Singida wana mkali kuliko Tambwe

KOCHA Hans Pluijm ndiye aliyemrejesha Amissi Tambwe kwenye makali yake baada ya kumnasa alipotemwa na Simba kwa madai ameisha na kazi aliyoifanya kila mmoja anaijua, sasa Mzungu huyo amepanga kumuibua mkali wa Tambwe.
Pluijm anayeinoa Singida United, aliliambia Mwanaspoti kuwa, anamtengeneza straika mwingine mkali wa mabao ndani ya Singida United, ambaye atamfunika vibaya Tambwe.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa Yanga kwa mafanikio alisema kuwa, Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Rwanda, Danny Usengimana ndiye anamwandaa kuwaliza vigogo wote wanaotamba katika soka la Tanzania kwa kuchana nyavu.
Wakati Pluijm akitamka hayo, Usengimana kwa sasa amekuwa akichunguza nani ni mkali wa kutikisa nyavu ambaye anaweza kumpa changamoto katika kuwania Kiatu cha Dhahabu ambacho amewahi kukitwaa mara mbili mfululizo katika ligi ya kwao.
Msimu uliopita Simon Msuva na Abdulrahman Musa walifunga mabao 14 kila mmoja huku Tambwe, Obrey Chirwa, Mbaraka Yusuph wakifuatia nyuma yao.
Pluijm alisema anaamini Usengimana atawasumbua sana mastraika wengine kwa kuwa kama alivyomweka Tambwe matawi ya juu ndivyo anavyoamini kwa Mnyarwanda huyo, huku akisisitiza lazima azilize Simba na Yanga sana tu.
Yanga na Singida kesho Jumamosi zitapimana nguvu katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Pluijm amesema haimpi shida kwani anawafahamu Yanga vizuri ikiwa ni pamoja na mbinu za kocha Mzambia, George Lwandamina na hata usajili wa nyota wao anaufahamu vizuri.
“Kikosi changu kitazisumbua sana hizi timu kongwe ambazo zinajiona ndizo vinara wa soka nchini, tukiwakosa kuwafunga kwenye mechi za kirafiki basi kwenye ligi lazima tuwafunge na atakayewaliza ni Danny,” alisema Pluijm.
Pluijm alisema kuwa ubora wa kikosi hautokani na usajili bora pekee bali kipato cha timu walichonacho kwa kupata wadhamini wengi ambao, wanawawezesha timu kutokuwa na njaa kwa wachezaji.
Jana Alhamisi, Singida United iliingia mkataba wa udhamini na Kampuni ya YARA Tanzania yenye makao makuu nchini Norway, inayojihusisha na masuala ya kilimo ambapo imetoa zaidi ya Sh 250 milioni pamoja na vifaa kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Huu ni udhamini wa sita kwa Singida United ambapo awali wamesaini mkataba na Sportpesa, Kampuni ya mafuta ya Puma, Benki ya NMB, Halotel na Oryx.
Usengimana aapa
“Ninapojiandaa kwa msimu huwa naweka malengo ya kuwa mfungaji bora, nimefika hapa na nimeuliza ni wachezaji gani wanaofunga mabao mengi ili nijue napambana nao vipi. Nimewafhamu na nimejipanga na nataka Kiatu cha Dhahabu. Kocha amenipa mbinu za kufunga na wenzangu tunashirikiana vizuri sana ili tupate mabao mengi. Ila nina hofu na viwanja vibovu na hizi safari za umbali mrefu zinachosha sana,” alisema Usengimana.