Straika Mashujaa kuibukia AS Vita

Muktasari:
- AS Vita inamtaka Mgunda kwenda kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji, ambapo nyota huyo ni mmoja wa mastaa wanaotakiwa na kocha wa kikosi hicho, Youssouph Dabo ambaye ni kocha wa zamani wa Azam FC.
MASHUJAA FC iko kwenye hatua za mwisho kufanya biashara na AS Vita ya DR Congo ambayo inamtaka mshambuliaji Ismail Mgunda.
AS Vita inamtaka Mgunda kwenda kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji, ambapo nyota huyo ni mmoja wa mastaa wanaotakiwa na kocha wa kikosi hicho, Youssouph Dabo ambaye ni kocha wa zamani wa Azam FC.
Mgunda ambaye msimu huu ameifungia Mashujaa mabao mawili, Dabo anamtaka kwenda kuimarisha safu ya ushambuliaji iliyofunga mabao 16 ikiongoza kundi baada ya mechi 12.
Taarifa kutoka DR Congo zinasema wakati wowote Mgunda atasafiri kwenda kufanyiwa vipimo vya afya na endapo atafuzu atasaini mkataba wa miaka miwili. “Tumeshakubaliana kila kitu juu ya Mgunda na klabu yake. Atakuja wakati wowote kumalizia hatua ya mwisho,” alisema mmoja wa mabosi wa AS Vita.
Wakati AS Vita ikisema hivyo, Mashujaa imeonyesha kukubaliana na taarifa hizo ikisema bado dili hilo halijakamilika, lakini mazungumzo ya mwisho yanaendelea.
“Kuna hiyo biashara kweli, lakini kwa sasa naomba muiache kwanza tumalizane na mchezaji asafiri akifika huko mtajulishwa,” alisema bosi mmoja wa Mashujaa.
AS Vita imenunuliwa na tajiri wa Kituruki aliyepania kuibadilisha timu hiyo ambapo mbali na Mgunda pia inamtaka beki Laurean Makame wa Fountain Gate.