Storelli : Siri ya makali ya Rooney na kifaa anachovaa kichwani

Muktasari:
- Kwenye mchezo huo, Rooney alionekana akiwa amevaa kifaa maalumu kilichomkinga jeraha lake na kuonekana kucheza bila ya wasiwasi wowote katika mchezo ambao alifunga bao maridadi kwa mpira wa adhabu ndogo kwenye ushindi wa mabao 2-0.
LONDON,ENGLAND
KAMA ukimuuliza, Martina Dolejsova, ambaye ni mke wa kipa, Petr Cech, anaweza kusema nini kuhusu soka, bila shaka atasema kuwa hataki kuona mumewe anatokewa na kilichomtokea mwaka 2006.
Bahati nzuri, Martina hakuliona tukio la mumewe kugongana na mchezaji wa Reading, Stephen Hunt, lililomsababishia kuvunjika mfupa wa kichwa na hivyo kuwekewa vyuma. Lakini, tangu hapo, kila anaposikia mumewe ameumia uwanjani, anakuwa na hofu kubwa kama endapo tukio hilo linafanana na lile la mwaka 2006.
Mwaka 2011 kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Fulham, wakati Cech alipoumizwa na Orlando Sa na kupelekwa hospitali, tukio hilo lilimpa hofu mkewe, lakini yeye mwenyewe anachoshukuru ni kifaa anachovaa kukinga fuvu la kichwa tangu alipoumizwa na Hunt.
Madaktari walimwambia Cech kuwa yupo salama, lakini yeye hajawahi kucheza bila ya kuvaa kifaa hicho tangu tukio hilo. Bado haifahamiki kuhusu mrembo, Coleen, mke wa straika wa Manchester United, Wayne Rooney, kama kuna hofu yoyote aliyopata baada ya mumewe kupata jeraha kubwa usoni baada ya kuumizwa mazoezini.
Aliumizwa mazoezini na mchezaji, Phil Jones na kumsababisha Rooney kukosa mechi ya kimataifa ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwakani na kikosi chake cha England.
Hata hivyo, wakati watu wakiamini kwamba straika huyo angekaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuuguza jeraha hilo, Rooney alirejea ndani ya uwanja na kucheza mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace iliyofanyika Old Trafford na kushangaza wengi.
Kwenye mchezo huo, Rooney alionekana akiwa amevaa kifaa maalumu kilichomkinga jeraha lake na kuonekana kucheza bila ya wasiwasi wowote katika mchezo ambao alifunga bao maridadi kwa mpira wa adhabu ndogo kwenye ushindi wa mabao 2-0.
Kifaa chenyewe
Kifaa hicho kimetengezwa na Kampuni ya Storelli yenye maskani yake jijini New York, Marekani. Ni kifaa mahususi kwa ajili ya wanamichezo, hususan wanasoka.
Kutokana na jeraha hilo la kichwani, jopo la madaktari liliketi na kutafuta namna ya kuhakikisha Rooney anarejea uwanjani haraka na hivyo kumtafutia kifaa cha kumkinga.
Ndipo walipoagiza kifaa hicho kutoka Marekani na kukijaribu kuona kama kitamfaa akikivaa kujikinga.
Ilipofika Alhamisi usiku wiki iliyopita, walifanikiwa kukipata na asubuhi yake, Rooney alivaa kifaa hicho kwenye mazoezi na ikaonekana inafaa kuvaa kwenye mechi.
Kinafanyaje kazi?
Kichaa hicho kinafahamika kwa jina la ‘ExoShield HeadGuard’, ni maalumu kwa ajili ya kuwakinga wachezaji waliopata majeraha ya kichwani hasa kwenye paji la uso.
Jopo la wataalamu wa ubunifu waliketi na kuibuka na wazo la kubuni kifaa hicho cha kuvaa kichwani kwa ajili ya kuwakinga wachezaji walioumia kwenye maeneo hayo ili kukinga mfupa wa kichwa usipate majeraha zaidi.
Kimetengenezwaje?
Vifaa vilivyotumika kwenye utengenezaji wa kifaa hicho havina tofauti na vile vinavyotumika kwenye kutengeneza kofia maalumu za jeshi la Marekani pindi wanapokuwa na shughuli maalumu.
Vitu vinavyotumika kutengenezea kifaa hicho vina uwezo mkubwa wa kuhimili mgandamizo na kupunguza makali yake kwa asilimia 50. Kifaa hicho kimeundwa kwa ajili ya matumizi ya kwenye hali ya hewa ya aina yoyote kwa maana hakiwezi kuwa kigumu kwenye hali ya baridi au kuwa laini kwenye joto.
Watumiaji wake
Kwenye Ligi Kuu England, Wayne Rooney kwa sasa ndiye mchezaji maarufu kutumia kifaa hicho, lakini nchini Marekani, wanasoka wa kike ndio wanaokivaa mara nyingi.
Nchini England kifaa hicho ni maarufu sana ukilinganisha katika nchi za Marekani, Canada, Australia, Colombia na Italia ambapo soko lake limekuwa kubwa.
Kimemgharimu pesa kiasi gani?
Imemgharimu straika huyo wa Manchester United Pauni 38 kukipata kifaa hicho, ambapo kwa nchini Marekani gharama yake ni Dola 60.
Chaanza kuhusishwa kiimani
Tangu alipoonekana na kichaa hicho, Rooney amefunga mara tatu katika mechi mbili, huku kiwango chake kikiwa kikubwa na kuwafanya baadhi ya watu kumtaka mchezaji huyo aendelee kukivaa wakiamini ni kitu chenye bahati kwa upande wake.
Jumanne iliyopita kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Rooney alifunga mabao mawili na kutengeneza moja katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Bayer Leverkusen, huku kiwango alichoonyesha kwenye mechi hiyo kikiwa ni mwendelezo wa kile alichokionyesha kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace Jumamosi iliyopita.
kwenye mazoezi ya kujiandaa na mechi ya Mabingwa Ulaya, Rooney alifanya bila ya kuvaa kifaa hicho, lakini ilipofika mechi yenyewe alivaa na kuonyesha kiwango bora. Kutokana na hilo, tayari kumekuwa na imani kwamba huenda, straika huyo akaendelea kuvaa kwa sababu kimempa bahati ya kucheza kwa kiwango kizuri.
Sheria za Fifa zinasemaje?
Kwa sheria za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), ni kwamba mchezaji hapaswi kuvaa kifaa ambacho kitasababisha madhara kwa wengine na kwake mwenyewe, lakini vifaa vya kisasa vinavyotengenezwa kwa vitu laini kwa ajili ya kuwakinga wachezaji wenye matatizo vinaruhusiwa kama si hatarishi kwa mchezaji mwenyewe na kwa wenzake.
Kocha Moyes
David Moyes alisema uamuzi wa kumtumia Rooney katika mechi ya Ligi Kuu ikiwa ni wiki moja tangu ashindwe kuichezea England ulisababishwa na kupatikana kwa kifaa hicho.
Moyes alisema baada ya kuona wamepata kitu ambacho kingemfanya Rooney kuwa salama, walikifanyia majaribio na hivyo kumvisha straika huyo kwenye mechi mbili mfululizo na kuonyesha makali ya hali ya juu.
Kesho Jumapili, Manchester United itakuwa na shughuli pevu mbele ya mahasimu wao wa Jiji la Manchester, Manchester City kwenye mechi ya Ligi Kuu na kuna dalili zote za kumshuhudia Rooney akiendelea kuvaa kifaa hicho kichwani.
Moyes anasema siri ya kumwona Rooney anafanya vyema ni kwa sababu anacheza bila ya hofu ya kutonesha jeraha lake kutokana na kifaa hicho cha kujikinga.