Staa aoa kwa Sh1 Milioni tu, kisa Kombe la Dunia

ya kiungo wa Southampton, Adam Lallana, akiwa na mke wake walipofunga ndoa. Picha na AFP
Muktasari:
- Lallana amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu kwenye kikosi cha Southampton na jambo hilo limemfanya aitwe mara mbili kuichezea timu ya taifa ya England chini ya kocha Roy Hodgson.
KURASA ya mbele ya Gazeti la The Sun, toleo lao lililotoka kwenye siku ya kufungua zawadi au Boxing Day, kulikuwa na stori nzuri sana ya kiungo wa Southampton, Adam Lallana.
Lallana amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu kwenye kikosi cha Southampton na jambo hilo limemfanya aitwe mara mbili kuichezea timu ya taifa ya England chini ya kocha Roy Hodgson.
Stori iliyobebwa na gazeti hilo ni ile ya harusi ya staa huyo, ambaye aliamua kufanya harusi ya gharama ndogo sana sababu ikiwa ni fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika baadaye mwaka huu huko Brazil.
Staa huyo amebadili jambo kubwa kwenye maisha yake baada ya kuoa kwa siri ili kuwa tayari kwa ajili ya fainali hizo.
Kwenye ukurasa huo wa mbele kulikuwa na kichwa cha habari “Nimeoa kwa ajili ya Brazil”, ikifichua harusi ya staa huyo ambayo awali ilipangwa kufanyika siku ambayo England itamenyana na Italia kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Katika kuondoa utata, staa huyo mwenye umri wa miaka 25, amemwoa kwa siri mrembo Emily Jubb, kwenye harusi iliyowagharimu pesa kidogo sana huko Peele, Dorset na sasa yupo huru kufikiria jambo moja tu, fainali za Kombe la Dunia.
Kombe la Dunia latibua
Kwa vyovyote itakavyokuwa, Juni 14, 2014, ingekuwa siku yenye kumbukumbu ya kipekee kwa staa wa Southampton, Adam Lallana na mchumba wake, mrembo Emily.
Kama ataendelea na kiwango chake cha sasa, kiungo huyo atakuwa na nafasi kubwa ya kujumuishwa kwenye kikosi cha kocha Roy Hodgson cha England kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Siku hiyo, England itacheza mechi yake ya kwanza kwenye fainali hizo kwa kumenyana na Italia uwanjani Arena Amazonia huko Manaus. Siku kama hiyo, staa huyo na mchumba wake, Emily walipanga kuoana.
Jambo hilo likaibua mjadala baina yao, itakuwa vipi kama akitajwa kwenye kikosi cha England kwa ajili ya fainali hizo.
Awali, Lallana alikuwa tayari kuahirisha harusi yake na kwenda Brazil kwanza na kisha akirudi ndiyo amwoe mrembo Emily, ambaye alidumu naye kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa miaka saba.
Mwaka 2012, Lallana alimchumbia Emily, kipindi hicho mwanamke huyo alikuwa mjamzito wa mtoto wao wa kwanza wa kiume, Arthur, mwenye mwaka mmoja kwa sasa na hapo wakapanga wafunge ndoa rasmi, Juni 14 mwaka huu.
Lakini, fainali za Kombe la Dunia zikatibua, Juni 14, England itacheza na Italia na kama staa huyo atakuwa kwenye kikosi basi atakuwa yupo Brazil na harusi isingefanyika tena.
Mrembo Emily akubali matokeo
Mrembo Emily anafahamu umuhimu wa siku hiyo, lakini kutokana na kiwango cha mpenzi wake kwa sasa kwenye kikosi cha Southampton, ambapo anatumika kama nahodha, akichaguliwa kwenda Brazil itakuwa zawadi kubwa zaidi kwao na ndiyo maana alikuwa tayari harusi yao isogezwe mbele hadi fainali hizo zitakapokwisha.
Lakini, kwa sababu Lallana alihitaji kuwa na Emily kwanza, akaamua afunge naye ndoa ya siri kwenye usiku wa Sikukuu ya Krismasi na Emily kakubaliana na hali halisi ili kumpa nafasi kubwa mumewe afanye maandalizi ya kutosha kwa ajili ya fainali hizo za Brazil.
“Kwa sasa sijui kitu hadi hapo kikosi kitakapotajwa. Lakini ni aina fulani ya tatizo lenye kuvutia,” anasema Lallana.
“Hivyo ndivyo mimi na Emily tunavyoisubiria siku yetu. Si kila mtu atasema amecheza fainali za Kombe la Dunia, hivyo si kitu cha ajabu kuahirisha harusi kwa ajili ya hilo.
“Nina imani hili limeshatokea miaka ya nyuma na nafahamu itatokea tena. Mimi na Emily tumezungumza juu ya hilo. Anaunga mkono na mimi nafarijika kwa hilo. Kwa kifupi tu, nimekuwa kwenye mwaka mzuri sana kwenye timu yangu. Tumecheza vizuri msimu huu na nadhani tumefika kwenye kiwango tofauti.”
Harusi yao yagharimu Sh1.3 milioni
Inawezekana kuwa ni harusi ya gharama ndogo zaidi kuwahi kufanywa na mastaa. Kwa sababu ilikuwa ni sherehe za siri, Harusi ya Lallana na Emily iliwagharimu Pauni 500 tu sawa na Sh 1,299,800 za Kitanzania.
Staa huyo wa Southampton alizungumza na mpenzi wake na kuamua kufanya sherehe hizo siku ya Krismasi ili kumaliza tatizo hilo na kuwa huru kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia.
Wawili hao wamekuwa pamoja kwa miaka saba, alikula viapo vya ndoa kwenye usiku wa Krismasi huko Poole, hafla iliyohudhuriwa na marafiki wachache na ndugu wa karibu wa familia hizo.
Sherehe hiyo iliyofanyika kwa dakika 30 ilimshuhudia Lallana akiwa kwenye suti ya ‘daki bluu’ huku Emily akiwa amevaa gauni la pinki na walionekana kuwa na furaha kubwa licha ya kwamba haikuwa siku yao ya harusi waliyoipanga awali.