Singida FG, Mtibwa mechi ya wanyonge

Aziz Andambwile (Singida Fountain Gate)
Muktasari:
- Singida itakuwa nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuwaalika Mtibwa Sugar katika mchezo utakaopigwa saa 10:00 jioni ambao unatarajia kuwa mkali kutokana na matokeo mabovu ya hivi karibuni kwa timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara.
Mwanza. WAKATI kesho Singida Fountain Gate ikiikaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu, itakuwa kwenye presha kubwa ya kumaliza ukame wa kutopata ushindi miezi mitatu, huku wageni wao nao wakisaka pointi tatu za kwanza baada ya miezi miwili.

Juma Liuzio (Mtibwa Sugar)
Singida itakuwa nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuwaalika Mtibwa Sugar katika mchezo utakaopigwa saa 10:00 jioni ambao unatarajia kuwa mkali kutokana na matokeo mabovu ya hivi karibuni kwa timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara.
Wenyeji hawajapata ushindi katika ligi hiyo tangu Novemba 27, mwaka jana walipoifunga Coastal Union kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Liti mjini Singida, huku wageni wao wakiwa hawajavuna pointi tatu tangu Desemba 19, mwaka jana walipoichapa Mashujaa kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Kocha Msaidizi wa Singida Fountain Gate, Nizar Khalfan amesema kurejea wachezaji Dickson Ambundo, Yusuph Kagoma, Amos Kadikilo na Abdulmajjid Mangalo kumewaongezea nguvu na wana matumaini kesho ndiyo utakuwa mchezo wa safari ya matumaini kwani wamefanya maandalizi mazuri na wamerekebisha makosa yaliyowagharimu kwenye kichapo dhidi ya Azam.
“Kitu kikubwa ambacho kinatupa matumaini mpaka sasa timu yetu imeanza kucheza vizuri. Hata juzi dhidi ya Azam tumecheza vizuri japokuwa hatukupata ushindi, lakini ni mwanzo mzuri. Naamini mechi ya kesho tutapata matokeo na ndiyo itakuwa mwanzo wa ushindi wetu,” amesema Khalfan na kuongeza kuwa:
“Mechi iliyopita tulikuwa na shida kufika eneo la mbele hilo tumeliona jana. Tumelizungumza na tumelifanyia marekebisho madogo na leo nadhani tutalirekebisha tena. Naamini kesho tutaingia vizuri watu wataona mabadiliko ya mechi iliyopita na kesho. Watu wa Mwanza wametupokea vizuri na mpaka sasa hatujawafurahisha tunawaomba kesho waje tutawafurahisha.”
Nahodha wa timu hiyo, Beno Kakolanya amesema wachezaji wanaujua umuhimu wa mechi ya kesho na waliongea baada ya mechi iliyopita kupoteza.
"Kwa hiyo tunachoangalia ni kushinda na nguvu zote zinaelekezwa mechi ya kesho. Kila mmoja ana ari na morali kwa ajili ya mchezo huo. Mashabiki wasife moyo na sisi ndiyo tumeanza taratibu na timu imeanza kukaa vizuri,” amesema.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amewaomba mashabiki wa timu hiyo kutokata tamaa kwani kikosi chake kina deni la kuwatafutia matokeo mazuri na kuwafurahisha, huku akiwatoa wasiwasi kwamba wana nafasi ya kufanya vizuri mechi zijazo.
“Ni kweli hatuna matokeo mazuri kipindi hiki. Ukiacha sare ya juzi dhidi ya Dodoma Jiji lakini ni kipindi tu ambacho tunapitia mwalimu au klabu yeyote anaweza kupitia. Kinachotakiwa ni utulivu kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kwa ujumla ili saikolojia zao (wachezaji) zikae sawa na kupata matokeo,” amesema Katwila.
“Utakapokuwa unapata matokeo mazuri nafikiri kila mmoja anapata kujiamini na kufanya vizuri. Kwa hiyo kikubwa ni kuwatuliza tu akili zao kupambana ili kucheza mchezo wetu wa kesho na kupata matokeo.”