Staa Simba aanika mazito

Muktasari:

  • Lakini amekwenda mbali zaidi kwa kudai hata mazoezi ya Kocha Abelhak Benchikha yanatumia muda mrefu sana ambao unachosha wachezaji na akasisitiza pia kwa kipa Ayoub Lakred hana tatizo.

STRAIKA wa zamani wa Simba, Felix Sunzu ametoa ya moyoni kuhusu mwenendo wa timu hiyo na kuonyesha sehemu ambazo zinahitaji mabadiliko ya haraka kama kweli viongozi wanataka mafanikio.

Lakini amekwenda mbali zaidi kwa kudai hata mazoezi ya Kocha Abelhak Benchikha yanatumia muda mrefu sana ambao unachosha wachezaji na akasisitiza pia kwa kipa Ayoub Lakred hana tatizo.

Sunzu ambae ni raia wa Zambia kwa sasa anaishi Kanda ya Ziwa, alipendekeza maeneo yanayopaswa kufanyiwa maboresho na kuletwa wachezaji wapya wenye viwango ni washambuliaji wawili, beki wa pembeni na kiungo mchezeshaji atakayemsaidia Clatous Chama.

“Chama ni mchezeshaji akichoka hakuna msaidizi mwingine kwa hiyo anatakiwa mtu mwenye uwezo kama wake, pia Simba watafute washambuliaji wawili wenye mbio na wanaoweza kuzuia na kushambulia kwa madhara. Fredy (Michael) ni mzuri kuzuia mpira lakini ni mvivu haendani na kasi ya mpira wa hapa,”alisema Sunzu ambaye asili yao ni DR Congo.

“Watafute na beki kule kwa kipa hatuwezi kugusa kipa ni mzuri mabao anayofungwa yanatoka kwa mabeki. Kapombe siyo kwamba amechoka lakini ni wa kumpumzisha ni mchezaji mzuri anapaswa kuwa na wa kumsaidia,” alisema Sunzu aliyesajiliwa Simba 2011 akitokea Al Hilal ya Sudan.

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa kwenye kikosi kilichoifunga Yanga 5-0 katika mechi ya kufungia msimu wa 2011-12,ameshauri na maboresho hayo yanatakiwa kuanza sasa wakati ligi ikiendelea kwa kutafuta wachezaji ili maandalizi yaanze mapema na kutengeneza muunganiko kuliko kukurupuka dakika za presha timu zote zikiwa sokoni.

“Lakini wanapaswa pia kuwaamini na kuwapa muda wachezaji wao na makocha na siyo kubadili kila wakati, mpira wa Tanzania ni mgumu mchezaji anapaswa kuambiwa unapokuja hapa unatakiwa uanze kufunga hii timu iko hivi na hivi kwahiyo anafunguka akili,” aliongeza Sunzu mwenye miaka 38.

“Benchikha siyo mbaya lakini nadhani kinachompa shida nimeenda kwenye mazoezi yao wachezaji hawapumziki wanafanya mazoezi muda mrefu sana hawana hamu ya kucheza. Mazoezi yanapitiliza kwa sababu kocha anataka matokeo,” alisema Sunzu ambaye ameoa Mtanzania.

Aliongeza kuwa ameangalia mazoezi ya Simba mara kadhaa na yale ya Yanga kuna utofauti mkubwa kwani Jangwani wanapata muda wa kupumua na kutafakari.


KUHUSU BENCHIKA
Viongozi wa matawi Nyanda za Juu Kusini, wammkingia kifua Kocha Mkuu, Abdelakh Benchikha wakisema asiguswe.
Katika michezo miwili waliyokutana na Yanga kwenye Ligi Kuu, Wekundu wamepigika nje ndani wakianza na kisago cha 5-1 raundi ya kwanza na juzi Jumamosi wakalala 2-1.

Katibu wa wanachama na mashabiki wa Simba mkoani Songwe, Dany Mgivilwa alisema Benchikha hahusiki kwa namna yoyote bali timu inahitaji mabadiliko kwa kusajili wachezaji wenye ubora.

Alisema kikosi hicho kinakosa straika mwenye makali, lakini eneo la beki linahitaji kupata nguvu mpya wa kuwasaidia Mohamed Husein, Henock Inonga na Shomari Kapombe.

“Wachezaji hawajitumi, wala Kocha hana hatia kwenye hili bali tujipange msimu ujao kwa usajili wenye mashiko, ikiwezekana ifumuliwe timu walete straika, mabeki na kiungo mkabaji,” alisema Mgivilwa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Simba mkoani Mbeya, Yusuph Mwambete alisema namna ya kuirudisha timu hiyo kwenye ubora ni muunganiko kwa viongozi wa juu.
Alisema haoni sababu ya kosa la Benchikha kwani kipo kitu ambacho uongozi unafeli kukifanya haswa kukosekana kwa muunganiko baina ya viongozi wa juu ndio inaipa msoto timu.

“Tunao washambuliaji wawili, Pa Omary Jobe na Fredy Michael kama hawafiti kwenye mfumo wa Kocha basi uwezo wao ni mdogo, lazima viongozi wenyewe wajitathimini,” alisema Mwambete.

Naye Paschal Mwila mwenyekiti wa timu hiyo mkoani Ruvuma alisema sehemu ya kufanyia maboresho ni eneo la straika na beki akieleza kuwa haoni tatizo kwenye benchi la ufundi.