KIKOSI cha Wekundu wa Msimbazi Simba kimewasili salama Jijini Dar es Salaam asubuh ya Leo na kwenda moja kwa moja Bunju kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao wa Kimataifa dhidi ya Al Ahly.
Simba walikuwa Kanda ya ziwa kucheza mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United na kujinyakulia pointi tatu Baada ya kushinda bao 1-0 lililofungwa na Bernard Morrison.
Mara ya mwisho Simba ilipocheza na Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya Makundi Simba alishinda bao 1-0 lililotiwa kimiani na Meddie Kagere katika dimba la Benjamini Mkapa (Zamani Taifa).
Akizungumza na Mwanaspoti Online Nahodha Msaidizi wa Wekundu hao Mohamed Hussein 'Tshabalala' amesema, ya Musoma yameisha sasa wanatizama mchezo wao ujao wa Kimataifa dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Februari 23 katika dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Tshabalala amesema maandalizi yao yako vizuri kuelekea mchezo huo kwani wanatambua ni mchezo mgumu.
"Nafasi ya Simba Klabu bingwa ipo na sisi Kama wachezaji tunajua majukumu yetu tuko tayari kwa mapambano kwani tunatambua Al Ahly ni timu kubwa, "
Aidha Tshabalala amesema, sasa hivi kila mchezaji macho na masikio yake yako katika mchezo huo kwa kuwa ndio unaofuata hivyo watajitahidi kuhakikisha wanatumia vyema uwanja wa nyumbani ili kupata pointi tatu nyingine.
Simba imevuna pointi tatu katika mchezo wa awali dhidi ya As Vita uliopigwa Congo na kushinda bao 1-0, matokeo yaliyoweka historia kwa timu ya Tanzania kushinda katika ardhi ya Nchi hiyo.