Taoussi apata akili mpya Azam FC

Muktasari:
- Azam FC juzi ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar inayoshiriki Championship kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro na kufungwa bao 1-0 lililopachikwa na Raizin Hafidh kwa penalti dakika ya 78.
KICHAPO cha bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa kirafiki kimemuibua kocha mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi aliyesema kilikuwa kipimo sahihi na kimempa mwanga wa nini afanye kabla ya kuendelea Ligi Kuu Bara mwezi ujao.
Azam FC juzi ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar inayoshiriki Championship kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro na kufungwa bao 1-0 lililopachikwa na Raizin Hafidh kwa penalti dakika ya 78.
Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema licha ya timu yake kukosa matokeo mazuri anaamini kuna mabadiliko makubwa na imani kubwa na wachezaji ambao licha ya mapumziko waliyokuwa nayo wamerudi wakiwa kwenye hali ya ushindani.
“Mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar kilikuwa ni kipimo sahihi na kwa wakati sahihi. Kupoteza haina maana hatukuwa bora, tumekutana na timu ambayo imetumia mbinu sahihi kutuadhibu na nafurahi kwa sababu imetupa changamoto,” alisema.
“Kupoteza kumetupa wakati sahihi wa kurudi kwenye uwanja wa mazoezi kusawazisha makosa ambayo yametufanya tuadhibiwe na hilo kila mmoja ameliona. Tunaendelea kujifua na tutakuwa na mchezo mwingine kabla ya kurudi kupambania nafasi ya kutwaa ubingwa michuano iliyo mbele yetu.”
Kocha huyo alisema wamecheza na timu nzuri ambayo imewapa kipimo sahihi kujiweka tayari kupambania nafasi ya kutwaa mataji ya michuano wanayoshiriki huku akidai wachezaji wanaendelea kuimarika siku hadi siku.
“Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye ligi hata kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA). Nina kikosi bora na hata ukiangalia mchezaji mmoja mmoja kuna ubora mkubwa, naamini kila mchezaji ana ndoto ya kutwaa mataji.”
Azam FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ambayo inatarajia kurudi Februari Mosi, baada ya kukusanya pointi 36 ikishuka dimbani mara 16. Timu hiyo inazidiwa pointi nne na vinara Simba wenye 40 wakicheza mechi 15. Nafasi ya pili inashikiliwa na Yanga ambayo nayo imecheza mechi 15 na kukusanya pointi 39.