Taifa Stars fanyeni kweli

Muktasari:

USHINDI wa ugenini dhidi ya Benin leo ndio matokeo pekee yatakayofufua ndoto za Taifa Stars kutinga hatua ya mwisho ya mtoano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Qatar mwakani.

USHINDI wa ugenini dhidi ya Benin leo ndio matokeo pekee yatakayofufua ndoto za Taifa Stars kutinga hatua ya mwisho ya mtoano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Qatar mwakani.

Baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 nyumbani, juzi Alhamisi, Stars inahitajika kupata ushindi wa ugenini leo ili ifikishe pointi saba zitakazoifanya iifikie Benin na kisha kuhamishia nguvu zake katika mechi mbili za mwisho dhidi ya DR Congo na Madagascar ili kujaribu kumaliza ikiwa ya kwanza kwenye msimamo wa Kundi J na kutinga hatua ya mwish ya mtoano.

Lakini ikiwa matokeo yatakuwa ni ya sare au kupoteza, kiuhalisia matumaini ya Stars kumaliza ikiwa kinara kwenye kundi hilo yatakuwa finyu kwani italazimika kuibuika na ushindi katika mechi mbili za mwisho huku ikiombea wapinzani wake wafanye vibaya ili waweze kusonga mbele.

Stars inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi isiyovutia katika mechi za ugenini na uthibitisho wa hilo katika mechi 10 za mwisho ilizocheza hivi karibuni imeshinda michezo miwili, imetoka sare mara tatu na kupoteza michezo mitatu

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Stars, wenyeji Benin wamekuwa wakifanya vizuri pindi wawapo nyumbani mfano katika mechi 10 za hivi karibuni, imeshinda tatu, imetoka sare sita na kupoteza moja.

Katika mchezo wa leo utakaochezwa kwenye Uwanja wa l’Amitié, uliopo jijini Cotonou kuanzia saa 8 jioni kwa saa za huko sawa na saa 10 kwa muda wa Afrika Mashariki na Stars itawakosa Mzamiru Yassin anayetumikia adhabu ya kutokana na kupata kadi mbili za njano pamoja na beki Erasto Nyoni ambaye bado anauguza majeraha yake.

Kocha wa Stars, Kim Paulsen alisema pamoja na kupoteza mechi iliyopita nyumbani, bado wana matumaini ya kupata ushindi dhidi ya Benin ugenini.

“Tumepoteza pambano lakini sio vita. Tulikuwa na uwezekano wa kupata ushindi nyumbani lakini hatukuweza kuzitumia vyema kufunga mabao na wenzetu wakapata moja ambayo waliitumia vizuri wakapata bao lao pekee la ushindi.

“Mechi hii ni ngumu lakini naamini tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huu ili kuweka hai matumaini yetu ya kufanya vizuri katika mashindano haya,” alisema Paulsen.

Mchezo mwingine wa kundi J utakuwa huko Antananarivo kwa wenyeji Madagascar ambao hawana pointi wataikaribisha DR Congo.