TETESI ZA USAJILI BONGO: Kapama ageuka lulu sokoni, Vikumbo Simba, Yanga

Muktasari:

  • Kapama ambaye alijiunga na Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miezi sita amemalizana na timu hiyo ambapo sasa anawindwa na Dodoma Jiji, Mashujaa na JKT Tanzania.

LICHA ya kuishusha daraja Mtibwa Sugar, lakini kiraka Nassoro Kapama amegeuka lulu kutokana na timu mbalimbali kusaka saini yake.

Kapama ambaye alijiunga na Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miezi sita amemalizana na timu hiyo ambapo sasa anawindwa na Dodoma Jiji, Mashujaa na JKT Tanzania.


MLINZI wa kulia wa Klabu ya KMC, Rogers Gabriel anawindwa na timu ya JKT Tanzania na KenGold ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Beki huyo ambaye amekuzwa na Klabu ya Pamba ya jijini Mwanza, amemaliza mkataba wa kuitumikia KMC ambayo hata hivyo hakuwa na namba ya kudumu kikosi cha kwanza.


TIMU za Kagera Sugar, KMC, Coastal Union na Dodoma Jiji, zimeonyesha nia ya kuiwinda saini ya kiungo wa Mtibwa Sugar, Juma Nyangi.

Kiungo huyo ambaye msimu ulioisha akiwa na Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja alihusika kwenye mabao manne, huenda akacheza tena Ligi Kuu msimu ujao kama mambo yataenda sawa. Charity James


BEKI wa Tabora United, Andy Bikoko ameziweka vitani timu tatu za Ligi Kuu, ambazo zote zinawania saini yake kwa ajili ya msimu ujao.

Mkongomani huyo aliyebakiwa na mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Tabora United, saini yake inawindwa na timu tatu ambazo ni Singida Fountain Gate, Pamba na Singida Black Stars. Victoruia Melkiad


SIMBA Queens na Yanga Princess zimeingia kwenye vita ya kumuwinda beki wa kati wa Alliance Girls, Anita Adongo ambaye anamaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu.

Katika vita hiyo, Ceasiaa Queens na Fountain Gate Princess zilikuwa zikihitaji saini ya beki huyo mwenye nguvu.


BAADA ya kufanya vizuri akiwa na msimu wake wa pili, Simba Queens ipo kwenye mazungumzo ya kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja, straika Mkenya Jentrix Shikangwa. Alirejea Simba katikati ya msimu huu akitokea timu ya Beijing ya China alikokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Simba. Nevumba Abubakar


CEASIAA Queens iliyopo Ligi Kuu ya Wanawake inatajwa kuwa miongoni mwa timu zinazohitaji winga wa Alliance Girls, Nelly Kache.

Licha ya Alliance kufanya vibaya WPL lakini Ceasiaa imevutiwa na winga huyo mwenye mabao matano kutokana na kiwango bora alichoonesha.