Sunzu: Simba sajili hapa

Muktasari:

  • Simba imepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, huku ikitolewa 16 bora ya Kombe la Shirikisho, robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na kupoteza fainali ya Kombe la Mapinduzi, hivyo kukosa makombe hayo iliyoshiriki msimu huu, ikiambulia Ngao ya Jamii.

KIPIGO cha mabao 2-1 kutoka kwa watani wao, Yanga ni kama kimeiondoa Simba kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na hesabu msimu huu kumalizika, lakini nyota wa zamani wa timu hiyo, Felix Sunzu ameipa njia ya kupita kwenye usajili.

Simba imepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, huku ikitolewa 16 bora ya Kombe la Shirikisho, robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na kupoteza fainali ya Kombe la Mapinduzi, hivyo kukosa makombe hayo iliyoshiriki msimu huu, ikiambulia Ngao ya Jamii.

Sunzu, raia wa Zambia ambaye kwa sasa anaishi nchini, amependekeza maeneo yanayopaswa kufanyiwa maboresho na kuletwa wachezaji wapya wenye viwango vya juu kuwa ni washambuliaji wawili, beki wa pembeni na kiungo mchezeshaji atakayemsaidia Clatous Chama.

“Chama ni mchezeshaji akichoka hakuna msaidizi mwingine kwa hiyo anatakiwa mtu mwenye uwezo kama wake, pia watafute washambuliaji wawili wenye mbio na wanaoweza kuchunga mpira. Fredy (Michael) ni mzuri kuzuia mpira lakini ni mvivu haendani na kasi ya mpira wa hapa,” amesema.

“Watafute na beki kule kwa kipa hatuwezi kugusa kipa ni mzuri mabao anayofungwa yanatoka kwa mabeki. Kapombe siyo kwamba amechoka lakini ni wa kumpumzisha ni mchezaji mzuri anapaswa kuwa na wa kumsaidia.”

Mshambuliaji huyo ameshauri kwamba maboresho hayo yanatakiwa kuanza sasa wakati ligi ikiendelea kwa kutafuta wachezaji ili msimu unapoanza waanze maandalizi mapema na kutengeneza muunganiko.

“Lakini wanapaswa pia kuwaamini na kuwapa muda wachezaji wao na makocha na siyo kubadili kila wakati, mpira wa Tanzania ni mgumu mchezaji anapaswa kuambiwa unapokuja hapa unatakiwa uanze kufunga hii timu iko hivi na hivi kwahiyo anafunguka akili,” amesema.

“Benchikha siyo mbaya lakini nadhani kinachompa shida nimeenda kwenye mazoezi yao wachezaji hawapumziki wanafanya mazoezi hawana hamu ya kucheza. Wanacheza vizuri sasa ile kupumua mazoezi yanapitiliza kwa sababu kocha anataka matokeo.”