Taifa Stars muda ule ule inatesti tena

BAADA ya kuchemsha kwenye mechi ya kwanza ya michuano maalumu ya Fifa Series mbele ya Bulgaria, timu ya taifa, Taifa Stars inatarajiwa kushuka uwanja ule ule na muda ule ule kuvaana na Mongolia.

Ikiwa imeongezwa nguvu na straika chipukizi anayecheza Genk ya Ubelgiji, Kelvin John 'Mbappe' Stars itaikabili Mongolia inayotokea Bara la Asia ambayo ilifungwa pia katika mechi ya kwanza na wenyeji Azerbaijan, kwenye Uwanja wa Dalga uliopo Baku, kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania.

Timu hiyo inayonolewa na makocha, Hemed Suleiman 'Morocco' na Juma Mgunda, ililala bao 1-0 mbele ya Bulgaria iliyowahi kufika nusu fainali ya Fainali za Kombe la Dunia za 1994, licha ya kuonyesha soka tamu na kutengeneza nafasi nyingi zilizoshindwa kutumiwa na washambuliaji wa timu hiyo.

Michuano hiyo maalumu ya Fifa Series inahusisha nchi 24 kutoka mashirikisho sita tofauti duniani ikitengwa katika makundi manne manne katika nchi tano tofauti ikiandaliwa na kugharamiwa kila kitu na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Mchezo huo kwa Stars utakuwa wa mwisho katika kipindi hiki cha kalenda ya Fifa na itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Mongolia iliyopoteza pia bao 1-0 mbele ya wenyeji ambao usiku watakaibilia Bulgaria.

Tofauti na mechi ya awali dhidi ya Bulgaria, Stars katika mchezo wa kesho itawakosa baadhi ya nyota wa Simba na Yanga walioruhusiwa kuwahi kambi za klabu hizo zinazojiandaa na mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri.

Wachezaji wa tano wa timu akiwamo Kibu Denis na Mohammed Hussein 'Tshabalala' kutoka Simba na Ibrahim Hamad 'Bacca', Mudhathir Yahya na Clement Mzize wote wa Yanga walishaondoka kambini na kuwaacha wenzao wakiendelea na majukumu ya kujiandaa na mchezo huo wa leo.