Thiago kuumia kuliitesa Bayern, baba yake
Muktasari:
- Hoffenheim waliwasumbua Bayern hadi Bayern wakalazimika kubadili uchezaji wao na kuanza kutegemea mashambulizi ya kushitukiza jambo lililokuwa la kushitusha hasa matokeo ya mwisho yalipokua sare ya 3-3.
TOLEO lililopita kwenye Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alizungumzia mabadiliko ya mambo katika Bayern huku baadhi ya makocha wakija na mikakati ya kudhibiti mbinu za Pep Guardiola na namna ambavyo Bayern walipata wakati mgumu katika mechi yao na Hoffenheim. Endelea…
Hoffenheim waliwasumbua Bayern hadi Bayern wakalazimika kubadili uchezaji wao na kuanza kutegemea mashambulizi ya kushitukiza jambo lililokuwa la kushitusha hasa matokeo ya mwisho yalipokua sare ya 3-3.
Kwa mara ya kwanza na wakati pekee katika Bundesliga, mpinzani wa Bayern alipiga mashuti mengi kwenye lango la Bayern, alikuwa na mashuti 20 wakati Bayern ya Pep ilikuwa na mashuti 11.
Halikuwa jambo zuri kwa timu mwenyeji ambaye rekodi yake ya ushindi wa mechi 19 mfululizo tangu Oktoba ilifikia ukomo, ni sare ya kwanza nyumbani katika mechi ya ligi kwa kipindi cha miezi 15 na mara ya kwanza katika miaka miwili Bayern kukubali kufungwa mabao matatu katika ligi.
Thiago aliumizwa katika dakika ya 21 na ndivyo ilivyokuwa kwa mpango aliokuwa nao Pep kwa mechi na United, nao ulipata pigo, nguvu ya jeshi lake ilionekana kama kuanza kuyumba.
Thiago ni mtu muhimu, si tu kwa pasi zake za hadhi na uhakika, pia ni muhimu kwa jinsi anavyowaunganisha pamoja wenzake na kuwafanya wacheze kitimu eneo la kati. Ni kifaa kinachosaidia kuunganisha timu.
Pep anakiri kwamba kukosekana kwa Thiago kunaweza kuleta utofauti katika nafasi yao ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa.
Wakati wa chakula cha jioni na wachezaji, Lorenzo Buenaventura akaona picha ya kwenye Twitter ikionyesha maumivu ya Thiago yalivyotokea, akalizungumzia hilo kumwambia Arjen Robben, “Lazima na wewe ukiingia uingie kwa nguvu zote ili kuupata mpira, usijilegeze unapowania mpira, kuwa makini kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu usiruhusu hali kama hii ijitokeze.
Dakika kadhaa baadaye, Thiago akiwa hospitali alikolazwa anampigia simu Buenaventura, “Ni kama nimeumia sehemu kubwa kwenye misuli, kwa uchache nitakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane, kwaheri Kombe la Dunia (2014).
Buenaventura akiwa ndiye kocha wa viungo anafikisha habari hiyo kwa Javi Martinez na moja kwa moja wanakwenda kwa Thiago kumfariji, wakati huo tayari kulikuwa na hali ya kutoelewana lakini baadaye kukawa na jambo lililowafanya watabasamu pamoja.
Thiago anampigia simu baba yake, Mazinho ambaye alikuwa na timu ya taifa ya Brazil iliyotwaa Kombe la Dunia 1994 na kumwambia anavyoumwa, Mazinho hakutulia na ujumbe ule, pale pale akampigia simu Buenaventura ambaye ni rafiki yake mkubwa.
Huku akitoa sauti inayoashiria huzuni, Mazinho alimwambia, “Loren nimeumizwa, Thiago ameumia hasa, atakuwa nje miezi sita hadi minane. Mazinho alielewa vibaya tatizo lile.
Ni tatizo ambalo wakati mwingine linaweza hata kuchukua miezi sita au minane, kwa kiasi fulani jambo lile liliwafanya Buenaventura na Thiago wacheke kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, wakamtuliza Mazinho na kumwambia si miezi sita ni kama wiki sita hivi, habari ambayo kidogo iliibua faraja na kuifanya jioni ile iwe nzuri.
Siku iliyofuata ya Jumapili asubuhi Machi 30, mazoezini, wachezaji waliotoka sare ya 3-3 na Hoffenheim waligawanywa katika makundi mawili, moja lilibaki katikati ya uwanja akiwamo Pizarro ambaye usiku wake haukuwa mzuri.
Zilikuwa dakika 90 za kwanza kwake katika msimu na akaumia vibaya, wachezaji wengine kina Ribery, Van Buyten, Schweinsteiger, Gotze na Shaqiri walichukua baiskeli zao na kufanya mazoezi ya kuzunguka mjini kwa nusu saa.
Thiago na Pep wanakutana na daktari Muller-Wolfhart kuzungumzia matibabu sahihi ya majeraha, daktari alianza kuweka utaratibu wa matibabu lakini Thiago akasisitiza ni muhimu atibiwe na mtaalamu wa siku nyingi, Ramon Cugat mjini Barcelona kutokana na aina ya matibabu yake
“Najua kuna maumivu anapofanya operesheni yake kwa sababu unaona kama ngozi unaunguzwa,’’ anasema Thiago lakini ni lazima uyakubali maumivu.
Wakati wakitoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, wachezaji wenzake walikuwa wakimtakia kila la kheri katika matibabu, “Matibabu yasiwe ya muda mrefu, tunakuhitaji Thiago,’’ Neuer alimwambia.
“Nimefarijika sana,” alisema Thiago, “nilikuwa katika unyonge jana usiku lakini nimepata nguvu asubuhi hii, niko hapa kwa ajili ya mlo wa asubuhi na wachezaji wenzangu na ninajiona kama baada ya siku moja tu nitakuwa fiti.
“Mtazamo wako una maana kubwa katika kubadili jambo, ni vipi utapona tatizo kama hili na kwa sasa kichwa changu kimetulia kiko katika fikra sahihi, wananiambia wiki sita hadi nane, mimi nataka kuzirudisha hadi tano.”
Pep naye alimhakikishia Thiago kuwa timu itafanya kila liwezekanalo ili kufikia fainali ya DFB Pokal na ligi ya mabingwa kwa ajili yake na Thiago akaahidi kupambana ili awe tayari kwa fainali zote hizo ingawa ukweli ni kwamba haikuwa rahisi kwa wote hao kufikia malengo hayo.
Itaendelea Jumamosi ijayo…