Prime
Siri imefichuka! Kilichomng’oa Dube chatajwa
KUNA nyakati kwenye soka fedha hushinda kila kitu lakini zipo nyakati nyingine ambazo pia maamuzi makubwa hayafanywi kwa kuangalia mkwanja uliopo mezani ila ni kutokana na kile ambacho kipo moyoni.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Prince Dube. Wakati vigogo wa soka Afrika wakivutana kuwania saini yake huku mezani kukiwa na ofa za zaidi ya Sh2 bilioni kwa pamoja kutoka Libya, Afrika Kusini na Tanzania, mshambuliaji huyo wa Zimbabwe alifanya uamuzi ambao haukutegemewa na wengi.
Badala ya kuendelea kutafuta mafanikio katika ligi zenye ushindani mkubwa na mishahara minono, Dube amegeuza usukani na kurejea nyumbani Zimbabwe ambako amesaini mkataba wa miaka miwili na Hardrock FC.Kwa wengi ulikuwa uamuzi wa kushangaza. Kwa wanaomfahamu kwa karibu ulikuwa uamuzi ambao alikuwa ameubeba moyoni muda mrefu.
Mwanaspoti imebaini kuwa nyuma ya uamuzi huo kulikuwa na sababu zilizokuwa nzito kuliko fedha.
FAMILIA IMESHINDA
Wakati Al Ittihad ya Libya ikimwekea mezani ofa ya zaidi ya Sh1 bilioni na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ikifuata kwa ofa inayokadiriwa kufikia Sh950 milioni huku Yanga nayo ikifanya juhudi za mwisho kumbakisha kwa mkataba mpya wenye maslahi makubwa, Dube alikuwa na mawazo tofauti.
Vyanzo vya karibu na mshambuliaji huyo vimeiambia Mwanaspoti kuwa baada ya miaka sita ya kucheza nje ya Zimbabwe alipoondoka 2020 na kutua Tanzania katika kikosi cha Azam kisha Yanga, mshambuliaji huyo alihitaji kurejea nyumbani ili kuwa karibu na familia yake na kuanza maisha mapya akiwa karibu na watu wake.
“Fedha ni nzuri sana lakini wakati mwingine kuna mambo ambayo hayawezi kununuliwa kwa pesa. Prince aliona umefika wakati wa kurudi nyumbani. Alihitaji utulivu wa maisha na kuwa karibu na familia yake. Hilo ndilo lililobeba uamuzi wake,” kilisema chanzo. Wakati familia ikipewa uzito mkubwa katika hilo, lakini inaelezwa uongozi wa Yanga ulikuwa kama haujafikia muafaka wa kumpa mkataba mshambuliaji huyo ambaye mwenyewe aliona bora afanye uamuzi wa haraka kabla ya mambo hayajawa mabaya kwake.
MSIKIE ANACHOSEMA
Baada ya kutambulishwa rasmi na Hardrock FC, Dube hakuwasahau viongozi na mashabiki wa Yanga waliompa sapoti kubwa katika kipindi chake cha misimu miwili.
“Ninawashukuru viongozi na mashabiki wote wa Yanga kwa upendo, sapoti na namna walivyonifanya nijisikie nyumbani tangu siku yangu ya kwanza,” amesema mshambuliaji huyo na kuongeza;
“Nimefurahia kuvaa jezi ya klabu hii kubwa na nitabaki na kumbukumbu nzuri maisha yangu yote. Nawataka waendelee kuiunga mkono timu yao na nawatakia mafanikio makubwa siku zijazo.”
SASA ITAKUWAJE?
Kwa mtazamo wa kawaida, unaweza kusema Yanga imepoteza mshambuliaji aliyekuwa na uhakika wa kufunga mabao yasiyopungua 10 kila msimu. Lakini ukiangalia kwa undani, utaona imepoteza silaha muhimu.
Dube hakuwa mshambuliaji wa kusimama ndani ya boksi kusubiri mipira pekee. Alikuwa na uwezo wa kucheza kama namba tisa lakini pia alitokea pembeni, hasa upande wa kushoto, akitumia nguvu na kasi kuingia katikati na kumalizia mashambulizi.
Kila Yanga ilipohitaji kubadilika kimfumo kutoka kutumia mshambuliaji mmoja hadi wawili, Dube alikuwa suluhisho. Alicheza sambamba na Clement Mzize kabla ya kuumia na msimu huu kuna nyakati alicheza pamoja na Laurindo Aurelio ‘Depu’.
Ilipohitajika timu kushambulia kwa mipira ya kushtukiza, Dube alimudu hilo. Ilipotakiwa kujenga mashambulizi kwa pasi fupi kutoka nyuma, pia alishuka chini kuchukua mipira na kushiriki katika ujenzi wa mashambulizi.
Akizungumzia ubora wa Dube, aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema mshambuliaji huyo ni wa kisasa mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja na anayewapa makocha uhuru wa kubadili mfumo wa mchezo bila kulazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji.
“Dube ni mshambuliaji anayefanya kazi kubwa kuliko kufunga mabao pekee. Ana nguvu, analinda mpira vizuri, anajua kucheza akiwa mgongo umeelekea langoni na anaweza kutokea pembeni au katikati. Wachezaji wa aina hiyo si rahisi kuwapata kwa sababu wanatoa chaguo nyingi kwa kocha ndani ya mchezo mmoja,” amesema kocha huyo ambaye kwa sasa yupo Ghana.
Kuondoka kwa Dube kunailazimisha Yanga kufanya maamuzi mapya katika dirisha lijalo la usajili.
Kwa sasa timu hiyo imesalia na washambuliaji watatu. Mmoja wao ni Depu ambaye pia alikuwa akitajwa huenda akaondoka kutokana na kukosa nafasi ya kutosha, hasa baada ya Yanga kuachana na aliyekuwa kocha wake, Pedro Goncalves.
Hata hivyo, katika mechi za mwisho wa msimu alionekana kurejea kwenye ubora baada ya kufunga mabao matatu katika mechi tano za mwisho za Yanga katika mashindano yote. Washambuliaji wengine ni Clement Mzize ambaye anatarajiwa kurejea kikosini msimu ujao baada ya kukosa sehemu kubwa ya msimu uliomalizika kutokana na majeraha huku Emmanuel Mwanengo akibaki kuwa chaguo lingine licha ya kushindwa kupata nafasi ya kutosha tangu alipojiunga na timu hiyo.
TIMU ALIYOTUA
Hardrock FC yenye maskani yake Kwekwe, inashiriki Ligi Kuu ya Soka ya Zimbabwe (ZPSL) msimu huu baada ya kupanda daraja iliposhinda ubingwa wa Kanda ya Kati. Kwa sasa Hardrock inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Zimbabwe inayoendelea baada ya kucheza mechi 19 ikikusanya pointi 38, ikizidiwa tano na kinara Scottland FC yenye 43 ikicheza mechi 20. Ligi Kuu Zimbabwe inashirikisha timu 18, hivyo Hardrock imebakiwa na mechi 15 kuhitimisha msimu.