Tajiri Yanga awapa jeuri mashabiki CAF

Muktasari:
- Bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ amenunua tiketi zote za mzunguko kwenye pambano hilo la marudiano ya Kundi D litakalopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya mechi ya awali iliyopigwa wikiendi iliyopita kumalizika kwa sare ya bao 1-1 mjini Kumasi, Ghana.
YANGA inashuka jioni ya leo kwenye Uwanja wa Azam Complex katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini wakimaliza watarudi kibaruani katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuialika Medeama, huku mashabiki 45,000 wakipata mchekea baada ya tajiri kuwapa jeuri.
Bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ amenunua tiketi zote za mzunguko kwenye pambano hilo la marudiano ya Kundi D litakalopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya mechi ya awali iliyopigwa wikiendi iliyopita kumalizika kwa sare ya bao 1-1 mjini Kumasi, Ghana.
Yanga inahitaji ushindi ili kujiweka pazuri kwenye kundi linaloongozwa na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri wanaofuatiwa na Medeama kisha CR Belouizdad ya Algeria.
Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, tajiri huyo ameamua kuwavuta mashabiki uwanjani kwa kununua tiketi zote za mzungumo ambazo zitapewa mashabiki zikiwa na thamani ya Sh135 milioni kwani kiingilio ni Sh3,000 kwa kichwa.
GSM amefanya hivyo akitaka eneo hilo lijae na kubaki tiketi za majukwaa mengine. Yanga kama ikitinga robo fainali itajihakikishia kiasi cha Dola 900,000 (takriban Sh2.2 bilioni).
Akizungumzia hilo, mmoja wa viongozi wa Yanga aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema kama kuna kitu ambacho uongozi na hata mfadhili huyo watafurahi ni kuhakikisha timu yao inatinga robo fainali.
“Nikuambie kitu ambacho rais wa Yanga na uongozi wake kiu kubwa ni kuona Medeama na timu zingine tutakazokutana nazo hapa nyumbani zinaacha alama zote,” alisema Kamwe.
“Tunataka hamasa kuwa kubwa kila mwana Yanga ushindi kwenye hiyo siku na mechi zingine zinazokuja mbele yetu. Tunautaka ushindi wetu hapa baada ya kufanyiwa mambo meusi kule ugenini. Viongozi hawa wanaona kwa timu hii tuliyonayo itakuwa sio haki kwetu kutotinga angalau robo fainali.”