TBC, TFF zaingia mkataba wa haki ya matangazo

Muktasari:

  • Huo ni muendelezo wa TFF kuingia mkataba wa haki ya matangazo baada ya ule wa Azam wa miaka 10 pia wa matangazo ya televisheni.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeingia mkataba wa miaka 10 na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wa haki ya matangazo ya radio kwenye mechi za Ligi Kuu.

Mkataba huo wa Sh 3.54 Bilioni umesainiwa leo na rais wa TFF, Wallace Karia na Gabriel Nderumaki, mwakilishi wa mkurugenzi wa TBC, Ayoub Rioba.

Karia amesema hiyo ni mara ya kwanza kuingia mkataba wa haki ya matangazo ya radio.

"Haijawahi kutokea katika soka letu," alisema.

Alisema kila mwaka watapata Sh 300 Milioni.

"Fungu kubwa la pesa hizi litaenda kwenye klabu na kila klabu itapata mgao sawa na nyingine," amesema.

Amesema pesa nyingine zitaelekezwa kwenye utawala bora.

Nderumaki amesema Shirika lao lina uwezo wa kurusha mubashara matangazo kutoka kwenye maeneo matano.

"Tumewahi kurusha kombe la dunia mwaka 2010, 2014 na 2018, lakini kwenye radio matangazo ya kimataifa tulirusha mbashara mechi ya Simba na Kaizer Chief.

"Pia haki hii sio kama tunafunga milango kwa wengine, la hasha, tutashirikiana kwa utaratibu utakaowekwa na TBC na TFF," amesema.