Straika Simba aipa Yanga ubingwa

NYOTA wa zamani wa kimataifa wa Simba, Eric Sagalla ameshindwa kujizuia na kuipa Yanga ndoo ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu akitaja sababu ni aina ya wachezaji iliyonayo wanaojituma na kuwa na kiu ya kupata matokeo mazuri.

Sagalla aliyeanzia soka lake CDA Dodoma kabla ya kutua Simba 1987 na kuichezea hadi 1990 kisha kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Botswana katika timu za Township Rollers na BDF 1X kati ya Mwaka 1990-1993, alisema anaipa nafasi Yanga kwa vile ina kikosi kipana tofauti na wengine.

“Simba inacheza kama haitaki, angalia wakifungwa wanacheza kama wameshinda, lakini iangalie Yanga, ikifungwa kila mmoja ana haha uwanjani kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.”

“Pia Yanga ina wachezaji wapambanaji kama Fiston Mayele ambaye muda wote anataka kufunga na akipata nafasi anafunga, lakini kila mpira wanaopata wanampelekea Mayele na anafunga, hiyo ndio inatakiwa,” alisema Sagalla aliyecheza pia soka la kulipwa Afrika Kusini.

Hata hivyo, amewashauri wachezaji wa sasa kujituma na kujitambua ikiwa ni pamoja na kutafuta washauri sahihi.

“Mtu anatoka Mali, anakuja kuchukua tu hela wakati tuna vijana wana vipaji tatizo wanawahi kuridhika wakati mbele ndio kuna hela zaidi.”