SMG aukubali mziki wa U20

Tuesday May 04 2021
smg pic
By Ramadhan Elias

UNAAMBIWA huko kwenye Ligi Kuu ya Vijana U-20, sio mchezo kwani mtu akizubaa tu inakula kwake huku, Kocha Mkuu wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ kukiri mambo ni magumu.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars anakinoa kikosi hicho cha Yanga U20, ameukubali mziki wa ligi hiyo akidai timu zote zimejipanga na wachezaji wenye vipaji wanajiachia na kuvurana kinoma.

Akizungumza na Mwanaspoti juu ya ligi hiyo inayozidi kushika kasi, SMG alisema; “Huku ni kugumu aisee, soka siku hizi limekuwa na kila timu imejipanga vyema sio kama zamani ambapo timu chache ndio zilikuwa na akademi bora.”

“Kwa sasa huwezi kujua unashinda kabla ya mchezo maana kila dakika 90 unazokutana nazo zinakuwa ngumu, lakini pamoja na yote hayo namshukuru Mungu tunaendelea vizuri na vijana wangu wanajua wanachokitafuta,” aliongeza SMG.

Yanga U-20 iliyopo kwenye kundi A imecheza jumla ya mechi 6 ikishinda tatu dhidi ya Namungo 2-0 mara mbili, na 2-1 kwa Coastal Union, ikipata sare ya 1-1 mbele ya Ruvu Shooting na kupoteza 3-1 dhidi ya Azam na 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania. hadi tunaingia mitamboni Yanga ilikuwa dimbani ikicheza na Coastal Union mchezo wa marudiano.

Advertisement