Tanzania yafunika michuano ya EAUWC

Muktasari:

  • Mashindano hayo yaliyoshirikisha jumla ya timu 19 kutoka nchi tatu za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania, yalifanyika kwa siku tatu katika viwanja vya Chuo kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela kilichoko Mkoani Arusha.

WENYEJI Tanzania imefunika katika mashindano ya michezo kwa Wanafunzi wa Kike wa Vyuo Vikuu vya Nchi za Afrika Mashariki (EAUWC) yaliyomalizika jana mkoani Arusha.

Mashindano hayo yaliyoshirikisha jumla ya timu 19 kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, yalifanyika kwa siku tatu katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela jijini humo.

Tanzania ilianza kufanya vema kupitia Chuo Kikuu cha Dodoma katika mchezo wa soka kwa kuifunga timu ya USIU ya Kenya mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.

Kwa upande wa mpira wa Pete, Chuo cha Dodoma ilitwaa tena kikombe cha mshindi wa kwanza baada ya kuifunga Mzumbe magoli 40-33, huku mshindi wa tatu akiwa USIU Afrika ya Kenya.

Chuo Kikuu cha Kisii Kenya ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Udom mabao 28-21, huku nafasi ya tatu akishika USIU ya Kenya.

Kwa upande wa wavu, Chuo cha Makerere kutoka Uganda ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Kisii ya Kenya mabao 3-1, huku Chuo cha Udom ikichukua nafasi ya tatu katika mchezo huo.

Akizungumzia ushindani huo, Mwalimu wa michezo kutoka Udom, Patrick Mwani alisema ushindi huo umetokana na mazoezi, pia morali ya wachezaji wake katika mashindano hayo na sapoti kubwa kutoka kwa uongozi wa Chuo chao.

"Sisi kama chuo kikuu cha Dodoma, michezo ni moja ya ajenda kubwa kwenye taasisi yetu ndio maana mnaona kila mashindano yanayohusu vyuo vikuu tushiriki," alisema Mwani, huku Rais wa Shirikisho la michezo hiyo, Profesa Simon Munai alisema mashindano hayo ya msimu wa tatu, yameshirikisha timu 19 za wanawake kutoka Vyuo Vikuu vya nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda.

Alisema changamoto kubwa ni baadhi ya vyuo vikuu kutoshiriki mashindano hayo, yanayolenga kuwapa fursa wanawake wa ngazi za juu za elimu kuchangamana pamoja na kujadiliana yanayowasibu kimaisha na kielimu ili  kung'amua ufumbuzi.

"Mfano hapa Tanzania kuna zaidi ya vyuo 30, lakini vilivyoshiriki havifiki hata 10, hii Inaonyesha jinsi gani viongozi wa vyuo hivyo hawajui thamani na maana ya michezo kwa wanafunzi wao wa kike pia wanapora haki zao za kubadilishana mawazo na kujenga mtandao wa kimaisha na ajira," alisema Prof Munai.