Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Straika aitosa Dodoma Jiji

Muktasari:

  • Nyota huyo amewashukuru mashabiki, viongozi, benchi la ufundi na kila mmoja aliyemuamini, huku akijivunia mafanikio na changamoto mbalimbali alizopita katika kipindi hicho chote cha misimu mitatu aliyoichezea timu hiyo hadi msimu unaisha.

LICHA ya uongozi wa Dodoma Jiji kumuwekea mkataba mpya wa miaka miwili mshambuliaji wa kikosi hicho, Paul Peter Kasunda, ila nyota huyo ameamua kutafuta changamoto sehemu nyingine, huku akiishukuru timu hiyo kwa nafasi iliyompa kuitumikia kwa misimu mitatu.

Nyota huyo amewashukuru mashabiki, viongozi, benchi la ufundi na kila mmoja aliyemuamini, huku akijivunia mafanikio na changamoto mbalimbali alizopita katika kipindi hicho chote cha misimu mitatu aliyoichezea timu hiyo hadi msimu unaisha.

“Asanteni Dodoma Jiji na wasimamizi wangu kwa upendo na heshima kubwa mliyonipa, uwepo wenu kwangu umekuwa nguzo muhimu katika safari yangu, naamini mwisho ni mwanzo mwingine,” aliandika Paul katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Mshambuliaji huyo aliyeonyesha kiwango bora msimu wa 2024-2025, mkataba wake umeisha na uongozi wa Dodoma Jiji tayari ulianza mazungumzo ya kumuongezea miaka miwili zaidi, ingawa ushawishi huo umegonga mwamba na sasa anasikilizia ofa nyingine.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilipomtafuta mshambuliaji huyo kuzungumzia suala hilo, alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa maslahi ya pande zote mbili, ingawa sehemu au timu atakayochezea kwa msimu ujao itajulikana muda sio mrefu.

“Nafikiri muda ukifika wa timu gani nitacheza msimu ujao basi nitaweka wazi, ila kwa sasa mashabiki zangu watambue bado sijafanya uamuzi wowote kwa sababu ndio kwanza tumemaliza msimu na yapo pia mambo mengi yanaweza kutokea,” alisema Paul.

Taarifa zinaeleza, Al Dahra Tripoli FC ya Libya bado inamuhitaji mshambuliaji huyo kwa ajili ya kuongeza nguvu, baada ya ofa ya kwanza waliyoiwasilisha Januari 2025, kugonga mwamba kwa kile kilichoelezwa waliwasilisha kiasi kidogo cha fedha.

Nyota huyo wa zamani aliyekulia akademi ya Azam FC kisha kupandishwa timu ya wakubwa, akiichezea pia KMC FC na Tanzania Prisons, amefunga mabao manane ya Ligi Kuu Bara na kuasisti mawili kati ya 31, yaliyofungwa na kikosi hicho msimu huu.