Simba yatupwa nje Ligi ya Mabingwa Afrika

SIMBA imeondoshwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu baada ya kuruhusu kufungwa bao 3-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Hiyo ni baada ya kuruhusukufungwa mabao matatu nyumbani na kufanya uwiano wa mabo kuwa 3-3 baada ya kushinda 2-0 ugenini hivyo wameondolewa kwa kanuni ya bao la ugenini.

Kipindi cha kwanza cha mechi hiyo, Simba ilionekana kulishambulia mara kwa mara lango la Jwaneng lakini Ubora wa kipa wao Ezekiel Morake uliifanya Simba kuondoka ba bao moja pekee lililofungwa na Rally Bwalya dakika ya 40.

Bao hilo la Bwalya lilitokana na John Bocco kupiga pasi kwa Bernard Morrison katikati ya Uwanja aliyekimbia na mpira mbele na kupiga pasi mpenyezo kwa Bwallya akapiga chenga mabeki wawili wa Jwaneng na kuingia kwenye boksi kisha kupiga shuti la wastani lililozama nyavuni.

Morrison, Shomari Kapombe, Hassan Dilunga, Bocco, Sadio Kanoute na Bwalya ni miongoni mwa wachezaji wa Simba walioweza kutengeneza nafasi za mabao na kupiga langoni kwa Jwaneng kipindi cha kwanza katika nyakati tofauti lakini kipa Ezekiel akaokoa mashuti yao.

Mphoyamodimo Keiponye na Thabo Leinanyane wote wa Jwaneng ndio wachezaji waliooneshwa kadi za njano katika dakika 45 za kwanza huku kukiwa hakuna kadi nyekundu kwa pande zote mbili.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko, Simba ikimtoa Dilunga na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Banda huku Jwaneng wakiwatoa Themba Dhladhla na Vicent Sesinyi na nafasi zao kuchukuliwa na Tshephang Boithatelo na Rudath Wendell.

Dakika moja baada Wendell aliisawazishia Jwaneng baada ya kupokea pasi akiwa ndani ya boksi la Simba na mabeki kujichanganya kisha kupiga shuti dogo na mpira kuzama wavuni.

Bao hilo liliwaamsha Simba na kuanza kutafuta bao la pili, huku Banda na Morrison wakiongoza mashambulizi  kwa takribani dakika kama tano hivi baada ya kufungwa.

Beki wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea faulo winga wa Jwaneng.

Dakika ya 59 yule yule aliyefunga bao la kusawazisha kwa Jwaneng, Wandell aliifungia bao la pili timu yake na kuongoza kwa bao 1-2.

Bao hilo lilitokana na mpira wa kurusha uliorushwa ndani ya boksi la Simba na kumkuta mchezaji wa Jwaneng aliyepiga pasi ya juu kwa Wandell na kufunga kiulaini baada ya mabeki wa Simba wakiongozwa na Pascal wawa kutegea kuruka.

Kipa Ezekiel wa Jwaneng aliendelea kuokoa michomo kadhihilisha ubora wake kwa kuokoa michomo ya Simba katika dakika ya 59 hadi 68 ambapo Simba walikuwa wakifika langoni kwa Jwaneng mara kwa mara.

Dakika ya 72 Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Morrison na Taddeo Lwanga aliyeumia na nafasi zao kuchukuliwa na Erasto Nyoni na Duncun Nyoni.

Dakika nne baadae Jwaneng walijibu mapigo kwa kuwatoa Luck Mokoena na Resaobaka Thatanyane na kuingia Tebogo Sembowa na Mpho Kgomo.

Banda wa Simba alionekana kupata nafasi mbili ambazo angezitumia vizuri angeipatia Simba mabao lakini alionekana kuwa muoaga na kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwa wakati.

Meddie Kagere wa Simba aliingia uwanjani dakika ya 84 kuchukua nafasi ya John Bocco aliyeumia baada ya kupigwa mpira wa kichwa na dakika moja baadae Gape Mohutsiwa wa Jwaneng aliifungia timu yake bao la tatu na kuifanya itinge hatua ya makundi.