Simbu avaa ubalozi wa matibabu Fistula

Mwanariadha Alphonce Simbu akionyesha fulana na medali kwa ajili ya mbio za Fistula Marathon zinazolenga kutoa elimu ya ugonjwa huo namna ya kujikinga, na pia  upatikanaji wa fedha za matibabu bure. Katikati ni mkurugenzi wa Martenity Africa wanaotoa huduma hizo, Michael Hunds na katibu wa Shirikisho la Riadha Mkoa wa Arusha, Rogert Steven.

Muktasari:

  • Msimu wa tatu wa Fistula Marathon unatarajiwa kufanyika Mei 24, 2024 jijini Arusha kwa ajili ya kusaidia utoaji elimu juu ya ugonjwa huo, kuwa unatibika lakini pia kusaidia upatikanaji wa fedha za matibabu kwa zaidi ya wanawake 250 wanaojitokeza wenye matatizo ya ugonjwa wa fistula ya uzazi.

Mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania, Alphonce Simbu anatarajia kuongoza zaidi ya wanariadha 600 nchini kushiriki mbio za Fistula Marathon kwa ajili ya kutoa elimu na kuchangisha fedha za kutibu wanawake waliokumbwa na ugonjwa huo kipindi cha uzazi.

Mbio hizo msimu wa tatu, zinatarajia kufanyika Mei 24, 2024 jijini Arusha kwa ajili ya kusaidia utoaji elimu juu ya ugonjwa huo kuwa unatibika lakini pia kusaidia upatikanaji wa fedha za matibabu kwa zaidi ya wanawake 250 wanaojitokeza wenye matatizo ya ugonjwa wa fistula ya uzazi.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Machi 4, 2024, meneja wa mbio hizo, Doreen Moshi alisema zitashirikisha wakimbiaji 600 katika umbali wa kilomita tano, 10 na 21 na zinatarajiwa kufanyika jijini Arusha siku moja baada ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Ugonjwa wa Fistula duniani.

Amesema lengo kubwa la Taasisi ya Martenity Afrika kuandaa mbio hizo ni kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo lakini pia jinsi ya kutibiwa ili kuwaweka wanawake salama dhidi ya uzazi.

"Taasisi yetu tunatoa elimu na matibabu ya ugonjwa wa fistula lakini pia huduma ya uzazi kwa wanawake wenye hali duni kiuchumi bure kuanzia malazi, chakula na usafiri kufuata tiba wanapotoka nyumbani au mikoani," amesema Doreen. 

Mkurugenzi wa Martenity Afrika, Michael Hunds alisema kuwa wamefikia hatua ya kutoa huduma hizo bure baada ya kuona wanawake wengi wajawazito wanapata ugonjwa wa fistula wakati wa kujifungua ambao ni zaidi ya 3000 kila mwaka huku wanaojitokeza kupata tiba ni 1300 pekee.

"Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 10,000 hadi 20,000 wanaishi na ugonjwa huo huku zaidi ya wanawake 3000 wanaugua kila mwaka lakini zaidi ya 700 wanajificha wakidhani ugonjwa huo ni wa aibu na fedheha lakini sio kweli kwani unatibika na sisi tunasaidia bure," amesema Michael.

Awali, Simbu alisema kuwa wamekuwa wakishiriki mbio nyingi kwa ajili ya kujipatia vipato lakini pia sadaka ni muhimu hasa kusaidia wanawake wanaojifungua kukabiliana na ugonjwa wa fistula. 

"Ugonjwa wa fistula sio kama dada au mama zetu wamependa kupatwa nao, ni katika harakati za kuwaleta wenzetu duniani ambao si ajabu wakaja kuwa wanariadha wazuri baadaye, hivyo tujitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizi ili lengo la matibabu na elimu, litimie na hii ndio itakuwa moja ya sadaka yetu ya kweli kwa Mungu," amesema Simbu.

Simbu anayekimbia mbio ndefu za kilomita 42, ni mmoja wa wanariadha wanne aliofuzu kuwakilisha nchi kwenye Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa Julai mwaka huu, alisema kuwa yeye kama balozi wa kujitolea wa mbio hizo anatarajia kuhamasisha wanariadha wenzake kushiriki na pia klabu yake ya riadha.

"Hili jambo tulivae wote, kuhakikisha wanawake hawa wanapata huduma, naombeni na makocha wenye wakimbiaji wawalete hapa kuhakikisha sadaka hii yenye baraka tunaipata wote," alisema mwanariadha huyo.

Mwenyekiti wa mbio za Fistula Marathon, Isack Shayo alisema ada ya usajili wa kushiriki mbio hizo ni Sh35,000 kwa mshiriki mmoja ambapo atapatiwa fulana na namba ya kukimbilia na siku ya mbio watahudumiwa matunda na maji njiani.

"Mbio zetu zitaanzia kwenye viwanja vya Magereza Kisongo saa mbili asubuhi ambapo washiriki wote watakaomaliza watavishwa medali ya rangi ya dhahabu yenye nembo ya kusaidia wanawake wenye ugonjwa wa Fistula."