TFF: Udhamini wa SBL kwa Stars chachu ya ushindi

Muktasari:
Mwezi Mei mwaka 2017, SBL iliingia mkataba wa udhamini wa miaka mitatu kwa Taifa Stars wenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 na kuifanya kampuni hiyo kuwa mdhamini mkuu wa Timu ya Taifa.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema timu ya Taifa (Taifa Stars) ina kila sababu ya kufanya vizuri katika mechi zake kwa ajili ya kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Cameroon mwakani (2019).
Kwa sasa, Taifa stars ipo kambini ikijiandaa na mchezo wake wa kufuzu AFCON dhidi ya timu ya taifa ya Cape Verde utaofanyika tarehe 12 mwezi huu ikiwa katika Kundi L.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam, mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF Clifford Ndimbo alisema, udhamini wa Kampuni ya Bia ya Serengetiu(SBL) kwa Taifa Stars umeondoa changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha na kuifanya timu iwe katika nafasi nzuri ya kushinda mapambano yaliyo mbele yake.
“Ili timu iweze kufanya vizuri ni lazima ipate maandalizi mazuri pia na rasilimali fedha ni muhimu kwa ajili ya kuweza kufanikisha maandalizi mazuri na kwa wakati. Tunawashukuru SBL kwa kuamua kudhamini timu yetu ya taifa na tuna kila sababu ya kufanya vizuri kutokana na uwezeshaji huu,” alisema Ndimbo.
Alisema udhamini wa SBL umekuwa ni chachu kwa mafanikio kwa Stars kutokana na kufanya maandalizi mazuri ambayo yameisaidia timu kupata matokeo ya ushindi katika mechi mbali mbali ambazo imekuwa ikicheza.
“Tumecheza na timu kubwa na ngumu kama Uganda na tukafanikiwa kutoa nao droo wakiwa nyumbani. Ni timu chache sana za Afrika ambazo zinacheza na Uganda nyumbani na zikatoka bila kufungwa,” Ndimbo aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL John Wanyancha alisema kampuni hiyo imekuwa ni moja kati ya mdau mkubwa wa michezo hapa nchini na hususani mpira wa miguu kwa kuwa michezo huwaleta watu pamoja.
“SBL ni mdau mkubwa wa michezo na hususani soka. Hii ni mara ya pili kutoa udhamini Timu yetu ya Taifa baadha ya udhamini wa mara ya kwanza ambao ulidumu kutoka mwaka 2007 hadi 2011.SBL pia ni mdhamini wa ligi ya wanawake,” alisema Wanyancha.