Taifa Stars imepata kipimo sahihi

Muktasari:

  • Kikosi cha Stars kitacheza michezo miwili kesho machi 22, dhidi ya Bulgaria na Jumatatu Machi 325 dhidi ya Mongolia kwenye michuano hiyo inayohusisha timu 20 na inafanyika kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Baku Azerbaijan.

Kesho timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itacheza mchezo wa kirafiki wa mashindano maalumu ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa), Fifa Series 2024.


Kikosi cha Stars kitacheza michezo miwili kesho machi 22, dhidi ya Bulgaria na Jumatatu Machi 325 dhidi ya Mongolia kwenye michuano hiyo inayohusisha timu 20 na inafanyika kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Baku Azerbaijan.


Mashindano hayo madogo yanayochukua nafasi ya mechi za kirafiki za kimataifa za Fifa na yanashirikisha  timu nne kutoka Afrika, Ulaya na Asia.


Afrika inawakilishwa na Tanzania, Ulaya, Bulgaria na Asia ni  Azerbaijan na Mongolia.


Kwa ukanda wa Asia, AFC, kuna nchi za Bhutan, Brunei, Cambodia,  Mongolia, Sri Lanka.  

 
 CAF kuna Algeria, Cape Verde, Afrika ya Kati, Misri, Guinea ya Ikweta,  Guinea, Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia, CONCACAF kuna Bermuda, Guyana, CONMEBOLBolivia, OFC New Zealand, Papua New Guinea, Vanuatu na UEFA kuna Andorra, Azerbaijan, Bulgaria na Croatia.


Hii ni mara ya kwanza kwa Stars kucheza dhidi ya timu ya Taifa ya Bulgaria na Mongolia michezo ya kirafiki ya Fifa.


Tunaamini kwa kuwepo kwenye mashindano hayo, itasaidia kuendelea kuifanya Stars kuwa imara kwani ni mara chache sana imecheza na timu za Ulaya na Asia.


Mara nyingi imekuwa ikicheza mechi za kirafiki na mashindano na timu za Afrika na kutoka nje ya bara hili kucheza na mataifa makubwa zaidi, itasaidia kuifanya izidi kupata uzoefu ikiwamo kujitangaza kwa wachezaji wetu kwa ajili ya kupata nafasi ya kuitwa kwenye klabu kubwa Ulaya na Asia.


Tanzania inakua kisoka na kudhihirisha hilo ni ushiriki wake mara mbili kwenye Afcon za miaka ya hivi karibuni mwaka 2019 na 2023 ingawa imeishia hatua ya makundi.


Uthubutu wa kushiriki Afcon ni moja ya sababu za kukua kwa soka na hata Fifa imeona hilo na ndio maana imeipa ushiriki kwenye michuano hiyo maalumu ikiwa ni mara ya kwanza kuanzishwa ili kufanya timu za taifa duniani kukutana mara kwa mara na kutoka mabara tofauti.


Stars ianakutana na timu ngumu na hivyo licha ya kujipanga inatakiwa ijue pamoja na kuwa ni mechi za kirafiki ila inatambuliwa na Fifa na hivyo ni moja ya njia ya kuipandisha viwango kwenye orodha ya timu bora duniani.


Stars isichukulie tu ni mashindano dhaifu kutokana na kuwa ni ya kirafiki, kuna suala la wachezaji binafsi kutakiwa kuonyesha viwango vyao kwa masilahi yao wenyewe, hivyo wanatakiwa kupambana hasa.


Mwaka kesho Fainali za Afcon 2024 zitafanyika Morocco na tunaamini kikosi hiki hiki na ama wataongezwa baadhi ya nyota watashiriki kwenye michuano ya kufuzu inayotarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu.


Hivyo, kwa kushiriki michuano hii ya Fifa,itasaidia kuwaweka sawa kiuzoefu na hata kocha atapata picha ya kikosi chake wapi apunguze na wapi aongeze ili kujiandaa vyema na Afcon ya mwakani. Kila la Kheri Stars kwenye Fifa World Series.