Singida FG, Mashujaa zagawana pointi Kirumba

Muktasari:

  • Ni sare ya pili mfululizo kwa timu hizo katika mechi za Ligi Kuu, ambapo mechi zilizopita Singida FG ilitoka sare ya 1-1 na Ihefu huku Mashujaa ikiilazimisha Azam FC suluhu (0-0).

Mwanza. Timu za Singida Fountain Gate na Mashujaa FC zimegawana pointi leo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao umemalizika kwa suluhu (0-0) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mchezo huo ambao umepigwa leo Aprili 21, 2024 kuanzia saa 10:00 jioni, ni wa pili msimu huu kwa timu hizo kukutana ambapo mchezo wa mzunguko wa kwanza ulipigwa Novemba 6, 2023 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Singida FG ikishinda mabao 3-1.

Suluhu hiyo ni ya pili mfululizo kwa timu zote mbili, ambapo mechi zilizopita Singida FG ilipata sare ya 1-1 mbele ya Ihefu huku Mashujaa ikitoka suluhu (0-0) na Azam FC.

Kwa matokeo hayo, Singida FG inafikisha alama 26 katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi, ikipoteza mechi 10, sare nane na kushinda sita, huku Mashujaa ikifikisha pointi 23 kwenye nafasi ya 14 ikipoteza mechi 11, sare nane na kushinda tano.

Wenyeji Singida wameendelea kutokuwa na bahati na Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa ambapo leo wamecheza mchezo wa tano wa ligi na kushinda mmoja pekee dhidi ya Namungo huku ikipoteza kwa Yanga, Azam na Mtibwa na sare dhidi ya Mashujaa.

Pia imecheza mechi mbili za Kombe la Shirikisho uwanjani hapo ikiifunga FGA Talents mabao 2-1 na kubamizwa mabao 3-0 na Tabora United ikitupwa nje ya mashindano hayo hatua ya 16 bora.

Ni mchezo wa tatu mfululizo kwa Benedict Haule akiidakia Singida FG baada ya kipa namba moja, Beno Kakolanya kudaiwa kutoroka kambini, ambapo alidaka dhidi ya Yanga na kuruhusu mabao 3-0, sare ya 1-1 na Ihefu na leo amevuna 'clean sheet' kwa kutoruhusu bao dhidi ya Mashujaa (0-0).

Kocha wa Singida FG, Ngawina Ngawina amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri licha ya kutopata ushindi, huku akilia na changamoto ya umaliziaji nafasi ambayo ameahidi kwenda kuifanyia kazi ili kupata matokeo mazuri mchezo ujao.

Naye, Kocha Msaidizi wa Mashujaa, Makatta Maulid amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo akiahidi kwamba hawatoshuka daraja kwani watapambana kadri ya uwezo wao ili kutoka nafasi za mkiani kwenye mechi zijazo.