yanga ina mabao 13 yakiwa yamefungwa na Kennth Asamoah (matano), Davies Mwape (mawili), Haruna Niyonzima `Fabregas' (mawili) waliofunga bao moja ni Shamte Ally, Rashid Gumbo, Hamisi Kiiza na Nurdin Bakari. Simba ndio imefunga mabao mengi zaidi, ina mabao 14. Katika programu ya mazoezi aliyoianzisha jana Jumatatu asubuhi, Timbe alikuwa akitumia muda mrefu kuwapa mbinu mbalimbali za kufunga bila kujali mchezaji huyo anacheza katika nafasi gani uwanjani. Pia, hakusita kutoa adhabu kali kwa wale wote ambao walikuwa wakishindwa kufuata maelekezo yake wakati wa kufundisha namna ya kupachika mabao. Hatua ya kwanza ilikuwa kutafuta pumzi na kasi ya mchezo kwa kukimbia mbio ndefu kwa kuzunguka uwanja na mbio fupi kwa kukimbia kwenye koni(vifaa vya kufanyia mazoezi ya soka). Baada ya mazoezi ya kuongeza pumzi, hatua iliyofuata ilikuwa ya kupiga mashuti ya umbali wa mita 18-25. Wachezaji waliofanya vizuri katika hatua hiyo walikuwa ni pamoja na Chacha Marwa, Oscar Joshua, Godfrey Taita, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kiggy Makasi. Walioboronga hatua hiyo walikuwa ni pamoja na Julius Mrope, Abuu Ubwa, Jerry Tegete, Godfrey Bonny na Rashid Gumbo waliojikuta wakipewa adhabu ya kuruka juu mara tano. Hatua ya mwisho, aligawa timu tatu zenye wachezaji nane kucheza uwanja mzima kwa lengo la kutafuta pumzi, kasi na kutengeneza nafasi na kufunga mabao. Waliofunga ni Hamis Kiiza, Juma Seif 'Kijiko' Chacha Marwa, Stephano Mwasika na Gumbo aliyemfunga Shaaban Kado kwa mkwaju wa penalti. Mazoezi hayo yaliyodumu kwa muda wa saa tatu yakianza saa mbili asubuhi hadi tano asubuhi, lengo kuu likiwa kuwapa wachezaji pumzi na kasi ya mchezo. "Kwa jinsi ligi ilivyopamba moto kwa sasa hatutakiwi kulala kabisa unasikia Tegete (Jerry), hakuna lelema hapa, lazima tuonyeshe bidii na kujituma bila kusukumwa," alisema Timbe, ambaye atapima ukali wa mazoezi yake wakati wa mechi ya keshokutwa Alhamisi dhidi ya Toto African itakayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika pambano la Ligi Kuu lililopita Yanga iliilaza Kagera Sugar bao 1-0 na kufikisha pointi 15 ikiwa sawa na Mtibwa Sugar na JKT Ruvu. Inashika nafasi ya nne.