Spier awaita mashabiki Gor uwanjani

Wednesday April 27 2022
Gor PIC

KOCHA wa Gor Mahia, Andreas Spier.

By Sinda Matiko

KOCHA wa Gor Mahia, Andreas Spier amewaomba mashabiki wa klabu hiyo kuwaiga wenzao wa AFC Leopards kwa namna wanavyoisapoti timu yao.

Kuelekea Mashemeji derby itakayopigwa Mei 8 katika uga wa Jomo Kenyatta, Kisumu, kocha Spier anawasihi sana mashabiki wao kuanza kuhudhuria mechi zao kabla ya ngoma hiyo.

Kwa miaka zaidi ya mitano, Gor imekuwa ikishuhudia ushabiki mkubwa mno kwenye mechi zao.

Hata hivyo toka tukio la Covid-19, kiwango cha mashabiki wanaohudhuria mechi zao kimeshuka mno. Siku hizi ni mashabiki wachache mno hushuhudiwa kwenye mechi za Gor. Baadhi ya mashabiki wengine wameonyesha kupoteza imani waliyokuwa nayo na timu yao ambayo kwa msimu wa pili mfululizo, hawaonekani kuwa na uwezo wa kutwaa kombe la ligi kuu.

Lakini wakati Gor wakitorokwa na mashabiki wao, Mashemejio Ingwe, ndio kwa sasa timu inayoshuhudia ushabiki mkubwa sana hasa kwenye mechi zao za Nairobi.

Licha ya kuwa wanakama nafasi ya 10, Ingwe imeweza kuwarejesha asilimia kubwa ya mashabiki wake uwanjani. Hili linaaminika kuchangiwa sana na uhamasishaji wa kocha Patrick Aussems.

Advertisement

Kando na uhamasishaji wa Aussems anayefahamika kwa matumizi yake ya mitandao, pia aina ya soka wanalopiga Ingwe, limekuwa la kuvutia sana na ndio sababu ya mashabiki wa Ingwe kuongezeka uwanjani.

Hii ndio taswira anayotamani kuiona kocha Spier kutoka kwa mashabiki wa Gor kuelekea Mashemeji derby yao itakayochezewa kwenye kitovu cha ushabiki wa Kogallo.

“Nawarai sana mashabiki wetu kuanza kufurika uwanjani. Tunahitaji sapoti yao sana kisaikolojia na tunaihitaji hata wakati huu. Tukiwa na mechi moja kabla ya Mashemeji Derby, watatutendea haki ikiwa watafuruka uwanjani angalau itupe morali ya kumaliza msimu kwa kishindo,” anasema Spier.

Tayari uongozi wa Gor umeanza uhamasishaji wa kuwarejesha mashabiki wao uwanjani. Lengo lao ni kuhakikisha uwanja huo wa Kisumu uliokarabatiwa unafurika pomoni. Uwanja huo unaweza kupakia watu 30,000 baada ya kufanyiwa ukaratabati.

“Tutakita kambi Kisumu baada ya mchuano wetu wa Mei 1, dhidi ya Kariobangi Sharks kwenye uwanja huo. Hii ni mechi kubwa sana kwetu na ni muhimu tuwe karibu na mashabiki wetu. Isitoshe pia ni karibu sana na kitovu cha mashabiki wa Mashemeji zetu hivyo tumewarahisishia kazi,” anasema Katibu Mkuu wa Gor, Sam Ocholla.

Advertisement