Star wa Black Panther afariki, aacha movie inatengenezwa

Muktasari:

Enzi za uhai wake Chadwick alicheza movie nyingi kali ikiwemo Black Panther (maarufu Wakanda) ambayo ndiyo iliyompa umaarufu zaidi duniani kote.

MAREKANI. Leo ulimwengu wa wapenda filamu duniani kote umepata pigo kubwa baada ya kutangazwa kifo cha aliyekuwa muigizaji wa Marekani Chadwick Boseman, 43.

Enzi za uhai wake Chadwick alicheza movie nyingi kali ikiwemo Black Panther (maarufu Wakanda) ambayo ndiyo iliyompa umaarufu zaidi duniani kote.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia, kifo cha Chadwick kimesababishwa na saratani ya utumbo mpana (colon cancer), ambayo aligundulika nayo tangu mwaka 2016. Hata hivyo hakuwahi kujitangaza hadharani, badala yake alipambana nayo kimya kimya huku akiendelea kucheza filamu na tamthilia mpaka usiku wa kuamkia leo ilipomchukua.

Kabla ya kifo chake Chadwick alikua na madili kibao ya kutengeneza filamu kubwa baada ya movie ya Black Panther kumpaisha. Miongoni mwa madili hayo ni Movie ya Black Panther 2 pamoja na Black Samurai ambayo ilikuwa inatarajiaa kuanza kutengenezwa mwaka huu — movie ambayo ni stori ya kweli kuhusu Samurai wa kwanza mweusi alifanya kazi katika tawala za Kijapani karne ya 16.

Chadwick alikuwa na mke mmoja, mwanamuziki Taylor Simone na hawakubahatika kupata mtoto. Hata hivyo, moja ya sifa kubwa ya Chadwick ilikuwa ni kutokuweka maisha yake hadharani kwani hata ndoa yake na Taylor haikuwahi kujulikana kwenye makamera ya paparazi.