Yanga, Mashujaa vita ipo hapa

Muktasari:

  • Yanga inaongoza msimamo kwa pointi 62 imebakiza michezo minne kutetea taji lake wakati Mashujaa ipo nafasi ya 14 ikikusanya pointi 23 kwenye mechi 24 ilizocheza.

Yanga inashuka katika mchezo wa leo kusaka pointi tatu ili kuendelea kuusogelea ubigwa wa Ligi Kuu Bara wakati Mashujaa wao wanatafuta ushindi wa kujikwamua kurudi walipotoka.

Yanga inaongoza msimamo kwa pointi 62 imebakiza michezo minne kutetea taji lake wakati Mashujaa ipo nafasi ya 14 ikikusanya pointi 23 kwenye mechi 24 ilizocheza.

Mchezo huo utakuwa wa muhimu zaidi kwa timu zote mbili kila timu ikisaka pointi kujiweka kwenye mazingira mazuri kwani Yanga itapunguza gepu la kuwania taji wakati Mashujaa wakishinda watapanda nafasi mbili kutoka 14 hadi 12.

Mashujaa ili iwe na uhakika wa kubaki msimu ujao inatakiwa ishinde mechi zake zote sita zilizobaki kwa idadi kubwa ya mabao kutokana na kupishana idadi ya mabao ya kufungwa na kufunga na mpinzani wake kwenye msimamo Tabora United wote wana pointi sawa.

Kama itashinda mechi zake zote sita ikiwemo ya leo dhidi ya Yanga itafikisha pointi 41 ambazo zitakuwa sawa na Tabora United iliyo nafasi ya 15 endapo nayo itashinda michezo yake yote utofauti utakuwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Endapo itapoteza mchezo huo itakuwa inajichimbia kaburi yenyewe kurudi ilipotoka kwani ilipanda daraja msimu huu.

Yanga ina rekodi nzuri kwenye mechi zake tano za hivi karibuni imepoteza mchezo mmoja dhidi ya Azam FC 2-1, imeshinda mechi tatu na suluhu moja.

Kwa upande wa Mashujaa wao kwenye mechi tano za hivi karibuni imeshinda mchezo mmoja suluhu mbili na kipigo kimoja.

Timu hizo zimekutana mara moja kutokana na Mashujaa kupanda daraja msimu huu hivyo mzunguko wa kwanza Yanga wakiwa nyumbani walishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya, huku bao la kufutia machozi upande wa Mashujaa lilifungwa na Emmanuel Mtumbuka.

Licha ya Yanga kuwa timu imara kwenye maeneo mengi ukiwamo ukuta wake ulioruhusu bao moja kwenye mechi nane zilizopita za mashindano yote hivi karibuni, utatakiwa kumchunga staa wa timu hiyo Adam Adam ambaye amepachika mabao saba hadi sasa.

Yanga katika mechi nane za michuano yote ilianza dhidi ya Mamelodi nyumbani na ugenini (0-0), Dodoma Jiji (2-0), Singida Fountain Gate (3-0), Simba (1-2), JKT Tanzania (0-0), Coastal Union (0-1) na Tabora United (0-3).

Hivyo ili kulinda rekodi hiyo Yanga watatakiwa kumchunga Adam asiweze kuvuka ukuta wao na hatimaye kuwafunga lakini pia kwa upande wa Mashujaa watatakiwa kuwa makini na Stephane Aziz Ki kinara wa mabao akipachika kambani (15).

Bato jingine kubwa na ambalo litaamua matokeo kwenye mchezo huo ni eneo la kiungo ambalo kwa upande wa Yanga limetawaliwa na viungo mahiri wenye jicho la kuona goli Aziz Ki na Mudathir Yahya ambaye aliwafunga bao la ushindi mzunguko wa kwanza wakati wao wakiwa na Mapinduzi Balama ambaye anaifahamu vizuri Yanga kutokana na kuitumikia kabla ya kutua hapo.

BARESI vs GAMONDI

Eneo jingine la kuamua matokeo ni mbinu za makocha wa pande zote mbili namna zitakavyopanga vikosi vyao kwaajili ya kuamua mchezo huo ndani ya dakika 90.

Mashujaa ambayo ndio timu mwenyeji wa mchezo ipo chini ya Mohammed Abdallah ‘Baresi’ huku Yanga ikiwa chini ya Miguel Gamondi.

Kocha wa Mashujaa, Baresi amesema wanatarajia mchezo mgumu na wa ushindani huku akibainisha kuwa wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata matokeo mazuri yatakayorudisha matumaini ya wao kubaki msimu ujao.

“Yanga ina timu nzuri na bora ina wachezaji walio wakomavu, hatutarajii mteremko tunaingia kwa kuwaheshimu lengo ni kuona tunaibuka na ushindi na kuendeleza kampeni ya kubaki msimu ujao,” alisema.

Gamondi kocha wa Yanga amesema kila mchezo ulio mbele yao ni fainali hivyo wanaingia kwa kumuheshimu mpinzani huku malengo ni kutwaa taji kabla ya kumaliza msimu.

“Ninajivunia kuwa na timu yenye njaa ya mafanikio naamini tulichokifanya kwenye mazoezi ya mwisho ndio kitafanyika ndani ya dakika 90 za mchezo lengo ni ushindi lakini hauwezi kupatikana bila juhudi za mchezaji mmoja mmoja.” alisema.