Straika wa AFC Leopards amfuata Matasi

Muktasari:

Mnigeria Alex Orotomal, alijiunga na AFC Leopards, mwezi Juni mwaka huu, akitokea katika klabu ya Sunrise FC ya nchini Rwanda, akisaini mkataba wa miaka miwili ya kuisaidia Ingwe kupata mabao, kazi ambayo hadi anaondoka alishindwa kuifanya kikamilifu.

Nairobi, Kenya. Baada ya kutangaza kukamilisha usajili wa Mlinda lango wa Harambee Stars na Klabu ya Tusker FC, Patrick Matasi, klabu ya St. George ya Ethiopia, imekamilisha dili la kumsajili Straika wa AFC Leopards, Mnigeria Alex Orotomal.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoifikia Mwanaspoti Digital ni kwamba, Orotomal aliyejiunga na Ingwe msimu uliomalizika, amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia klabu hiyo, ambayo iko katika harakati ya kukisuka upya kikosi chake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi nchini Ethiopia.

Orotomal anakuwa mchezaji wa pili kuigura ligi kuu ya Kenya (KPL), baada ya Patrick Matasi kutua Addis Ababa Jana, akisaini dili la miaka mitatu ya kurithi nafasi iliyowachwa wazi na mlinda lango wa Uganda, Robert Odongkara.

"Alex Orotomal amekubali kusaini mkataba na St George. Ametia wino wa kukipiga katika klabu kwa miaka miwili. Anakuwa nyota wan ne kutua Jijini Addis Ababa, tumejipanga kuhakikisha tunakuwa sawa kabla ya msimu kuanza,” ilisema sehemu ya taarifa kutoka kwa mtandao wa klabu hiyo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa AFC Leopards walikubali kumuachia Straika huyo baada ya St. George, kuweka kiasi cha Ksh. 1.5 mezani. Kuondoka kwake kunaifanya Ingwe kusalia na Ezekiel Odera na Vincent Oburu kama washambuliaji pekee.