SPOTI DOKTA: Utamu wa Mkude uko hapa

Muktasari:
- Spoti Dokta ilitoa makala kipindi hicho kuonyesha kuwa kitendo cha Yanga kumbeba kiungo huyo kilikuwa ni cha kitaalamu cha benchi la ufundi kuona mbali katika majukumu ya klabu hiyo.
Wakati Jonas Mkude anatua Yanga 2023 akitokea Simba ambayo aliitumikia kwa kipindi cha miaka zaidi ya miaka 10 ilionekana kuwa zama zake zimekwisha.
Spoti Dokta ilitoa makala kipindi hicho kuonyesha kuwa kitendo cha Yanga kumbeba kiungo huyo kilikuwa ni cha kitaalamu cha benchi la ufundi kuona mbali katika majukumu ya klabu hiyo.
Waliona kuwa pamoja na umri wa Mkude kuwa mkubwa na huku akiwa ametumika sana katika klabu ya Simba na timu ya Taifa angeweza kuwafaa.
Wengi walidhani umri wa mchezaji huyo wa miaka 31 sasa kuwa umekwenda kucheza soka, lakini asingeweza kuonyesha makali yoyote akiwa Yanga.
Pamoja na umri kwa mwanasoka huo ni mkubwa lakini utimamu binafsi wa mwili ni moja ya vitu vinavyoweza kumbeba mchezaji katika kucheza soka.
Ukiacha mechi mbalimbali za ligi alizocheza vizuri lakini katika mechi dhidi ya Mamelod Sundowns kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, hususa iliyochezwa Dar es salaam, Mkude alionyesha uwezo mkubwa.
Kiungo huyo alikuwa msaada mkubwa ambao katika mchezo huo yanga ilikuwa inawakosa wachezaji wake nyota watatu muhimu ikiwamo Pacone Zouzoua na Khalid Aucho. Mkude aliweza kucheza soka la hali ya juu katika eneo la kiungo ambalo huwa linahitaji mchezaji aliyekamilika ikiwamo kuwa na kasi, nguvu, kunyumbulika na ustahilivu dhidi ya rafu mbaya za wapinzani.
Katika mchezo huo umri kuwa mkubwa na kuwahi kutumika sana kulionekana si lolote, bali kipaji binafsi pamoja na utimamu wa mwili ili kuweza kucheza.
Wachezaji vijana wachache wa aina hiyo ambao wanaendelea kufanya vizuri katika soka la Bongo hasa ukizingatia yupo katika nchi ya dunia ya tatu ambayo ulinzi wa majeraha bado unakwamakwama kutokana na gharama kubwa za mifumo hiyo kimataifa.
UTIMAMU WANASOKA WENYE UMRI MKUBWA
Ukimkuta mwanasoka mwenye umri mkubwa aliyetumika sana kama Mkude kinachowabeba ni utimamu binafsi na kudumu kwa kiwango cha juu.
Wanasayansi wa fiziolojia wanaeleza kuwa utimamu wa mwili unahusisha utendaji wenye ufanisi usio na shaka wa moyo na mapafu, pamoja na misuli na mifupa ya mwili. Kila kinachofanyika mwilini kinaathari pia kwa tunachoweza kufanya na akili. Utimamu unachochea ubora wa akili na uimara wa hisia za mwili.
Ndio maana mchezaji mwenye utimamu wa mwili anatakiwa pia kuwa na utimamu wa akili. Ikitokea utimamu wa mwili ukayumba anaweza pia kuteteresha afya ya akili na kumpa hisia hasi. Kuwa na utimamu uliothabiti unaweza kuboresha afya ya ubongo, kusaidia kudhibiti uzito, kupunguza hatari ya kupata magonjwa, kuimarisha afya ya mifupa na misuli na kuongeza uwezo kufanya majukumu au kazi za kila siku.
Mchezaji mwenye bidii na kujituma katika mafunzo na mazoezi ya kati mpaka yale makali anapata faida kubwa zaidi katika utimamu wa mwili ukilinganisha na mchezaji mvivu.
Hapa tunapata picha kuwa utimamu wa mwili kwa mwanasoka haupatikani tu kirahisi rahisi, bali inahitajika kuwa na nidhamu ya mazoezi ya kujenga afya ya mwili.
VITU VINAVYOBEBA UTIMAMU WA MWILI
Kuna mambo kadhaa katika utimamu wa mwili ambayo ni pamoja na ustahimilivu wa moyo na mzunguko wa damu, uimara na ustahimilivu wa misuli na mifupa, unyumbulikaji na vitu vilivyomo ndani ya mwili.
Vilevile kuna kujimudu katika mhimili wa mwili, uratibu, kukimbia, nguvu, kasi na maamuzi na kutenda kwa wakati
Moyo na mishipa ya damu yenye afya ndio inatuwezesha kuwa na utawanyaji wa damu yenye oksijeni na sukari kwa ufanisi katika misuli ambayo ndio inahitajika kwa mwanasoka kutumika kufanya kazi.
Misuli na mifupa ni lazima iwe imara na uwezo wa kufanya kazi kwa kipindi kirefu pasipo kuchoka kirahisi. Utimamu wa viungo hivi ndio pia unamfanya mchezaji kutopata majeraha kirahisi.
Unyumbulikaji yaani flexibility ni uwezo wa viungo vya mwili kufanya mijongeo mbalimbali katika uelekeo chanya kupitia maungio ya mwili ikiwamo ungio la goti, kifundo, nyonga, kiganja, kiwiko na bega.
Mfano uwezo wa mchezaji kupiga chenga kwa ufanisi na kuwatoka wapinzani ni lazima awe na utimamu wa maungio haya. Mchezaji anahitajika kuwa na mazoezi bora ya viungo ilia kunyumbulika.
Ndani ya mwili kuna vitu ambavyo lazima viwepo katika kiwango kinachotakiwa kitabibu ili kutimiza utimilifu wa mwili ikiwamo kiwango sahihi cha mrundikano wa mafuta.
Uwepo wa mrundikano mkubwa wa mafuta maana yake ni kuwa na uzito uliokithiri au unene. Mchezaji mwenye utimamu wa mwili huwa na kiwango cha mrundikano wa mafuta kinachokubalika.
Wachezaji hupimwa afya na kutathiminiwa kiwango cha mafuta ya mwili kwa kukokotoa uwiano wa uzito na urefu kitabibu hujulikana kama Body Mass Index (BMI), kupimwa mzunguko wa tumbo na paja.
Uwezo wa kujimudu katika mhimili wa mwili dhidi ya kani ya uvutano. Utimamu wa mfumo wa fahamu na misuli na mifupa ndio unaweza kuutuliza mwili katika mhimili wake bila kuyumba yumba. Uwezo wa kuratibu viungo vya mwili na matendo yake, mchezaji timamu anatumia ogani za fahamu kwa ufanisi ikiwamo macho na masikio hatimaye kutafsiri na kufanya vitendo sahihi.
Mfano mchezaji timamu atasikia mwito na kuona hatimaye kupiga au kutoa pasi mahali sahihi. Mfumo wa fahamu ndio unaratibu mambo haya.
Nguvu kwa mwanasoka ndio msingi wa kuweza kufanya matendo mbalimbali ikiwamo kukimbia kwa kasi kupiga mashuti na kukaba kwa nguvu.
Mchezaji mwenye utimamu anakuwa na nguvu za kutosha na hatimaye kuweza kutoa msukumo au shinikizo kubwa katika kukabana, kusukumana, kupiga au kukimbia kasi katika kukaba au kushambulia.
Kukimbia haraka kirahisi, ni uwezo wa mchezaji kuukimbiza mwili wake na huku pia akiwa katika uelekeo sahihi wakati wa kutii msisimko wa mwili wake.
Kuamua na kutenda kwa wakati, mchezaji mwenye utimamu wa mwili hufanya maamuzi kwa wakati na kutenda haraka kwa usahihi
Mfano mchezaji anapoondosha mpira unaokaribia kuingia golini kwao, ni kitendo kinachohitaji maamuzi ya haraka na sahihi pasipo kujifunga.
Kasi ni moja ya matokeo makubwa ya mwanasoka mwenye utimamu, ni hali ya kuweza kukimbia umbali fulani kwa muda mfupi. Mabeki wa pembeni na mawinga ndio mfano hali wa kasi.
FAHAMU HILI
Mienendo na mitindo mizuri ya kimaisha, utulivu wa kiakili, kula lishe bora iliyozingatia ushauri wa mtaalamu lishe, kupumzika na kulala saa nane kwa usiku mmoja na kuburudika kiakili vinachangia kuwa timamu.