Tamasha la utamaduni wa Mtanzania lazinduliwa Mwanza

TAMASHA la Utamaduni wa Mtanzania la mwaka 2021 lenye lengo la kutoa mafunzo na maelekezo kwa vijana, kuitangaza Tanzania katika mambo ya utalii wa ndani limezinduliwa rasmi leo katika viwanja vya Ngomeni- Kisesa wilayani Magu mkoa wa Mwanza.
Likiwa limebeba kauli mbiu ya 'Tudumishe Utamaduni Wetu - Kazi iendelee', tamasha hilo ambalo litahitimishwa kesho Septemba 8 limeanza leo saa 3 asubuhi na kuzinduliwa rasmi saa 6:40 mchana na Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula kwa niaba ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa.
Mabula amesema tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kudumisha tamaduni kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo na kutangaza vivutio vya asili na utamaduni kwa mataifa ya nje.
"Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na umoja wa Machifu na kituo cha utamaduni na historia Bujora kwa kurithisha utamaduni kwa vizazi,
nimefarijika kuona mmendelea kurithisha mila na desturi zetu ili vizazi vyetu visije vikapoteza utambulisho wa Mtanzania na historia yake," amesema Mabula.
"Uwepo wa Machifu wetu wanaoendelea kulinda na kuenzi tamaduni zetu kunaendelea kulifanya taifa letu liwe salama, nawaomba machifu wasisite kuingilia kati pale wanapoona vijana na jamii inakengeuka na kuvuruga maadili ya Mtanzania," amesema.
Makamu Mwenyekiti Umoja wa Machifu Tanzania (UMT), Chifu Msagata Fundikira, amesema tamasha litashirikisha mashindano ya kurusha mikuki, kucheza bao, ngoma za asili ambapo vikundi 11 vya ngoma vitashindana na kufundisha mila na desturi ambapo ameiomba Serikali kuusajili umoja wao uweze kufanya shughuli zake kwa uhuru.