Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Team Samatta, Team Kiba hapatoshi kila kona hapo Taifa leo

Muktasari:

Viingilio kwenye mchezo huo ni Sh2,000 kwa viti vya mzunguko, Sh5,000 eneo maalumu (VIP B) na eneo maalumu zaidi (Champion) itakuwa Sh20,000.

VITA ni vita muraa! Huku ni Samatta, kule ni Alikiba wanatunishiana misuli leo Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni mchezo maalumu wa kuchangisha fedha kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu.
Huu ni msimu wa pili wa kampeni za ‘Nifuate’ kupitia taasisi ya Samakiba zilizoanzishwa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ akishirikiana na msanii Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’.
Akizungumzia mchezo huo, Samatta alisema wanakwenda kutoa burudani kwa wadau wa soka ili kuchangisha fedha kuisaidia jamii.
“Hatuna kiwango maalumu ambacho tumekilenga kupata, chochote kitakwenda kusaidia jamii, msimu uliopita ulikuwa na mwamko mkubwa, hivyo ni matumaini yangu kuwa safari hii itakuwa mara dufu,” alisema nyota huyo.
“Nimeunda timu makini ambayo itaendeleza dozi kwa timu ya bishoo, Alikiba. Siwezi kufungwa na kikosi chake, mwaka jana tuliichapa mabao manne nadhani awamu hii ni tano.”
Upande wake Alikiba alisema mchezo wameumaliza nje ya uwanja kwa kuwakamata kila kona wapinzani wao na kilichobaki ni kwenda kuwaadabisha ndani ya uwanja.
“Ujue kulipiza kisasi ni dhambi, siwezi kusema nitalipiza kisasi ila nakwenda kumaliza kabisaa, naziona tano, lazima nishinde huu mchezo ndio maana nimeamua kuchukua kocha Mzungu,” alisema, Alikiba na kumalizia “Yeee baba.”
Fedha zitakazopatikana zitaelekezwa kwenye mambo matatu ambayo ni kutoa misaada kwa yatima, kusaidia wenye ulemavu na wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu.
Viingilio kwenye mchezo huo ni Sh2,000 kwa viti vya mzunguko, Sh5,000 eneo maalumu (VIP B) na eneo maalumu zaidi (Champion) itakuwa Sh20,000.

VIKOSI VYAO USIPIME
Kikosi cha timu ya Alikiba kinaundwa na kipa Aishi Manula, Abdi Banda, Saimon Msuva, Aggrey Morris, Haruna Niyonzima, Said Ndemla, Shiza Kichuya, Ibrahim Ajibu na Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Upande wa Samatta kipa ni Juma Kaseja, Shaaban Chilunda, Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngassa, Farid Mussa, Athuman Chuji, Amri Kiemba, Jerry Santo na Ramadhan Kessy.