Sven akabidhiwa faili la Kichuya, winga Mkongo

Muktasari:

Uongozi wa Simba kwa maana hiyo ulikuwa na majina ya wachezaji wawili straika kutokea KCCA ya Uganda na Tuisila Kisinda, kutokea AS Vita ya nchini DR Congo.

KOCHA wa Simba, Sven Ludwig Vandenbroeck, amepewa muda wa siku 14 na mabosi wake kupeleka mahitaji ya kikosi huku akiachiwa hatima ya Mkongo Tuisila Kisinda na nyota wa zamani wa timu hiyo, Shiza Kichuya anayetajwa kutaka kurejea Msimbazi.

Sven ameachiwa jukumu la kujua wachezaji gani anaotaka wasajiliwe kulingana na upungufu na pia kupendekeza wa kumtoa kwa mkopo kupitia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa jana Jumatatu na litakalofungwa Januari 15.

Kabla ya kuwasili kwa Sven, tayari uongozi wa Simba ulikuwa na majina mawili ya wachezaji ambao walitaka kuwasajili katika dirisha dogo kutoka na ripoti ambayo iliachwa na kocha aliyeondoka Patrick Aussems.

Ripoti hiyo ya Aussems, ilikuwa inataka asajiliwe mchezaji mmoja ambaye ni mshambuliaji kutokana na upungufu wa timu hiyo ambao ulitokana na majeraha ya mara kwa mara ambayo alikuwa akiyapata John Bocco na Wilker Da Silva, ambao wote wawili kwa sasa ni wazima.

Uongozi wa Simba kwa maana hiyo ulikuwa na majina ya wachezaji wawili straika kutokea KCCA ya Uganda na Tuisila Kisinda, kutokea AS Vita ya nchini DR Congo.

Baada ya kuwasili kwa Sven, uongozi wa Simba chini ya Ofisa Mtendaji Mkuu Senzo Mazingisa, alisema wamempa kwanza wiki mbili kocha wao ili aweze kukifanyia tathmini kikosi hicho na kueleza maeneo gani ambayo yanatakiwa kuongezwa nguvu katika dirisha dogo.

“Sasa hivi Sven anafanya kazi ya kuandaa timu na kila mchezaji kumfuatilia mmoja mmoja ili kuona upungufu na ubora wake, na baada ya hapo tutafanya kikao na kujadiliana kipi ambacho amekiona na ambacho anataka afanyiwe,” alisema.

“Sitaweza kumsajili yeyote kwanza mpaka hapo ambapo nitajadiliana na benchi la ufundi na wao kutoa maamuzi ya aina ya wachezaji ambao wanawataka na kila katika nafasi moja atakuwepo chaguo la kwanza mpaka la tatu ili kuwa na uwanja mpana wa kuchagua.

“Katika hizi wiki mbili Sven, anaendelea kuandaa timu kwa ajili ya kucheza mechi za Kombe la FA, Ligi Kuu Bara, kufuatilia ubora na upungufu wa wachezaji waliokuwepo na hata majina ya nyota wapya tuliompatia akiwemo Tuisila, baada ya hapo ndio tutafanya maamuzi katika hili.”

KICHUYA ANARUDI

Katika hatua nyingine Mwanaspoti lilipata taarifa kutoka ndani ya Simba kuwa winga wa Pharco inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Misri, Kichuya, anaweza kurejea katika timu yake ya zamani baada ya kumuza msimu uliopita.

Kichuya aliuzwa na Simba kutokana na kutokuwa mchezaji chaguo la kwanza mbele ya Aussems na pia kitendo chake cha kutaka kucheza soka la kulipwa hasa walipowekewa mezani, lakini amekuwa na wakati mgumu tangu aondoke na kwa sasa inaelezwa yupo njiani kurudi.

Senzo alikiri taarifa za kumtaka Kichuya kama watakubaliana na mchezaji huyo na katika maeneo mengine yote ya msingi, lakini hataweza kumpitisha mpaka hapo benchi la ufundi chini ya kocha Sven litakapo kubali.

“Kama Sven atamkubali Kichuya anaweza kurudi tena katika timu kwani ni mchezaji mzuri lakini benchi la ufundi ndio lenye maamuzi ya mwisho na si peke yake bali hata wachezaji wengine wote ambao tunataka kuwasajili,” alisema Senzo.